INAWEZEKANA ujumbe huu ukaonekana umechelewa. Kwamba ulihitajika utolewe mapema kabisa mara tu kampeni za kuwania ubunge wa jimbo la Igunga zilipoanza. Ni sawa. Hata hivyo, nimeamua kutoa ujumbe huu kipindi hiki kutokana na yale ambayo yamekuwa yakiendelea wakati huu wa kampeni.
Yanayotokea na yaliyotokea ndio yamenisukuma kuandika ujumbe huu. Ningeutoa mapema sana ingeonekana ni utabiri wa ama mambo hewa au ya kufikirika. Hivyo; kutokana na mwenendo wa hali ya mambo jimboni Igunga kwa sasa, kuna kila haja ya kutoa ujumbe huu. Mengi ambayo mtu angetarajia yawe ndio kipaumbele katika kampeni hizo, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali tunazozipata, hususan za vyombo vya habari, inaonekana yametupwa kapuni. Na ikumbukwe kuwa ni takribani majuma mawili tu yamesalia ili wananchi wa Igunga wachague mbunge wao.
Kabla ya kujadili ni kwa nini ujumbe huu umebeba dhima kuu ya wana-Igunga kujihadhari na wapita njia, tujikumbushe kidogo kuhusu mwenendo wa chaguzi ndogo nchini. Kwa kawaida uchaguzi mdogo mara nyingi huwa ni kivutio katika namna nyingi.
Ukitaka kuthibitisha hili, rejea chaguzi ndogo kadhaa ambazo zimewahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Mathalani, kumbuka uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime mwaka 2008 na ule wa jimbo la Busanda mwaka 2009.
Mojawapo ya hali ya kawaida ya chaguzi ndogo ni kuwa hubadili upepo wa kisiasa nchini; kwani masikio na macho yote huelekezwa sehemu ambako uchaguzi huo unafanyika. Hii huwa ndio njia mojawapo ya kuifanya sehemu husika ifahamike sana na masuala yanayozunguka sehemu hiyo kama vile hali ya maisha ya watu wa hapo, raslimali zilizopo na matatizo yaliyopo eneo hilo.
Kwa namna Fulani, uchaguzi mdogo ni karata njema kwa watu wa eneo husika. Kama walikuwa hawajawahi kutembelewa na viongozi wa kitaifa wawe ni wa serikali au wa vyama vya siasa kwa miongo kadhaa, basi, huu ni wakati ambapo hawakosi kupata ugeni wa viongozi hawa, angalau hata mmoja.
Jimbo ambalo kuna uchaguzi mdogo hupata pia bahati ya kuhudumiwa kikamilifu na waandishi wa habari ambao, ingawa mara nyingi wanakuwa wakiandika habari zinazohusu uchaguzi, lakini pia huweza kujikita kuhusu masuala mengine tofauti. Hizi ni kati ya ‘faida’ chache kwa wakazi wa maeneo ambayo uchaguzi mdogo unafanyika, kama hivi sasa ilivyo Igunga.
Hata hivyo, pamoja na faida hizo na nyinginezo zinaloletwa na uchaguzi mdogo, kuna hasara nyingi ambazo hujitokeza kama masuala ya msingi hayajazingatiwa kuhusiana na uchaguzi huo. Mara nyingi hasara hizi huwa ni za kudumu, na ni mbaya zaidi hasa kwa ustawi wa jimbo ama eneo husika.
Hapa ndipo tunapokutana na dhana ya ‘wapita njia’, ambao kwa kawaida ninamaanisha waliokuja kupiga kampeni kwa maslahi yao na ama ya vyama vyao au ya waliowatuma; wakisahau kuwa kipaumbele cha yote inatakiwa yawe maslahi ya watu wa jimbo ambalo uchaguzi unafanyika.
Kati ya masuala yote ambayo wapiga kura katika eneo la uchaguzi mdogo; hususan Igunga wanatakiwa wajihadhari nalo, ni hawa wapita njia. Kwa sababu kadhaa.
Mosi, tunatambua kuwa Tanzania ni moja na hivyo yanayozingatiwa kama vipaumbele katika chaguzi ndogo kwa namna moja ama nyingine yanaakisi mahitaji ya Watanzania kwa ujumla. Hata hivyo, kuna mahitaji maalumu ambayo yanatakiwa kuzungumzwa kwa ajili ya sehemu fulani tu, ambayo ni tofauti na sehemu zingine.
Kwa mfano, wakati kule Kagera watazungumzia zaidi namna ya kuwaendeleza na kuwanufaisha wakulima wa kahawa na migomba, watu wa Dodoma vipaumbele vyao haviwezi kuwa sawa na vya hao wa Kagera. Hawa mtaongelea masuala tofauti, mfano kilimo cha karanga na mengineyo.
Ni kwa msingi huu huu, tunapojadili suala la uchaguzi wa Igunga, kuna agenda zimefunikwa ambazo ni za msingi zaidi kwa wana-Igunga, lakini kwasababu ya ‘wapita njia’ waliopo kule, hatuzisikii zikiongelewa hata kwenye ripoti za vyombo vya habari.
Hivyo, moja ya sababu za kujihadhari na ‘wapita njia’ ni namna ambavyo wanafunika na kuziweka chini kabisa katika orodha, agenda na masuala ya msingi yanayohusika kwenye jimbo husika.
‘Wapita njia’ mara nyingi wanakuwa na malengo mengine kabisa; ambayo kwao ndio msingi mkubwa unaokuwa umewapeleka kule. Kwa mfano, wapo wanaokwenda kule na kuutumia uchaguzi husika kama ‘wasifu au cheti kisafi’ kwa wakubwa wao kuwa wamefanya kazi vizuri.
Hawa kazi yao kubwa ni kuhakikisha kwa njia zozote zile mgombea wao anashinda ili wapate sifa, na hata kupandishwa vyeo na wakubwa wao.
Wapo ambao wapo kule kuutumia uchaguzi huo kama karata ya ‘kuweka mambo sawa’ ndani ya vyama vyao. Kwamba kama wanashinda katika uchaguzi huo, ndio kipimo cha ama mambo ndani ya vyama vyao ni mazuri ama ndio yamechacha zaidi. Uchaguzi kama huo unakuwa ni kipima joto cha hali ya migogoro yao ndani ya vyama.
Kama hiyo haitoshi, wapo wanaoenda kule kwa lengo mahususi la kuongeza idadi ya viti vya ubunge katika vyama vyao. Tunajua kuwa kila chama kinakuwa na lengo kama hili, lakini kama chama husika kinaliweka lengo hili kuwa ndio kipaumbele kikuu, huku kikisahahu vipaumbele hasa vya jimbo husika na wakazi wake, hii si sawa.
Kuna haja gani ya kuongeza kiti cha ubunge kwa ajili tu ya chama bila kuweka na kuwaambia watu ni mikakati gani ‘kiti hicho mnachoongeza’ kitakuwa na tija katika kukabili matatizo ya jimbo husika; hususan Igunga?
Hapa ndipo tunapofikia mahali ambapo, badala ya kusikia uchambuzi wa kina kutoka kwa wagombea wa ubunge kupitia vyama mbalimbali kuhusu masuala ambayo ni ya msingi, na yanayopaswa wana-Igunga wahakikishiwe yatayasimamiwa, tunasikia masuala tofauti yasiyo kipaumbele kwao.
Yanayojaza macho na masikio yetu ni vijembe vya watu binafsi wa chama na chama, watu kushambuliwa, tuhuma za ugoni na mengine mengi.
Ni katika hatua hii wana-Igunga hawana budi washtuke na kutazama upya nini hasa ‘wapita njia’ wanaitakia Igunga katika miaka minne ijayo hadi pale watakapofanya uchaguzi mwingine wa kiti cha ubunge. Wakumbuke kuwa ni wao wenyewe ndio wenye uwezo wa kuhakikisha kuwa wanayemchagua ni shurti ayajue, ayaeleze kinagaubaga na kuweka kwa ufasaha ni kwa namna gani atayasimamia masuala ya Igunga.
Kwamba hao wanaojinadi wanautaka ubunge wa Igunga waeleze ni kwa jinsi gani watatatua kero ya miaka nenda rudi ya daraja la mto Mbutu. Daraja ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii kati ya watu wanaoishi upande mmoja kwenda mwingine wa mto huo; hasa wakati wa masika.
Kwamba, wanaojindai wanautaka ubunge wa Igunga waeleze ni kwa jinsi gani na ni mikakati gani wataiweka, wakishirikiana na wananchi wa eneo hilo, kuwakwamua wafanyabiashara wa ng’ombe, biashara ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa walio wengi, na hata kuweka mikakati madhubuti ya kuwaendeleza ili biashara hiyo iwaletee manufaa ziadi.
Kwamba, wanaojinadi wanautaka ubunge wa Igunga wana mkakati gani wa kushirikina na wana-Igunga kubadili dhana potofu kuwa Igunga ni sehemu kavu na palipo masikini, wakati ukweli ni kuwa kuna madini mengi yapo katika vijiji kadhaa. Na hivyo suala ni jinsi gani na mikakati gani inawekwa ili raslimali kama hizo ziweze kuwanufaisha wananchi, ni suala la kiongozi kushirikiana kwa karibu na wananchi na serikali kuwezesha hili.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo kwa wana-Igunga ni kipaumbele cha msingi katika uchaguzi huu mdogo. Wana-Igunga wanayajua vizuri zaidi masuala haya ambayo ni sehemu ya maisha yao.
Lililo la msingi zaidi, wakumbuke tu kuwa masuala haya ni ya muhimu zaidi kuliko vyama na tofauti zao za kiitikadi. Masuala haya yamebeba mustakabali wao na wa watoto wao au vizazi vijavyo. Masuala haya ni zaidi ya hao ‘wapita njia’. Wajihadhari nao.
Toa maoni yako