Wanakuza demokrasia, sisi tunashambulia waandishi

TUKIO la kutekwa na kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri wa Kampuni ya magazeti ya New Habari, Absalom Kibanda, limeendelea kuitia madoa nchi yetu katika upande wa demokrasia inayozingatia uhuru wa maoni na wa vyombo vya habari.

Aidha, kwa kuzingatia mfululizo wa matukio yanayofanana na hilo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara (kwa wananchi wa kawaida, waandishi wa habari, wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa makundi yanayotetea haki kwa njia za maandamano au migomo, na wengineo) ni dhahiri kuwa upo ulegevu mkubwa katika sekta ya usalama.

Kwamba, kama viongozi husika wa vyombo vya dola wamekuwa mahiri zaidi kuunda tu tume kuchunguza kilichotokea, huku tume hizi zikishindwa kuzuia kutokea tena kwa matukio ya aina, tafsiri yake ni kuwa kuna kufeli kwa hali ya juu katika kuzuia kutokea kwa matukio ya aina hii. Na tafsiri ya jumla zaidi ni kuwa kila mmoja wetu, hapo alipo, hayuko salama tena.

Kwa maneno mengine, kwa kutumia udhaifu uliopo katika vyombo vinavyotakiwa kuhakikisha usalama wa kila mmoja wetu (katika nafasi zetu anuai: iwe kiongozi, mwandishi wa habari au mwananchi wa kawaida), baadhi ya watu wamejipa uwezo na mamlaka ya kumshughulikia mtu yeyote aliye kinyume na matakwa yao.

Mtindo wa aina hii wa kushughulikia baadhi ya watu, katika nchi nyingine umekuwa ukifanywa na makundi fulani maarufu kama ‘Mafia’, ambayo hutumiwa ama na wanasiasa, wafanyabiashara au watu wengine, alimradi wakiwa na malengo yao mahususi (yaliyo kinyume cha sheria) kuyatimiza.

Yamkini hata hapa kwetu, kwa mlolongo wa matukio ya watu kushugulikiwa, makundi ya aina hii si kwamba tu kuna uwezekano yapo, bali pia yameshakomaza mizizi na labda baadhi ya watu walio katika mamlaka ama ni wahusika, au wanayakingia kifua na kuyafadhili kwa maslahi yao.

Kinachoshitua zaidi ni kuwa ‘washughulikiaji’ hawa wameamua kuwalenga zaidi wanahabari. Idadi ya waandishi ambao wamekuwa wahanga wa matukio ya aina hii inaendelea kuwa kubwa siku hadi siku: Saed Kubenea, Daudi Mwangosi, Mnaku Mbani, na sasa ni Absalom Kibanda.

Wanazuoni wa masuala ya demokrasia, siasa na utawala bora na wanafahamisha kwamba vyombo vya habari na shughuli zake ni sehemu na muhimili muhimu sana katika ustawi wa demokrasia. Pamoja na vyombo vya habari (vilivyo huru kutimiza majukumu yake), mihimili mingine ya demokrasia ni pamoja na  kuzingatia haki za binadamu, uwepo wa chaguzi huru na za haki, utaratibu unaozingatia kuwa wananchi wana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika mfumo wa siasa au uongozi.

Katika hali ya kawaida, matukio ya kushambuliwa waandishi kama ilivyotokea kwa Kibanda na wengineo huko nyuma hayatokei tu bila madhumuni maalumu. Kwa namna moja, yanafanyika ili kukandamiza na kudidimiza juhudi za waandishi wa aina yake katika kutekeleza majukumu yao. Kwa upande mwingine, yanalenga kurudisha nyuma maendeleo na hatua ambayo imefikiwa na tasnia ya habari hapa nchini. Hivi vyote vina athari mbaya katika ustawi wa demokrasia yetu.

Tukio la kushambuliwa kwa Kibanda limetokea wakati ambapo jirani zetu, hapo nchini Kenya, wakifanya uchaguzi wao mkuu. Kwa kulinganisha hili lililotukia hapa kwetu, na mchakato wa uchaguzi huo (ambao ni sehemu ya utekelezaji wa muhimili mmojawapo wa demokrasia), yapo mambo ya kujifunza, na kujipima nani kati yetu anapiga hatua mbele au kurudi nyuma katika kustawisha demokrasia.

Yaweza kujitokeza hoja kuwa hatuwezi kujifananisha na Wakenya kwa kuwa kama mataifa mawili tofauti, tumepitia historia tofauti tofauti. Historia hizi ni pamoja na hali (kiuchumi, kisiasa na kijamii) tulizorithi baada ya Uhuru, mifumo ya kisiasa tuliyoamua kufuata baada ya Uhuru na hata aina ya watu/makabila tuliyonayo, pamoja na matukio ambayo kila taifa limeyapitia hadi leo, yanaleta ugumu katika kufanya ulinganifu.

Pamoja na hayo, bado upo umuhimu kwa kujilinganisha na Wakenya kwasababu, sote kama watu wa ukanda wa Afrika ya Mashariki yapo masuala mengi tunayoshabihiana ikiwemo mila, desturi na tamaduni zetu. Vilevile, sote tumeamua kufuata aina inayofanana ya ‘mfumo wa demokrasia’ ya vyama vingi, na inayozingatia mihimili niliyoitaja hapo awali ikiwemo kuwa na vyombo huru vya habari na utaratibu wa kuwa na uchaguzi katika kupata viongozi.

Ingawa hali ya tofauti za kikabila nchini Kenya, ambayo ilipelekea uwepo wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, haijapata dawa ya kutokomezwa kabisa, kwa kutazama namna ambavyo wameendesha uchaguzi wao mwaka huu, ni dhahiri kuwa wenzetu wanafanya juhudi kubwa sana ili kudumisha demokrasia, wakati sisi tukiwa tumebweteka, na kudhani kuwa tunasonga mbele.

Lakini kumbe, kwa matukio kama ya kushambulia waandishi (na hata wapigania haki wengine), ni dalili kuwa sisi tunarudi nyuma, tukijipambanua kama tusioweza kuwa na ustahimilivu na uwezo wa kuvumiliana katika tofauti zetu za kimtazamo na kadhalika. Kama alivyowahi kunena Kiongozi wa zamani na baba wa taifa la India, Mahatma Gandhi, ‘Intolerance is itself a form of violence and an obstacle to the growth of a true democratic spirit’ (Kwa tafsiri isiyo rasmi, ‘ukosefu wa uvumilivu ni aina ya ghasia na kizingiti katika ukuaji wa demokrasia ya kweli’).

Kati ya hatua kubwa ambazo wenzetu wamepiga ni kuendesha mdahalo kati ya wagombea wa Urais, huku masuala muhimu kwa maendeleo ya taifa kama vile ardhi, uadilifu wa viongozi na mipango ya wagombea katika kuinua vipato vya wananchi yakitawala. Suala la msingi zadi ni namna ambavyo kulikuwa na uvumilivu wa hali ya juu kati ya wagombea, na namna walivyojikita zaidi katika hoja na ufafanuzi wa masuala hayo ya kitaifa.

Hata kama kuna kasoro za hapa na pale katika mchakato wote wa Uchaguzi wa Kenya, ukweli ni kuwa ni dhahiri kwamba wenzetu, kwa kutumia pia na katiba yao mpya, wamepiga hatua kubwa katika kujibidiisha kudumisha demokrasia.

Tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwa wenzetu. Ni heri basi nguvu nyingi zinazotumika kupanga na kutekeleza matukio ya kuzima juhudi za wanaodumisha demokrasia ikiwemo waandishi, zibadilishwe na kuwa nguvu njema za kutatua matatizo yetu kama kitaifa kama vile elimu inayopromoka, rushwa na umasikini.

One thought on “Wanakuza demokrasia, sisi tunashambulia waandishi”

  1. kanyambala says:

    Uchu wa madaraka, kulewa sifa, ufisadi na siasa zilizojaa uwongo ndiyo zimetufikisha hapa tulipo leo. Chama tawala hakijui tena uzalendo. Wameshika hatamu hawajui farasi watampeleka wapi. Akili yao yote ni kushika hatamu, wamesahau kuwa ukishika hatamu, unatakiwa umuongoze farasi muelekeo! Inatisha hapa tulipofikia, kwamba tumepoteza muelekeo, kila mtu anaeweza kuongea anaongea anavyotaka. Udini ndiyo huo, vyama ndiyo hivyo, bunge ndiyo hilo! Hakuna tena mipango wala nini. Elimu ndiyo hiyo inayoyoma. Kilimo kwanza kimetanguliwa na njaa kila kona. Mazingira yanaharibika kila kona, wakuchukua twiga wanabeba, wakuchinja Tembo, wanachinja, mapori yanayoyoma, mito inakauka, watu bado wanang'ang'ana kugombea hatamu! Kama kweli Chama tawala wangekuwa ni Wazalendo, nadhani wafike mahali wao wenyewe waseme jamani tumechoka, sasa ngoja tukae pembeni, wengine wajaribu, kama kuna chembe ya uzalendo imebaki ndani yao, maana taifa linaangamia na wao wapo, inakuwaje? Mbona wanapoingia kugombea madaraka wanafanya fujo zote kama abiria wa Mbagala, halafu wakifika , wanakaa wanabweteka, tuliii?! Serikali ya CCM ituambie, kunani! Mmechoka mno, kubalini tu, maana mtatufikisha pabaya jamani!!!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *