Wafahamu watu wanaosimama nyuma ya Conte

ANTONIO Conte amewasha moto katika Ligi Kuu ya England. Conte ambaye ni kocha wa Chelsea ameifanya timu hiyo kuwa na kiwango kizuri na yeye mwenyewe akishinda tuzo ya kocha bora wa mwezi mara mbili mfululizo. Ameshinda tuzo hiyo mwezi Oktoba na Novemba.

Licha ya Conte kutajwa kama kocha bora wa kizazi kipya, lakini kuna watu wanaosimama nyuma yake na kumfanya aonekane bora dhidii ya makocha wenzie.

Angelo Alessio

Alessio ambaye ni Mtaliano ndiye msaidizi namba moja wa Conte. Alessio na Conte wametoka mbali na waliwahi kucheza pamoja Juventus na kufanikiwa kutwaa mataji mbalimbali. Conte alianza kumuamini Alessio kama msaidizi wake tangu alivyokuwa mwalimu wa timu za Siena, Juventus mpaka timu ya taifa ya Italia. Sifa kuu ya Alessio ni kufahamu kwa haraka zaidi mbinu za wapinzani na kuwasilisha taarifa kwa bosi wake.

Steve Holland

Conte amemkuta mtu huyu ndani ya Chelsea na ameamua kumuamini na kuendelea kufanya nae kazi kutokana na maono ya Holland katika soka. Holland aliwahi kufanya kazi pamoja na Andre Villas Boas (AVB) baadae Robertto Di Matteo, Rafael Benitez, Jose Mourinho na Guus  Hiddink.

Kinachotajwa Conte kuwa na Holland katika benchi lake ni kutokana na Holland kufahamu mazngira ya Chelsea na ligi ya England. Licha ya Holland kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Chelsea, lakini pia anamsaidia kocha wa timu ya taifa England Gareth Southgate. Holland anatajwa kukubalika na wachezaji.

Gianluca Conte

Huyu ni mdogo wa Conte na wote walianzia maisha ya mpira kwa kucheza soka katika timu yao ya mtaani ya Lecce na wote walisomea pamoja masuala ya soka, huku Gianluca akiwa amesomea zaidi mambo ya Sayansi ya Michezo (Sports Science).

Moja ya sifa yake ni kuwa na maono ya hali ya juu kufahamu kila hali ya mchezaji ndani ya kikosi chake pamoja na vikosi vya wapinzani.

Carlo Cudicini

Cudicini licha ya kuwa msaidizi wa Conte katika masuala ya ufundi, lakini pia ni Balozi wa klabu hiyo nchini Italia. Cudicini amekaa miaka 10 ndani ya kikosi hicho akicheza michezo 216.

Gianluca Spinelli

Huyu ndiye anayetajwa kumtuliza mlinda mlango Thibaut Courtois ambaye alikuwa akitajwa kuondoka baada ya kugombana na aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo Christophe Lollichon aliyeondolewa na Conte.

Spinelli ni fundi katika idara hii aliyoanza tangu mwaka 2002 mpaka sasa amedumu kwenye idara hii ya kocha wa makipa na amefanya kazi kwa mafanikio akiwa Kocha bora wa Makipa wa Seria A misimu ya 2011/12,2014/15 na msimu uliopita 2015/2016.

Spinelli, anasimama nyuma ya ubora wa mlinda mlango wa Italia na Juventus Gianluigi Buffon, ambaye mara ya mwisho alikuwa naye katika michuano ya Ulaya 2016, iliyofanyika nchini Ufaransa.

Henrique Hilario

Hilario ni msaidizi wa Spinelli katika kuimarisha viwango vya walinda milango wa Chelsea. Hilario ni mlinda mlango wa zamani wa timu hiyo ingawa hakucheza kwa mafanikio makubwa akiwa amecheza michezo 39. Alianza kujifundisha kazi ya ukocha mara alipostaafu.

Paolo Betelli

Majukumu ya Betelli ndani ya Chelsea ni kufanya kazi za viungo.  Betelli alifanya kazi na Conte wakiwa Juventus na baadae timu ya taifa ya Italia. Mwalimu huyo wa viungo alianzia kazi hii kwenye klabu ya Fiorentina aliyodumu nayo kwa miaka 14 na aliwahi kuwa na kocha wa sasa wa Leicester City Claudio Ranieri katika klabu ya Fiorentina. Betelli amewahi kuwa kocha bora wa viungo mara nne tofauti katika ligi ya Italia (Serie A).

Julio Tous

Tous ni Mhispania ambaye ni mtaalamu wa viungo na misuli na alikuwa na Conte katika timu ya taifa ya Italia na amewahi kuwa katika timu za Real Zaragoza, Barcelona, Sampdori. Tous ana shahada ya Sayansi ya Michezo (Sports Science)

Chris Jones

Jones mwenye jicho pevu katika timu B ya Chelsea alijiunga Chelsea tangu 2006 akifanya kazi na makocha mbalimbali waliokuja kufanya kazi katika kikosi hicho. Jones amepewa kazi ya kocha wa wachezaji wa akiba akifanya kazi ndani ya kikosi hicho kwa muda mrefu sasa.

Constatino Coratti

Coratti ambaye ni Muitaliano kama Conte ni mtaalamu wa viungo na walikua na Conte kwenye timu mbalimbali alizofundisha Conte. Huyu ndio mtu pekee ambaye kila anapokwenda Conte, Coratti nae atakwenda.

Tiberio Ancora

Ancora ni mtaalamu wa masuala ya upishi. Majukumu yake ni kuwapangia wachezaji wale nini kulingana na program za mazoezi. Ancora ameanza kufanya kazi na Conte tangu Bari, Torino, Verona, Lecce na timu ya taifa ya Italia.

Hao ndio watu waliopo nyuma ya Conte ambao wengi hawafahamiki ni kutokana na kutojionyesha mbele ya kamera mbalimbali za waandishi wa Habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *