Wadau washinikiza sera za kilimo sasa zifanyiwe kazi

WATAALAMU wa kilimo na wadau wengine wameshauri kwamba serikali ianze kutekeleza kikamilifu zaidi maazimio na sera zake za kukiendeleza kilimo ili kitoe mchango stahiki kwa pato la taifa.

Msisitizo huo ulitokana na mjadala juu ya mchango wa kilimo katika maendeleo ya nchi kwa ujumla katika mada iliyochochewa na Audax Lukonge, mkurugenzi wa asasi ya ANSAF.

Asasi hiyo ambayo ni mkusanyiko wa asasi za kiraia zinazojihusisha na kilimo (Agricultural Non State Actors Forum) imekuwa ikijihusisha na tafiti na pia kutoa mapendekezo juu ya kukinyanyua kilimo cha Tanzania.

Akiwasilisha mada katika ukumbi wa British Council Ijumaa iliyopita, Lukonge alisema Tanzania inapoteza pesa nyingi za kigeni kwa sababu ya kuagiza mazao ya kilimo yanayoweza kuzalishwa hapa nchini.

“Kwa mwaka 2014 pekee Tanzania ilipoteza takribani dola za Marekani milioni 13.9 kutokana na uzalishaji chini ya kiwango katika sekta ya kilimo. Iwapo sekta hii itafanya kazi kwa ubora unaotakiwa basi inaweza kuzalisha ajira kwa asilimia 67,” alisema.

Zao la korosho huuzwa nje ya nchi katika mfumo wa malighafi kwa kiwango cha asilimia 85, hali ambayo hulinyama taifa mapato makubwa stahiki.

Pia mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini katika baadhi ya mikoa kama Dodoma na Singida yanaweza kukidhi soko la ndani lakini serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kuagiza mafuta kutoa nje ya nchi.

Alishauri kwamba sekta binafsi itoe mchango stahiki katika eneo la usindikaji ili kuipunguzia serikali uzito wa jukumu hilo. “Tunapaswa kufahamu kwamba tumebaki nyuma kiasi kwamba jirani zetu wa Kenya na Msumbiji sasa wapo mbele yetu katika ufanisi kwenye eneo hilo,” aliongeza.  

Alifafanua kwamba kitendo cha kuuza mazao yasiyosindikwa kinapeleka ajira nje ya nchi badala ya kuwanufaisha Watanzania. Alibaisha kuwa eneo jingine ambalo halijafanyiwa kazi vya kutosha ni mazao ya mifugo hususani maziwa na ngozi.

Alishauri njia sahihi za kuleta mabadiliko katika eneo hilo kuwa ni pamoja na kuogeza tafiti. Lakini pia akashauri upanuzi wa sekta ya wajasirimali kwa kuwawezesha ili watoe mchango stahiki.

Zaidi ya hayo aliomba mchango wa taasisi kama vile SIDO, TEMDO, CARMATEC, TIRDO uboreshwe zaidi. Pia alishauri kwamba kuwepo na taarifa za kutosha katika tovuti na pia walengwa wajifunze kuyapenda mazao ya kilimo hususani vyakula kutoka nyumbani Tanzania.

Lakini kwa upande mwingine alishauri kwamba sekta ya benki iongeze mikopo kwa pande zote mbili wakulima na wasindikaji ili kufanikisha zoezi hilo. Na pia mfumo wa sheria na sera virahisishwe ili viweze kueleweka hadi kwa wakulima na wafugaji wadogo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Sembeye alikosoa tabia ya kuwapo maandishi na sera nzuri katika kilimo zisizofanyiwa kazi. Alirejea chapisho la Kilimo Kwanza na kueleza kwamba linajitosheleza lakini utekelezaji wake ni duni na hakuna mwelekeo kwamba mambo yatabadilika hivi karibuni.

“Tangu mwaka 2005 tumesikia hii habari ya usindikaji na mwaka 2009 tukapata hili andiko la Kilimo Kwanza lakini mpaka leo hakuna utekelezaji yaelekea kuna matatizo katika mfumo wa utawala wa eneo hilo na hili linahitaji kufanyiwa kazi,” alidokeza.

Alishauri kuwepo ujenzi wa viwanda vilivyojikita katika kilimo na pia menejimenti ya kodi itoe unafuu kwa wawekezaji katika sekta ya kilimo. Zaidi ya hayo alishauri kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), iangalie namna ya kuwaruhusu wazalishaji wadogo ili wapate leseni za biashara ingawaje viwango vya ubora vinatakiwa vizingatiwe.

Akichangia katika mada hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya SAGCOT, Godfrey Kirenga, alisema ukanda wa kusini na pwani mwa Tanzania unazalisha theluthi moja ya chakula chote cha Tanzania na akasema kwamba taasisi yake inazingatia juu ya kilimo endelevu.

“Tumejikita katika kuhakikisha kwamba mazao ya kilimo yana ubora wa kuweza kuuzwa nje ya nchi lakini pia kilimo kiwe kwa ajili ya biashara na chakula kwa pamoja. Alikosoa uzembe wa kutozalisha mazao mapya na badala yake kuendeleza yale yaliyoachwa na wakoloni akitolea mfano zao la korosho.

Alikosoa kwamba sekta binafsi haijachangia vya kutosha katika eneo la usindikaji ndiyo maana hata baadhi ya ranchi zinalazimika kuagiza chakula cha mifugo kutoka nje wakati kingeweza kuzalishwa nchini.

Profesa Adolfo Mascarenhas anasema asilimia 18 ya wafugaji waliathiriwa na sera ya Kilimo Kwanza baada ya kutakiwa kuacha ardhi kwa ajili ya kilimo lakini bado kilimo chenyewe hakijakidhi mahitaji na wakati huo huo wafugaji wanaendelea kutafuta malisho ya mifugo yao kila uchao.

Naye pia akashauri juu ya uwepo wa viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya usindikaji na pia kubadilisha fikra za watu juu ya ulaji wa mazao yanayozalishwa nchini. Alishauri serikali kuwa makini na wafanyabiashara kutoka nje ambao hutumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha uzalishaji unakwama ndani ya Tanzania ili wao walete bidhaa zao.

Lakini pia akashauri kwamba maelekezo ya kitaalamu yatumike badala ya kutanguliza siasa katika eneo hilo. Alisisitiza kwamba kilimo cha Tanzania kitasonga mbele kwa kuzingatia utaalamu wa ndani na uzoefu kutoka nje na hivyo kuna umuhimu wa wataalamu wa Tanzania kusafiri mara kwa mara kwa ajili ya kupata uzoefu huo.

Wachangiaji katika mjadala huo walishangaa kuona kwamba serikali ya Tanzania inaruhusu kuingizwa kwa vitu vidogo ambavyo vingeweza kuzalishwa hata hapa nchini kwa mfano maziwa na asali. Walishauri serikali ivilinde viwanda nchini.

Akichangia katika mjadala huo Revelian Ngaiza kutoka wizara yenye dhamana na kilimo nchini alishauri kwamba watumiaji wa mazao ya kilimo waelimishwe ili kubadili tabia zao.

Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda na Biashara Ndogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Consolata Ishebabi, alishauri kwamba njia nzuri ya kuendesha miradi ya kilimo ni kwa kuingia ubia kati ya serikali na sekta binafsi. Hata hivyo alishauri kwamba jukumu kubwa zaidi ni kulinda masoko ya ndani ili kutoa fursa kwa wazalishaji wadogo.

Pia aliitetea serikali kwamba mara kadhaa imekuwa ikizuia baadhi ya miradi “isiletwe” nchini ili kuwapa mwanya huo Watanzania. “Siyo lengo la serikali kuwavunja moyo Watanzania, bali wakati mwingine mazingira ya kiuchumi yanakuwa magumu kwao, tunatakiwa kuwa na ‘visheni’ moja kati ya sekta binafsi na serikali,” alisistiza.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuka ni pamoja na ushauri wa kupanua kilimo cha umwagiliaji. Na pia kusindika nyama ili kuwaongezea kipato wafugaji, lakini pia ikiwa ni njia mojawapo ya kuzalisha ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *