Habari
Wadau wamtwisha Kikwete zigo la Pamba
Mwandishi Wetu
Toleo la 244
20 Jun 2012

MSIMU wa ununuzi wa pamba uliotarajiwa kufunguliwa Juni 25, mwaka huu, umeahirishwa kwa muda usiojulikana kufuatia wakulima na wanunuzi wa pamba kushindana bei elekezi.

Akitangaza kuahirishwa kwa msimu huo kwenye Kikao cha Wadau cha kupanga bei, kilichofanyika hapa Jumatatu Juni 18, mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba Dk. Festus Limbu alisema kutokana na pande mbili hizo kutoafikiana bei ya kuuzia na kununulia pamba mbegu, Serikali kupitia TCB imeshindwa kutangaza bei wala tarehe ya kuanza kwa ununuzi wa pamba hadi hapo tatizo la bei na mizani ya kupimia pamba itakayotumika litakapotatuliwa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Pamba ya 2001, TCB ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza bei elekezi na tarehe ya kuanza kwa msimu wa kununua pamba kwa kushauriana na wadau wa zao hilo.

Akiwasilisha mapendekezo ya bei elekezi kwenye kikao hicho kwa niaba ya wakulima, Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Pamba (TACOGA), George Mpandulizi, alisema kwa kuzingatia bei ya pamba ya senti za Kimarekani 81 katika soko la dunia siku hiyo, bei sahihi kwa mkulima ilipaswa kuwa Sh. 745 kwa kilo.

Mwenyekiti wa TCA, Mwita GachumaLakini Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wachambuaji wa Pamba (TCA) Mwita Gachuma, akiwasilisha mapendekezo ya bei kwa niaba ya wanunuzi alisema bei sahihi katika soko la dunia siku hiyo ilikuwa senti za Kimarekani 69, na hivyo bei sahihi kwa mkulima ilipaswa kuwa Sh. 504 kwa kilo ya pamba safi.

Hata hivyo, TCB, kwa upande wake iliona kuwa, bei sahihi elekezi kwa mkulima ilipaswa kuwa Sh. 650 kwa kilo moja ya pamba nyuzi, kwa maana ya senti 70 za Kimarekani katika soko la dunia, ambayo ilipingwa vikali na wanunuzi (TCA) wakidai kuwa TCB haikusema ukweli kuweza kuisaidia Sekta ya Pamba inayoendelea kuporomoka kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa wakulima, wanunuzi na Serikali.

Katika kutangaza bei elekezi, TCB huzingatia bei ya pamba katika soko la dunia sambamba na gharama mbali mbali za wanunuzi/wachambuaji na wakulima wa la pamba.

Kwa mujibu wa taarifa za TCA na TCB mkutanoni, bei ya pamba katika soko la dunia inaendelea, na itaendelea kuporomoka, kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo sababu za nchi zinazotumia pamba kuwa na akiba kubwa ya pamba ya msimu uliopita; China kupunguza manunuzi kutoka nje, India, Pakistani na Brazili kuwa na pamba nyingi na safi ya kuuza nje, na kuparanganyika kwa uchumi wa Marekani na Ulaya.

Katika vuta nikuvute hiyo yenye malumbano, kati ya wakulima na wanunuzi mkutanoni, hatimaye pande hizo mbili zilikiri kwamba suala la bei lilikuwa nje ya uwezo wa wadau na kwamba TACOGA katika kupinga bei ya 520/= kwa kilo iliyowasilishwa na TCA, haikuzingatia kupanda kwa gharama za umeme kwa asilimia 42, mafuta na gharama za usafiri, hivyo kwamba bei ya Sh. 520 ilikuwa sahihi ingawa haikubaliki.

“Wanunuzi wana uchungu na fedha zao; Wakulima nao wana uchungu na jasho lao; kamwe hatuko tayari kuuza pamba yetu kwa bei ya kinyonyaji, tutaihifadhi majumbani hadi bei ipande”, alisema Mwenyekiti wa TACOGA, Elias Zizi kuashiria suluhu ya pande mbili zilizokuwa zikilumbana.

Zizi alitoa wito kwa Serikali kufikiria nguvu kubwa anayowekeza mkulima kwenye kilimo cha pamba, na hasara anayopata kutokana na kuuziwa kwa gharama kubwa viuawadudu bandia na mbegu za kupanda zisizoota. 

Katika mkutano wa wadau uliofanyika takriban wiki mbili zilizopita, wadau walioshiriki mkutano huo, Elias Mabuba na mwenzake, Muso Alphayo, waliainisha dawa zisizofaa na ambazo zimesambazwa kwa wakulima ni pamoja na dawa aina ya lamddex super.

“Mkulima amekuwa uwanja wa majaribio ya kupiga shabaha ya soko huria katili asiye na mkombozi,” alilalamika.

“Sisi ni wadau wa pamba; wala hatuwezi kujigeuza kuwa wafadhili au watoa msaada kwa wakulima wakati tunaangamia kibiashara kwa bei isiyolipa, kama ambavyo tu hatupendi kumnyonya mkulima.  Hatua yoyote ya kutulazimisha tununue na kuuza pamba kwa hasara, tutaipinga kwa nguvu zote na bila ya suluhu; kwa hili, tunaomba Serikali na wakulima watuelewe hivyo,” alisema Salum Khamis ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Oilmills, kwa niaba ya wanunuzi wenzake.

Dk. Festus LimbuIli kupata ufumbuzi wa tatizo hili, kikao hicho cha Wadau kiliunda kamati ya watu 10 kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete, ikiongozwa na Dk. Limbu na wajumbe kutoka TCA na TACOGA pamoja na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, John Magalle Shibuda, ambaye alijitambulisha kuwa ni mlezi wa TACOGA.

Wakati haya yakitokea, wabunge kutoka Kanda ya Ziwa yenye kulima pamba kwa wingi; waliendelea kushinikiza Serikali bei isipungue Sh. 1,000 kwa kilo moja na wakatoa wito kwa wakulima wasiuze pamba yao chini ya bei hiyo.

Mwaka jana (2011/2012) bei elekezi iliyotangazwa Juni 2011, ilikuwa Shs. 1,100,  ilifikiwa wakati bei katika soko la dunia ilikuwa dola za Kimarekani kati ya 1.50 na 1.60 kwa ratili ya pamba nyuzi; na iliporomoka wiki mbili baadaye kuwa Shs. 800 bei iliposhuka katika soko la dunia kuwa senti za Kimarekani 80, kabla ya kupanda tena mwezi mmoja baadaye kurejea kiwango cha awali.

Minyukano hii ikiendelea, Raia Mwema limebaini kuwa, tatizo la bei duni ya pamba si kwa Tanzania peke yake, bali ni kwa nchi nyingi za dunia ya tatu, hususan nchi za Kiafrika.

Kwa mujibu wa gazeti la Cotton Outlook la Juni 12, mwaka huu, lichapishwalo Liverpool, Uingereza; minyukano juu ya bei ya pamba, kati ya wakulima na wanunuzi imeendelea sehemu nyingi za Afrika. 

Kwa mfano, nchini Zimbabwe, wadau wamekutana mara tano bila kufikia mwafaka, kama ambavyo hawakuweza kukubaliana nchini Zambia juu ya bei elekezi.  Bei ya pamba nchini Zimbabwe, Zambia na Malawi hivi sasa kwa thamani ya fedha ya Tanzania ni kati ya Sh. 430 na 460.

Wakati sakata la utata wa bei likiendelea, uwezekano wa kuanza kwa msimu wa pamba mapema umo shakani pia kutokana na kuchelewa kuingia nchini mizani ya digitali iliyoagizwa na TCA kutoka India, kufuatia Serikali kupiga marufuku matumizi ya mizani aina ya “rula” iliyokuwa ikitumika kwa madai ya kuwa ilikuwa inampunja mkulima.

Mwenyekiti wa TCA, Gachuma, aliwaeleza wadau kuwa, mizani mipya ilitarajiwa kuingia nchini kabla ya Juni mwaka huu, lakini hadi siku hiyo ilikuwa haijawasili na kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda ikawasili Julai, wakati msimu wa ununuzi tayari umekwishatangazwa.

Alisema, jumla ya mizani 8,800 inahitajika, lakini inayotarajiwa kuwasili ni chini ya 3,000, hivyo kutoweza kutosheleza mahitaji ya wanunuzi.

Ili ununuzi wa pamba ya wakulima usiathirike, Gachuma alisema Serikali itaombwa kusitisha kwa muda zuio lake la matumizi ya mizani ya “rula” ili iweze kutumika sambamba na mizani michache ya digitali itakayopokewa.

“Hata Serikali inapoanzisha noti mpya, haiziondoi za zamani kwa mpigo, bali huziondoa taratibu hadi zitakapotoweka; na tunaomba iwe hivyo kwa mizani ya rula”, alisema Gachuma na kuongeza kuwa, huo utakuwa utaratibu mwafaka na utatoa nafasi nzuri kuweza kupima kwa uhakika ubora wa mizani mipya inayotarajiwa kuanza kutumika kwa mara ya kwanza katika Sekta ya pamba,  ikilinganishwa na ya zamani.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako