Waliofukuzwa CCM Babati wamlilia Magufuli

WALIOKUWA viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Manyara ambao wamefukuzwa uanachama wa chama hicho kwa madai ya kukisaliti wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2015, wamemlilia Mwenyekiti wa Taifa,  Dk. John Pombe Magufuli  kuwa wapewe fursa ya kusikilizwa.

Viongozi hao ni miongoni mwa wanachama, makada na viongozi zaidi 1,000 waliofukuzwa wakati wa kikao cha Mkutano Mkuu wa CCM kilichofanyika Dodoma mwezi uliopita.

Kwa mkoa wa Manyara, viongozi wa juu waliovuliwa uanachama ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Ali Khera Sumaye na Mwenyekiti wa wilaya  ya Babati Mjini, Ali Msuya.

Katika uchaguzi huo mwaka juzi, mgombea wa CCM katika jimbo hilo la Babati, Kisyeri Chambiri, alishindwa vibaya na mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Paulina Gekul na pia chama hicho tawala kilipoteza Halmashauri ya Mji wa Babati kupata madiwani watatu tu katika kata nane.

Katika waraka wao kwa mwenyekiti wa chama hicho wa Machi 7 mwaka huu, viongozi hao pamoja na mambo mengine, wameanisha  sababu kadhaa za chama hicho kushindwa uchaguzi katika jimbo la Babati Mjini.

Waraka huo umeambatanishwa na vielelezo kadhaa ikiwemo taarifa rasmi ya Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Manyara iliyokutana Februari 25 mwaka 2016 kuhusu tathmini ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Vielelezo vingine ni nyaraka zinazohusiana na upotevu na ufisadi wa fedha za chama za malipo ya mabalozi ya kiasi cha Sh. milioni 40 wakati uchaguzi uliofanywa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bernard Ghati na watumishi wa ofisi ya CCM wilaya na matumizi mabaya ya fedha na tozo za kodi ya pango kwa majengo na mali za chama hicho Mkoa wa Manyara.

“Kuvuliwa kwetu uanachama ni uonevu mkubwa na ni ukiukwaji wa katiba ya Chama Cha Mapinduzi kwamba  hatua ya kumvua uanachama mwanachama yoyote lazima zianze na vikao vya chini vya chama katika ngazi ya matawi na kata,” anasema aliyekuwa Mjumbe wa NEC,  Ali Sumaye.

Sumaye alieleza kuwa hatua hiyo ya kuvuliwa uanchama imemdhalilisha sana mbele ya jamii na marafiki zake wanaomwamini kutokana na hadhi aliyonayo na kwamba ameitumikia CCM kwa zaidi ya miaka 20 kwa kushika vyeo mbalimbali katika ngazi ya mkoa wake wa Manyara na kitaifa.

Aliongeza kuwa jambo baya zaidi ni kwamba kuna baadhi ya viongozi akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera wamekuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kuwaaminisha wananchi na wanachama wa CCM kuwa wao walikuwa wasaliti.

“RC anazunguka na kuwaaminisha watu kuwa sababu ya CCM kuangushwa ilikuwa ni sisi, na amefanya hivyo kuwaaminisha pia viongozi wa ngazi ya juu wa chama jambo ambalo si sahihi,” alisema Sumaye.

Aliongeza: "Mimi binafsi nilimpelekea RC Bendera  jalada lenye tuhuma na vielelezo vyote muhimu ya mambo yaliyokuwa yanafanywa na viongozi wa chama wilaya na mkoa ili  aviagize vyombo dola kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria lakini alipuuza na hakuna hatua zilizochukuliwa na badala yake wametutoa kafara sisi ili kuficha aibu na fedheha iliyowakuta.”

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera alipuuza madai na tuhuma dhidi yake kwa kueleleza kuwa hakuna namna yoyote kama Mkuu wa Mkoa alihusika na siasa za Chama Cha Mapinduzi na kuvuliwa uanachama kwa viongozi hao.

“Hayo ni madai ya kushangaza sana, mimi ni msimamizi wa shughuli za serikali katika mkoa sihusiki kwa namna yoyote na shughuli za CCM. Mimi si mwenyekiti, mimi si katibu, wala si msemaji wa CCM, sasa huyo ananihusisha vipi na yeye kuvuliwa uanachama?" alihoji Bendera.

Sababu za CCM kushindwa

Katika waraka huo, viongozi hao wameainisha sababu kadhaa chama hicho kushindwa katika uchaguzi huo wa mwaka 2015 kuwa ni pamoja na uzoefu na uwezo mdogo wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kuwashirikisha viongozi  wenzake kama ilivyo kawaida za chaguzi ndani ya chama.

“Pia  mgombea aliyependekezwa kugombea (Kisyeri Chambiri) alihusishwa  na kashfa  ya rushwa baada ya kukamatwa na Takukuru wakati wa mchakato wa kura ya maoni na kashfa hiyo iliwaudhi wapiga kura wengi wa jimbo la Babati Mjini,” unaeleza zaidi waraka huo.

Ulieleza zaidi waraka huo: "Wakati wa kampeni mgombea na mkurugenzi wa Uchaguzi waliamua kujitenga na kamati ya siasa na viongozi wengine na kufanya kampeni wenyewe tofauti na utaratibu wa chama na pia alitumia ndugu zake kuwadhalilisha kijinsia wasichana waliokwepo kwenye kampeni.”

Sababu nyingine imetajwa kuwa ni ubadhirifu na ufisadi wa fedha zilizotolewa na makao makuu ya chama kusadia uchaguzi kutowafikia walengwa ambao ni mabalozi, makatibu wa matawi na kata hivyo wengi kukosa morali ya kampeni na hatiamaye chama kushindwa.

Nagu, mwenyekiti wahusishwa

Katika sehemu ya mwisho ya waraka huo huo, viongozi  hao waliovuliwa uanachama wameandika kuwa wakati wa kikao cha Halmashauri  Kuu kupitisha majina ya wagombea wa CCM mwaka 2015, Mwenyekiti Jakaya Kikwete alishawishiwa na Mbunge wa Hanang, Mary Nagu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara Luka ole Muksi.

“Kutokana na tuhuma za rushwa alizokuwa nazo mgombea wa jimbo la Babati, Kisyeri Chambiri aliondolewa na Kamati Kuu lakini kesho yake asubuhi Nagu na Mwenyekiti ole Muksi walikutana na Mwenyekiti wa Taifa wa  chama Kikwete na kumshawishi kurudisha jina lake kuwa mgombea wa Babati Mjini,” uliongeza waraka huo.

Sumaye ameeleza kuwa kutokana na hali iliyojitokeza, alitoa angalizo kwa Mwenyekiti  Kikwete  kuwa mgombea huyo hakubaliki na iwapo atashindwa uchaguzi basi viongozi waliofanya ushawishi wawajibike.

“Viongozi hao walikubali mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu kuwa wangewajibika lakini tunawashangaa hadi leo bado wako madarakani na hawajachukuliwa hatua yoyote na wameendelea kupotosha umma kuhusu sisi kuvuliwa uanachama,” umeongeza waraka huo.

“Kwa vielelezo tulivyowasilisha tunamwomba Mwenyekiti wetu wa chama, Taifa Dk. Magufuli ambaye tuna imani naye arejee maamuzi yaliyofanyika juu yetu na tupewe fursa ya kujieleza na kuwasilisha ushahidi wa hujuma dhidi yatu ili haki iweze kutendeka, ” alisema aliyekuwa Mwenyekiti Ali Msuya.

Aliongeza ya kuwa wanacholilia kwa Mwenyekiti Dk. Magufuli ni kupewa nafasi ya kusikilizwa hata kama kuna uwezekano  waundiwe kamati huru itayochunguza  mgogoro wa ndani ya chama hicho ngazi ya wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara.

Kauli ya Polepole

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Polepole alisema asingweza kujibu chochote kuhusu waraka huo kwa vile bado haujamfikia.

“Ningeweza kukufanyia upendeleo maalumu pamoja na kwamba hii ni wiki ya sikukuu lakini kama sijauona na nini kimeandikwa siwezi kujibu chochote,” alisema katibu huyo.

Hata hivyo, alifafanua kuwa  mwanachama yoyote anaweza kufikiriwa kusikilizwa malalamiko au rufaa yake  baada ya miezi 48 kwa mujibu wa kanuni zilizopo.

“Wote waliovuliwa uanachama wamefanya makosa ya kukiuka kanuni  na miiko ya uongozi wa  chama chetu, na tulichofanya ni kusafisha chama na nikisema hivyo nina maanisha hasa,” alisema Polepole.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *