Wana-ndoa wengi Malawi wasema ni halali kupigwa na waume zao, wataja sababu tano

RIPOTI ya utafiti wa masuala afya na idadi ya watu (MDHS) nchini Malawi kwa mwaka 2015/2016 imebaini kwamba asilimia 16 ya wanawake nchini humo wanakiri kuwa ni halali kwa mume kumpiga mkewe.

Matokeo hayo ya utafiti ni kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Malawi (NSO). Ripoti ya utafiti huo ilizinduliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Goodall Gondwe, akiwa pamoja na Kamishna wa NSO, Mercy Kanyuka.

MDHS ni utafiti unaohusisha kaya ili hatimaye kupata takwimu za kitafiti zitakazosaidia nchi hiyo kuratibu shughuli za kijamii kama masuala ya afya na lishe.

Utafiti huo uliofanywa na NSO umefadhiliwa na serikali ya Malawi kwa kushirikiana na taasisi kadhaa zikiwamo USAID, UNICEF, NAC, UNFPA, UN Women, Shirika la Misaada la Ireland na Benki ya Dunia.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wanaounga mkono vipigo vya wanaume kwa wake zao wameainisha sababu kadhaa ambazo ni pamoja na wake hao kugoma kufanya mapenzi na waume zao, na wakati mwingine kuuguza chakula.

“Asilimia 16 ya wanawake na asilimia 13 ya wanaume wanakubali kwamba ni haki mwanamume kumpiga mkewe kwa sababu zifuatazo: endapo mwanamke atapika chakula na kukiunguza, mwanamke atabishana na mumewe, ataondoka nyumbani bila kumtaarifu mumewe, kutokuwajali watoto au kukataa kufanya mapenzi na mumewe,” inasomeka sehemu ya utafiti huo.

NSO imeeleza kwamba hii si mara ya kwanza kwa utafiti wa aina hiyo kutoa matokeo hayo na kwamba, tangu mwaka 2010 matokeo ya tafiti za aina hiyo yamekuwa yakifanana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo hivi karibuni, Waziri Gondwe alisema ni lazima takwimu hizo zitumike kikamilifu kutimiza malengo yaliyokusudiwa ambayo ni pamoja na kuboresha sekta ya afya nchini Malawi.

“Haitoshi tu kuishia kusikiliza matokeo ya utafiti huu, tunapaswa sasa kwenda mbali zaidi kuhusisha utafiti huu na hali halisi nchini. Kuchukua hatua stahiki kwa kushirikisha wadau wa maendeleo ,” alisema Gondwe.

Kwa upande wake, Kamishna wa NSO, Mercy Kanyuka alisema takwimu za utafiti huo zitasaidia wadau kutimiza wajibu wao kikamilifu kwa jamii.

Alisema matokeo ya utafiti huo ni muhimu kwa wadau mbalimbali kwa kuwa yatawasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Ripoti hiyo pia imebainisha kwamba wanawake kwa sasa wamekuwa mstari wa mbele katika kutumia njia za kisasa za kupanga uzazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo asilimia 58 ya wanawake waliofunga ndoa wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango kutoka asilimia 24 mwaka 2010.

Wilaya ya Chiradzulu ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, ikiwa na asilimia 68 na inayoshika mkia ni Wilaya ya Mangochi yenye asilimia 31.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), Littleton Tazewell naye alizungumzia utafiti huo akisema: “…ni lazima tuzingatie kuwa takwimu pekee haziwezi kuboresha maisha ya mamilioni ya raia wa Malawi.”

Akaongeza; “Takwimu ni chombo cha kututaarifu uhalisia ili hatimaye tufanye uamuzi sahihi. Takwimu zinatuwezesha kujua tutumie mbinu gani muafaka ili tufanikiwe.”

Utafiti huo umehusisha sampuli 24,562 za wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 katika kaya 26361, na pia umehusisha wanaume 7478 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 54.

One thought on “Wana-ndoa wengi Malawi wasema ni halali kupigwa na waume zao, wataja sababu tano”

  1. Ben says:

    Jamani, asilimia 16 ni WENGI kweli? Ebu tumieni weledi kidogo

    Anyhow, je na wanawake kuwapiga wanaume pia ni halali? Si mapenzi pande zote mbili? Kwanini wanaume tu waoneshe mapenzi na wanawake wasioneshe?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *