“PADRE Mapunda Tunda la Kanisa je, umepigwa marufuku na Kardinali Pengo usiongelee tena siasa au unaogopa kushughulikiwa na CCM?” hili ni swali kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa makala zangu katika gazeti hili, msomaji huyu na wenzake waliniandikia kutaka kujua kilichonipata baada ya kukosekana kwa makala zangu katika gazeti hili.
Majibu yangu kwake na wenzake ni kwamba; “Mimi ni mtu huru na ninawajibika kwa Yesu na wakubwa wangu na ndiyo waajiri wangu na si serikali yoyote hapa duniani.
“Ndani ya kanisa najua nafasi yangu na sheria za kanisa langu ninalolipenda tangu kuzaliwa kwangu mwaka 1959. Siwezi kubabaishwa na maneno ya mitaani kamwe. Msimamo wangu ni mmoja, kama unahoja, njoo tuzungumze ana kwa ana na siku hiyo chakula cha mchana utalipa wewe na nitaongelea mambo ambayo hujawahi kuyasikia tangu taifa lizaliwe, kama upo tayari karibu sana!
Yesu alisema kwamba “utawala uliogawanyika haufai kabisa” katika moja ya hotuba zake. Utawala inabidi uwe na umoja, upendo na mwelekeo unaoeleweka. Yesu kama kiongozi alikuwa na kazi kubwa sana ya kujenga maadili katika chuo chake cha Mitume (Chuo Kikuu cha Maisha cha Yesu Kristo).
Sera ya chuo hicho ilikuwa ni Upendo, Unyenyekevu na Utumishi; kwa kifupi (U3). Yesu alisisitiza kwamba wale ambao wanakuwa mabosi lazima wawe watumishi wa watu. Lakini sera hii inapingana na sera ya dunia hii. Ukweli ni kwamba katika dunia hii “bosi” ni mtawala na anatumikiwa.
Matokeo ya sera hii ni kuanguka, kwa sababu inapingana na sera ya uongozi wa Mungu. Daima watu wanajidanganya siku ya kuapishwa kwamba “mamlaka yote yatoka kwa Mungu” lakini inakuwa ni ukasuku tu wala watu hawajaribu kuelewa maana ya maneno haya. Mwisho wake ni anguko, tena anguko baya sana kama lile la mnara wa Babeli kwa sababu ya majivuno na kujiamini mno kwa watawala.
Walatini wanasema kwamba “ Vox populi, Vox Dei” yaani sauti ya wengi, ni sauti ya Mungu” na kwa upande mwingine, Yesu alisema kwamba “mimi ni mchungaji mwema, mchungaji mwema hujitoa kwa ajili ya kondoo wake” (John 10:10).
Tujiulize je, viongozi wetu wa Serikali na chama tawala wanajitoa kweli kweli au ni ubabaishaji tu katika kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wa kivyama, ukanda au udini?
Kwa kuzingatia matukio mbalimbali ya mauaji kwa wasio na hatia nchini, uporaji haki kwa wasio na uwezo, tuendelee kujiuliza; je, Watanzania tunaweza kujigamba kwamba tupo huru? Uhuru wa bendera sawa, wa kimawazo, na uhuru wa rasilimali zetu je? Leo Watanzania wengi wanalalamika kwamba wageni wanafaidi mali zetu kuliko sisi wenyewe. Serikali imekwenda likizo? Natamani Nyerere afufuke leo halafu tungeona serikali ingejibu nini.
Matukio ya hatari nchini yanazidi kuongezeka kiasi kwamba binafsi naelekea kuogopa kuishi nchini Tanzania, nilifikiri Kenya ilikuwa hatari kwangu kumbe si hivyo. Kibaya zaidi, baadhi ya matukio ya unyanyasaji Tanzania yanaanza kuzoelekea na kuonekana ni kero ndogo tena za kawaida tu.
Viongozi hawana majibu sahihi kwa kero nyingi za wananchi, wakiamini kwamba Watanzania bado hawana utambuzi wa kutosha kuhusu haki zao. Kiwango cha utambuzi wa haki miongoni mwa wananchi kimeanza kuwachanganya viongozi, hawajielewi na wengine wanabwatuka na kukasirika hovyo, wakiishia kutoa matusi badala ya majawabu ya matatizo ya wananchi.
Mkutano wa NEC ya CCM wiki iliyopita na hata mingine iliyowahi kufanyika haijafanya uamuzi wa kujivunia. Ingawa yapo masuala yaliyoamuliwa yakibeba sura ya kuwasaidia Watanzania lakini kama kawaida, ugonjwa wa kudumu katika chama hicho na serikali yake ni kukosekana kwa ari ya utekelezaji. Hakuna utekelezaji wenye nia ya dhati.
Chama cha CCM kilijiamini mno kupita kiasi. Sasa ni wazi kimechokwa na baadhi ya wananchi mijini na vijijini. Nilipokwenda nchini Uingereza kusomea madhara ya pombe niliambiwa na mmoja wa washauri nasaha kwamba; “yaani kwa kawaida watu wote kijijini kwenu wanajua kuwa wewe ni mlevi, ila wewe tu ndiyo hujui.”
Kwa hiyo basi, ni dhahiri kuwa siasa za kujidanganya kwa upande wa CCM hazitawasaidia ni vema wakakubali kwamba kuna shida ndani ya chama chao kitukufu.
Ni vema Watanzania wakaelimishwa kuna vyama mbadala katika kuongoza nchi na kwamba uongozi wa nchi si taji maalumu kwa ajili ya CCM. Binafsi, naamini chama mbadala ni CHADEMA.
Ni kwa mantiki hii, naamini kuendelea kuichagua CCM ni kuendelea kuridhia udhaifu wa kiutendaji serikalini na katika taasisi nyingine nje ya Serikali.
Tumejionea wenyewe kwamba wakati wa kikao cha mwisho cha Bunge lililopita, Zitto Kabwe alitoa hoja ya kumwajibisha Waziri Mkuu na waliosaini ile fomu ni wabunge watano tu wa CCM kati ya 253.
Je, hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba wabunge wengi wa CCM hawapo tayari kushughulikia suala la ufisadi kwa sababu lipo ndani ya chama chao. Haya ni maoni yangu na nina haki ya kuyasema leo na siyo kesho.
Nikiwa kama Mtanzania na mzalendo nafurahi kushiriki katika kuongoza na kutoa maoni yangu juu ya hali ya kisiasa katika nchi ya Musa ( Mwalimu Nyerere). Watanzania lazima tuwajibike katika kuiongoza nchi yetu kuanzia serikali za mitaa hadi taifa na hii ni imani ya TANU na baadaye ya CCM.
Mwisho napenda kuwapongeza wabunge wa upinzani na wale wachache wa CCM walitoa changamoto juu ya wale mawaziri nane, nasema hongereni sana. Lakini mimi nasema bado mapambano yaendelee.
Nasisitiza kwamba, wananchi wakiukataa uongozi maana yake ni Mungu ameukataa kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.
Vilio vya Watanzania wengi na machozi yao Mungu lazima atasikiliza tu, kwani yeye ni Baba wa wote bila kubagua. Mungu ataendelea kutenda kwa jili ya watu wake wanaomlilia kwa dhati. Watanzania tuendelee kutafakari kwa kina juu ya nchi yetu ilikotoka na inakokwenda, je ndiko tunakotaka iende?
Mjadala wa kuandika Katiba mpya tuwe macho nao kwa sababu mwovu shetani angependa kuingilia katika masuala ya Muungano ambao ni muhimu kujadiliwa, madaraka makubwa ya Rais, masuala ya kuingiza OIC na Mahakama ya Kadhi katika Katiba mpya, suala ya kushitakiwa Rais aliyepita kama aliboronga na hatari ya kupindisha mambo kama vile kuweka zamu ya urais kwa Tanganyika na Zanzibari kitu ambacho hakina maana kwetu.
Nionavyo mimi kunauwezekano mkubwa wa kupotosha ukweli wa mambo katika Katiba hii kama hatutakuwa makini. Nampongeza Profesa Issa Shivji kuanzisha vipindi vya kuelimisha umma kuhusu masuala ya Katiba.
Kujitolea kwa namna hii ni alama kwamba Mungu hapendi Tanzania kuingia katika machafuko kupitia Katiba mbaya, tazameni yanayotokea Kenya ambayo ni matokeo ya kuweka ajenda za siri katika Katiba kama ndoa za mashoga na utoaji mimba.
Toa maoni yako