Tahariri
Maoni ya Mhariri
Wahandisi sasa watumike kikamilifu
John Bwire
Toleo la 244
20 Jun 2012

TAASISI ya Wahandisi Tanzania imebuni mradi wa kujenga uwezo wa wahandisi wa Tanzania ambao kama utakwenda kama ilivyopangwa, tutaanza kuona kazi tulizozoea zinafanywa na wageni, zikifanywa na Watanzania wenyewe na mwamko wa fani ya uhandisi nchini kuwa mkubwa kuliko ilivyo hivi sasa.

Rais wa taasisi hiyo, Malima Bundara aliwaambia waandishi wa habari  jana Jumanne kwamba wamebuni mradi huo kutokana na ukweli kwamba ongezeko la wahandisi  wasiokuwa na kazi  hata ya kujiajiri inakatisha tamaa vijana kusomea au kujiunga na fani hiyo. 

Siyo siri kwamba pamoja na taifa kuzalisha wahandisi wengi kila mwaka, miradi mingi ya maendeleo nchini hufanywa na wahandisi kutoka nje hivyo kugharimu taifa pesa nyingi za kigeni.

Tanzania ina wahandisi waliosajiliwa na Serikali zaidi ya 10,400  na inakadiriwa wahandisi wengine zaidi ya 2,000 hawajasajiliwa kwa sababu mbalimbali.

Wahandisi wanaozalishwa nchini hawatumiki ipasavyo licha ya kuwapo kwa kazi lukuki katika nyanja za nishati na madini, miundombinu, ujenzi wa majumba na mradi wa Kilimo Kwanza.

Kwa mujibu wa Bundara, mradi huo utakuwa ni wa maeneo manne, maeneo hayo yakiwa ni ya uhamasishaji  wa shughuli za kiufundi, kurekebisha muundo wa taasisi ili nguvu kazi isiyotumika ya marais wastaafu wa taasisi hiyo ipewe jukumu la ushauri (think tank) ili kutumia uzoefu na utaalam wao. Kukusanya, kuhifadhi na kutumia takwimu za wahandisi mahiri.

Hili suala la kuwa na kumbukumbu au  takwimu za wahandisi mahiri nchini ni muhimu mno ili matatizo ya Watanzania yatatuliwe na Watanzania wenyewe  kama vile  yanapotokea majanga badala ya kuanza kufikiria wahandisi wa nje kwa utatuzi.

Tanzania ina wahandisi ambao ni wataalam wa nyanja  mbalimbali lakini kwa vile hakuna kumbukumbu au takwimu zinazowahusu, taifa hulazimika kutumia wahandisi wa nje wenye utalaam ule ule inapotokea shida.

Aidha taifa lisingelazimika kuunda tume za uchunguzi kwa matatiz yanayojikeza kwa vile tume nyingi zimekuwa zikichunguza matatizo ambayo wahandisi wetu  wangeweza kuyatatua.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
John Bwire
jbwire@raiamwema.co.tz

Maoni ya Wasomaji

HIlo ni jambo la msingi litatusaidia sisi ambao bado tuko masomoni kujua nini kinachoendelea katika fani ya uhandisi

Toa maoni yako