Habari
Wananchi walia na Mgodi wa Geita
Mwandishi Wetu
Toleo la 226
15 Feb 2012

SHUGHULI za uchimbaji dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita, Bulyanhulu, Wilaya ya Geita, mkoani Mwanza na hasa ulipuaji miamba, zimeanza kusababisha madhara kwa makazi ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo, Raia Mwema, limeelezwa.

Wakazi walioanza kupata athari kutokana na shughuli za mgodi huo ni pamoja na wanaoishi katika kata ya Mwingiro ambao vishindo vya mipasuko ya miamba mgodini humo vimekuwa vikisababisha nyufa katika nyumba zao.

Kata hiyo ya Mwingiro inaundwa na vijiji viwili vya Mwasabuka na Eyenze pamoja na vitongoji vya Stamiko na Iyogero.

Akizungumza kwa simu na mwandishi wa gazeti hili, diwani wa kata ya Mwingiro, Hamisi Temela, alisema hali hiyo ilianza kujitokeza tangu mwaka jana, baada ya wananchi wa kijiji cha Mwasabuka kuhofia maisha yao, hasa baada ya kutokea matetemeko mfululizo ya ardhi kwa siku kadhaa kati ya saa 11 na 12 asubuhi.

“Yanayotokea mgodini yanakuja kwenye kata yangu, awali ilikuwa mipasuko lakini kwa sasa hofu imeongezeka kutokana na matetemeko makubwa ya ardhi yanayotokana na upasuaji wa miamba,” alisema Temela na kuongeza:

“Hali hiyo imetufanya kuamka mapema asubuhi na kusikilizia matetemeko hayo yaliyokuwa yakisikika kutoka chini ya ardhi tukiwa nje ya nyumba zetu,” alisema.

Alisema hali hiyo imeendelea kuwa mbaya zaidi baada ya nyufa kuanza kujitokeza kuanzia mgodini hadi kwenye makazi ya watu.

“Baadhi ya wanakijiji ambao nyumba zao zimepata nyufa kutokana na shughuli za mgodi ni Idd Ibrahim pamoja na Mgeshi ambao wote ni wanakijiji wa kijiji cha Mwasabuka katika kitongoji cha Stamiko, kata ya Mwingiro,” alisema Temela.

Kwa mujibu wa diwani huyo, waliwasilisha malalamiko kuhusu tukio hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Philemon Shelutete na uongozi wa wilaya kupitia ofisa madini.

Waliwasilisha malalamiko hayo kupitia barua ya Oktoba 19, mwaka jana, yenye kumbukumbu namba DA.241/451/01/V.III/124.

Mbali na hatua hiyo, walifanya mazungumzo moja kwa moja na mkuu wa wilaya pamoja na mtendaji mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdul Mruma na kwamba, baadaye jopo la wataalamu kutoka GST, walifika katika eno husika kwa uchunguzi zaidi.

Baadhi ya watendaji wa vijiji hivyo wameeleza kusikitishwa na ukimya wa Serikali kuhusu tatizo hilo licha wao kuwasilisha taarifa mapema.

“Jambo linalotufanya tuwe na mashaka ni ukimya wa Serikali katika kulishughulikia suala hili, mkuu wa wilaya alileta wataalamu baada ya sisi kumpelekea malalamiko lakini tunashangaa hali inazidi kuwa tete na hatusikii kauli yoyote kutoka serikalini,” alisema mmoja wa watendaji hao.

Mkuu wa Wilaya alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kushughulikia tatizo hilo kwa kuzingatia malalamiko ya wakazi wa maeneo husika, hakuwa tayari na kusisitiza kuwa hana taarifa zao.

“Sina habari wala sifahamu chochote, wanaongea habari za uongo labda kuna hicho wanachokihitaji,” alisema Shelutete.

Alipokumbushwa kwamba ni yeye ndiye aliyetajwa kupeleka timu ya wataalamu wa wakala wa jiolojia katika maeneo hayo kuchunguza mipasuko hiyo baada ya wananchi kulalamika kisha kukalia ripoti kwa sababu anazozijua yeye, kiongozi huyo aligeuka mbogo kuwa hizo taarifa ziko hadi wizarani na kwamba hawezi kutoa ufafanuzi kwa kuwa gazeti hili lilikwisha kuzungumza na vyanzo vingine.

“Kama una taarifa basi waambie hao waliokupatia taarifa wakupe na nyingine, ungekuja kwangu ningekupa taarifa nilizonazo, lakini kwa kuwa wamekupa wao basi nenda wakakupe, ninachofahamu mimi hizo taarifa ziko mpaka wizarani,” alisema.

Naye ofisa uhusiano wa mgodi huo aliyejitambulisha kwa jina moja la Chaula, alipoulizwa juu ya tatizo hilo alisema suala hilo ni zito linalohitaji uchunguzi wa kina na kwamba hawezi kulizungumzia na kwamba, mwenye uwezo huo ni meneja mkuu wa mgodi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi alimtaka mwandishi wetu kuzungumza na mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania.

“Nipo kikaoni mpigie mtaalamu wetu Profesa Mruma, Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania awape maelezo,” alisema Waziri Ngeleja.

Gazeti hili lilipomtafuta Profesa Mruma alikiri timu ya watalaamu kufika eneo hilo la wanakijiji.

“Nipo Cape Town (Afrika Kusini) kwa sasa, lakini ni kweli tumekwenda tumepachunguza, tumechukua takwimu na tunazifanyia interpretation (tafsiri), matokeo yakitoka nitayatolea maelezo ya kina,” alisema Profesa Mruma kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Hata hivyo, wakati gazeti hili likiendelea kufuatilia suala hilo kwa watu mbalimbali, ofisa uhusiano wa mgodi huo, Chaula alikana majibu yake ya awali aliyoyatuma kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu.

“Nashauri uwaulize waliokupa hizo taarifa, naambiwa kuna wataalamu walikuja kufanya utafiti hatujui aliwaleta nani, hatuna ripoti ya matokeo ya utafiti wao. GM haina taarifa ya jambo hilo,” unasomeka ujumbe wa huo mfupi wa maandishi wa Chaula.

Ripoti ya kitaalamu Januari 10, 2012, mtaalam wa jiolojia pamoja na mtaalamu wa jiofizikia , (majina yanahifadhiwa kwa sasa ), walisema vipimo vyao walivichukua kwa kutumia teknolojia ya precision magnetometer GSM19TW ambayo ni maalumu kwa kupima hali ya miamba iliyoko chini ya ardhi.

Majibu ya awali ya vipimo hivyo vilionyesha uwepo wa kijiji hicho karibu na maeneo ya mgodi hivyo kuhofia kwamba huenda mipasuko hiyo ikawa imesababishwa na shughuli za mgodi au matetemeko ya kawaida ambayo yanaweza kuwa yamepasua miamba aina ya Geu (metamorphic rocks) na miamba moto (Granite) ambayo ndiyo iko katika eneo hilo.

Nyufa zilizoonekana katika utafiti huo zinaelezwa kuwa na upana wa kati ya nchi moja hadi futi mbili na urefu wa hadi mita 100 na kina cha hadi mita moja na nusu.

Kwa upande wao wananchi wa vijiji hivyo vilivyoathirika wanaiomba Serikali kufanya mpango wa kuwahamisha kwa kuwa hivi sasa wanaishi kwa hofu kubwa.

Baadhi ya wananchi hao walihoji uhalali wa mgodi wa Bulyanhulu uliodaiwa kuwa Mkoa wa Shinyanga Wilaya ya Kahama kufanya shughuli za uchimbaji katika vijiji vya Geita ilihali mapato yote yanapelekwa Kahama.

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.