INAWEZEKANA sisi ni kati ya nchi chache duniani ambazo raia wake ni wema na wakarimu sana. Hii ndio sababu ambayo imetupatia sifa kubwa duniani kiasi kwamba, kwa watu wa mataifa mengine wanaoifahamu nchi yetu wasikiapo jina Tanzania, hutuelezea kwa maneno mawili ‘Nyerere’ na ‘ukarimu’.
Hata majirani zetu wa Afrika ya Mashariki huielezea Tanzania kwa maneno haya mawili, na wakati mwingine wakiongezea neno la tatu, ‘Kiswahili’.
Lakini ukarimu wetu huu bila shaka inabidi usiwe ukarimu wa kupindukia. Hii si kwa sababu tu za kuhakikisha usalama wa nchi yetu na ustawi wa Watanzania kwa ujumla, lakini pia ni kwa ajili ya kulinda amali (values), mila, tamaduni na hata historia yetu kama taifa. Hivyo nitakachokijadili hapa ni kwa misingi hii hii na si vinginevyo.
Kuutazama ukarimu wetu kama unavuka mipaka au la, ni suala la muhimu pia kama kipimo cha kutathmini jinsi tunazingatia sheria na taratibu tulizojiwekea kama nchi. Hata sheria za kimataifa zinatambua mipaka, uhuru na hata sheria za kila nchi ilizojiwekea katika kupokea, kuishi na hata kuwaruhusu wageni kuendesha shughuli mbalimbali katika nchi husika.
Tumekuwa na kawaida ya kusikia kuwa wageni kadhaa wamekamatwa katika mipaka ya nchi yetu (na hata wengine wakiwa wameshafika miji ya katikati ya nchi) wakiwa kwenye malori au mabasi. Lakini ukiacha hao wanaokamatwa wakiwa wengi, lipo tatizo kubwa hivi sasa la wageni, walio mmoja mmoja au wawili, kuingia nchini na kufanya shughuli zao hasa za kibiashara bila kufuata taratibu na sheria zinazowaruhusu kufanya hivyo.
Natambua kuwa, katika ulimwengu huu wa maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na utandawazi, au wengine waitavyo nyakati za “dot com”; maingiliano ya watu ni ya kasi sana na kuyadhibiti ni changamoto kubwa. Hata hivyo, kama taifa, vipo vyombo maalumu kama vile idara ya uhamiaji na vinginevyo ambavyo kazi yake kubwa ni kukabiliana na changamoto hizi kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kila leo.
Lakini kwa nchi yetu, kinachoonekana hivi sasa ni ama vyombo au taasisi hizi zimejisahau, au zimeelemewa na changamoto hii ya wageni kuendelea kujazana na ‘kujichanganya’ kama Watanzania.
Kama hali itaendelea hivi, ipo siku tutafikia hatua mbaya kama hapa Afrika Kusini ambapo katika miaka ya karibuni katika sehemu kadhaa kumekuwa na uhasama mkubwa kati ya wageni na wazawa.
Ingawa zipo sababu zinazodaiwa ni za kibaguzi zinazochochea uhasama huu, lakini pia kujisahau na kuzembea kwa vyombo husika katika kuwabana wageni kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu zinazotakiwa kumekuwa chanzo cha uhasama huu.
Hata nchini kwetu, wapo wageni ambao wanadaiwa kufanya shughuli zao, huku nyingine zikiwa haramu, wameendelea kujistawisha na shughuli hizo lakini walio karibu nao hawawaulizi, na hata vyombo vinavyohusika (hata kama vinajua kinachoendelea vimekaa kimya).
Ndugu mmoja wa nchi mojawapo jirani na Tanzania nilikutana naye eneo maarufu sana kwa wageni lijulikanalo kama Brookyln (inatamkwa Brukilin) jijini Cape Town nchini hapa alikuwa ananisimulia jinsi alivyofanya shughuli zake za kibiashara kwa miaka mingi sana katika jiji mojawapo nchini kwetu, bila kubughudhiwa.
Hapo Brooklyn wapo wageni wengi sana kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama vile Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Cameroon na kwingine. Wapo pia Watanzania wengi wanaoishi na pia kuendesha shughuli zao za biashara hapo.
Wakati nikitembezwa eneo hilo, kilichonistaajabisha ni kuwa, kwanza kulikuwa na wengi kati yao ambao wamewahi kufanya shughuli za kibiashara (ndogo ndogo) nchini Tanzania. Pili, kati ya hao waliowahi kuwa Tanzania, Mtanzania anayefika eneo hilo wanapenda kuzungumza naye kwa kutumia Kiswahili. (hili sio tatizo kwani Kiswahili ni fahari ya Utanzania).
Lakini cha tatu ni kuwa ndugu hawa waliowahi kuishi Tanzania hupenda kujidai kuwa wao ni Watanzania; utagundua kuwa si Watanzania iwapo tu atakuwepo Mtanzania halisi mwenyeji wako atakayekuambia kuwa hao si Watanzania; au mpaka utumie muda mrefu kuwatafiti.
Tukirudi kwenye hiyo hadithi ya ndugu huyo aliyefanya shughuli zake kwa muda mrefu nchini Tanzania, katika maelezo yake na wenzake, alitusifia Watanzania kwa jinsi tulivyo wakarimu, lakini pia tusivyo na gere ya kumbugudhi mgeni afanye shughuli zake.
Katika msingi wa mantiki iliyokuwa katika maelezo yake, nilibaini kulikuwa na chembembe za kejeli ndani yake. Kwamba, sisi Watanzania wema wetu ni ule wa kuruhusu mgeni afanye chochote kile hata kama ni kiovu na kinyume cha sheria, ilikuwa ni kejeli.
Maelezo ya jamaa huyu wa Brukylini yalishabihiana na mazungumzo ya abiria wenzangu kwenye daladala jijini Dar es Salaam, Desemba mwaka jana. Huu ulikuwa ule wakati wa mvua zilizoleta mafuriko yaliyoathiri maeneo mengi ya mabondeni jijini. Tukiwa tunapita kandokando ya maeneo ya Kigogo, yalizuka mabishano yaliyoibua mjadala wa suala la wahamiaji wanaofanya shughuli zao nchini bila kufuata taratibu na sheria.
Mabishano ya mwanzo yalihusu nani hasa alipaswa kulaumiwa kati ya serikali na wakazi waliokuwa wakiishi maeneo hayo ya mabondeni, kwa maafa yale ya mafuriko. Kila upande ulikuwa na hoja zake; upande mmoja uliwalaumu wananchi waliokuwa wakiishi maeneo hayo kwa kutokuchukua tahadhari mahususi ikiwemo kuitikia wito wa serikali wa kuhama maeneo hayo kwani ni hatari.
Lakini upande mwingine ulisema serikali inapaswa kubeba lawama kwa sababu haikuweka mipango madhubuti ya kuwaondoa wanaoishi sehemu hizo na pia kuwaandalia maeneo ambayo wangeweza kuishi.
Katika hawa waliokuwa wakiilaumu serikali, ndipo abiria mmoja alitoa mfano wa tatizo la wageni kujazana nchini na kufanya shughuli zao bila kufuata taratibu zinazotakiwa. Kwa mujibu wa maelezo yake, hili ni mojawapo ya mambo yanayoonesha kuwa serikali imekuwa haichukui hatua madhubuti na kwa uzito unaotakiwa kuyashughulikia matatizo mahususi.
Hoja ya abiria huyu ilibadilisha upepo wa mabishano yaliyokuwa yakiendelea na kuwa ndio mjadala mkubwa. Katika mjadala huo, maneno ya abiria mmoja yamebaki kuwa kumbumkumbu kwangu; alisema: “Ndiyo, wageni wamejazana, wakikaa kidogo tu wakaongea Kiswahili kama sisi, wanafanya shughuli zao, wanauza chips, na kadhalika lakini walio na vibali vya kuwa nchini niulize ni wangapi!”.
Inawezekana maneno haya yaliongezwa chumvi ili kukoleza hoja ya mzungumzaji. Lakini kwa vyoyote vile yanafikirisha. Ni mara chache sana kwa mtu kuongea maneno yasiyo na ukweli wowote katika mazingira yale; hasa ikizingatiwa kuwa hakuwa mwanasiasa au mgombea anayejitafutia kura kutoka kwa abiria wenzake.
Tukatae au tukubali, ukweli ni kuwa lipo tatizo mahali fulani. Zipo sehemu nyingi nchini, hasa mijini, ambazo zinao wageni wanaofanya shughuli zao bila kufuata taratibu zinazotakiwa. Na Watanzania walio karibu nao, wakiwemo wanaofanya kazi katika vyombo vinavyoshughulika na suala hilo, wanajua lakini wamenyamaza.
Hatuna budi kuchukua hatua kushughulikia tatizo hili mapema. Huu si ubaguzi bali ni kuhakikisha kuwa kama taifa, tuko salama, amali zetu na thamani yetu kama Watanzania inabaki kama tulivyorithishwa na wazee wetu.
Nchi nyingine zinafanya hivi pia kwa umakini na zimefanikiwa katika kuhakikisha wageni wanaosoma, wanaofanya shughuli zao ziwe za kibiashara au vinginevyo kuwa wana vibali vya kufanya hivyo na wanafuata sheria na taratibu zilizowekwa. Tukifanya hivi pia, Uutaifa wetu pia utakuwa salama salimini; Hii haiathiri silka na hulka yetu kama Watanzania wakarimu- vitaendelea kubaki. Hatujachelewa sana.
Maoni ya Wasomaji
Nenda kariakoo ukawashuhudie
Nenda kariakoo ukawashuhudie wasomali hata kiswahili hawaju lakini wana maduka makubwa na uraia juu! Usishangae sana, bongo pesa ndo inaongea!