Wabunge wetu mko wapi?

UMEPITA mwaka mmoja na miezi mitatu tangu tumefanya uchaguzi mkuu na sasa tumesalia na miaka mitatu na miezi saba mpaka uchaguzi mwingine mwaka 2020.

Wakati wa kampeni za mwaka 2015, wabunge wetu walipata fursa ya kuweka sera zao hadharani ili kutushawishi tuwapigie kura watuongoze katika nchi ya ahadi. Ni imani yangu ili sera za wabunge hawa ziweze kufanikiwa ni dhahiri lazima washirikiane na sisi wananchi.

Swali la msingi baada ya kuwapa kura wabunge wetu leo hii mko wapi mbona hatuwaoni majimboni kwetu?

Nikiri wazi ya kuwa sio wabunge wote ambao hawaonekani majimboni kwao, kuna baadhi ya wabunge wako majimboni mwao wakitenda kazi na jamii zao, ila pia kuna wabunge ambao wao huenda majimboni mwao wakati wa misiba, wakati wa majanga kama mafuriko ama wakisikia ujio wa waziri fulani ndio wao hutokea majimboni mwao.

Kwani wabunge kazi yao ni nini hasa? Je, wabunge hupaswa kwenda bungeni kwa niaba yetu na kuwasilisha shida zilizopo majimboni mwao na kusubiri serikali kutenda ama wanapaswa kutenda zaidi ya hapo?

Kwa mtizamo wangu, nadhani wabunge wana kazi zaidi ya kwenda bungeni kwani wabunge wametokana na sisi wananchi na hivyo ni jukumu lao kama wabunge kuhakikisha wanafanya kazi na wananchi wao na sio kwa niaba ya wananchi wao.

Ni vyema kuelewa kuna tofauti ya wabunge kufanya kazi kwa niaba ya wananchi na kufanya kazi na wananchi. Ni ukweli kwamba kwa muda mrefu wabunge wetu wamekuwa wakitenda kazi zao kwa niaba ya wananchi na sio kufanya kazi na wananchi wao.

Ili maendeleo endelevu na imara yaweze kuletwa na wabunge wetu, ni vyema wafanye kazi na sisi wananchi na sio kwa niaba yetu kwani sisi wananchi tuna majukumu ya kushiriki kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo yetu wenyewe.

Ikumbukwe ya kuwa wabunge ni kiunganishi baina ya wananchi na Serikali na ni muhimu kwa wabunge wetu kutushirikisha kila hatua wanayofanya katika kuleta maendeleo kama walivyoadhidi katika sera zao.

Mantiki ya makala hii ni kueleza yale ambayo wabunge wanapaswa kufanya ili kuleta maendeleo endelevu na sio kubaki kama wawakilishi wetu na kutenda kwa niaba ya wananchi waliowachagua.

Ni ukweli ulio wazi ya kuwa wengi wa wabunge wetu hurudi katika majimbo yao mara kadhaa ila wananchi wanaweza wasitambue ya kuwa wamerudi majimboni mwao na wengine huishia kuwaona wabunge wao wakati wa uchaguzi tu.

Kwa kuwa wabunge wametokana na sisi wananchi ambao tuliwapa ridhaa, ni wazi wanapaswa kuishi katika majimbo yao kwani haileti mantiki yoyote kama tunamchagua mbunge asiyeishi jimboni mwake na kuwa anaishi sehemu zingine.

 Kuwa na wabunge wanaoishi miji mingine tofauti na majimboni mwao ni sawa na kuwa na baba asiyeishi na familia yake huishi kwa jirani halafu huja kuwaona watoto wake pale anapojisikia.

Kwa upande mwingine wabunge wawapo majimboni muda wote kazi yao kubwa sio kukaa ofisini kwani hatukuwachagua ili wakae ofisini bali ofisi zao ni katika mitaa, vijiji ama mijini katika majimbo yao.

 Hapa ningependa kusisitiza ya kuwa, kazi kubwa ya wabunge ni kufanya vikao na wananchi wao ama makundi mbalimbali ya wataalamu katika majimbo yao ili kujua changamoto na maoni ya wananchi wao.

Wabunge wanapaswa kukaa na wananchi katika sehemu mbalimbali za majimbo yao na kutoa mrejesho wa kila hatua wanayopitia katika kuhakikisha sera walizoahidi zinatimia na pia kupata maoni ya wananchi ya namna bora ya kutenda pamoja.

 Ni wazi ya kuwa mara nyingi sera zinazoahidiwa na wabunge hutegemea fedha za serikali ili kuona zinatimia, hivyo serikali ikishindwa kutoa fedha ni wazi sera za wabunge wetu hazitatimia.

Hapa ndio maana nasisitiza ya kuwa maendeleo ya majimbo yanachangiwa na wananchi na sio kuwaachia wabunge watende kwa niaba yetu.

 Wabunge wanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwashirikisha wananchi katika jitihada wanazofanya na kuweka bayana jitihada ambazo zinakwama ila wananchi wanaweza kujituma kuhakikisha wanafikia kile wanachokitaka.

Ni vema nikatoa mfano katika hili. Mimi naishi wilayani Tarime kwa sasa ambako shida kubwa ya wilaya yetu ni maji safi na salama kwani bado asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiii hutegemea maji ya visima vya asili ama vile vya kuchimbwa kwa mikono. Ni watu wachache sana wenye uwezo wa kupata maji ya bomba.

Lakini cha ajabu wilaya hii imezungukwa na mto mkubwa sana ujulikanao kama Mto Mara na pia kwa upande mwingine umezungukwa na Ziwa Victoria ambavyo haviko mbali sana na mji wa Tarime ila vyanzo hivi havitumiki katika kuleta maji safi na salama kwa wananchi wake. Mara nyingi majibu ambayo hutolewa ni kwamba serikali haijatenga fedha.

Hapa tukisubiri serikali itenge fedha kwa ajili ya kuleta haya maji ni ukweli tutasubiri sana. Hapa ndipo tunapopaswa kuona jitihada za mbunge wetu ambapo anapaswa kukaa na wananchi na kuzungumza nasi na tuweze kutoa mapendekezo ya pamoja kuona nini tunaweza kufanya kama wananchi ili kuleta maji.

 Kuwashirikisha wananchi katika maendeleo ni muhimu na umuhimu  huonekana hapa kwani ni wazi mbunge hana uwezo wa kuleta maji kwa jitihada zake bila kushirikiana na sisi wananchi.

Kwa upande mwingine, changamoto nyingi huonekana katika hospitali, shule, kwenye masoko, kwenye vituo vya mabasi ama sehemu zingine muhimu. Ni muhimu kwa wabunge wetu kutembelea sehemu hizi na kujua changamoto zilizopo na kuzitatua kwa kutumia wataalamu wa ndani na kuwashirikisha wananchi badala ya kusubiri serikali na wizara zitende.

Nimalize kwa kusema ya kuwa, uwepo wa wabunge majimboni mwetu sio kushiriki misiba na sherehe tu, bali ni kuwa chachu ya maendeleo majimboni na tena sio kwa kusubiri serikali itoe fedha kwenye kila ahadi ila kwa kuwa chachu kwa wananchi ili washiriki katika kuleta maendeleo yao wenyewe.


*Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii. Anapatikana kwa baruapepe: j_mulikuza2000@yahoo.com na simu +255 786 946 931

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *