Wananchi walindwe mwisho wa mwaka

TOLEO lijalo la gazeti hili litatoka mwezi Desemba mwaka huu. Ni kwa sababu hiyo basi tumeona ni vema tuweke rai yetu mapema kabla mwezi huo haujafika.

Kama ilivyo ada duniani kote, siku za mwishoni mwa mwaka watu wengi huzitumia kusafiri kwa ajili ya kupumzika na kwenda kusalimu ndugu, jamaa na marafiki.

Kwa Tanzania, na bara la Afrika kwa ujumla, huu ni utaratibu muhimu kwa vile bado sehemu kubwa ya wananchi wanaishi vijijini kuliko mijini.

Kwa miaka mingi sasa, umekuwa utaratibu wa kawaida kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma za mabasi na usafiri mwingine wa kwenda mikoani, kupandisha bei zao wakati huu wa mwishoni mwa mwaka.

Limekuwa jambo la kawaida kuona nauli kutoka mikoa mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya kwenda mikoani ikipanda maradufu – wakati mwingine mara tatu kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu.

Bei hizo hupandishwa hata kama umbali ni uleule na bei ya mafuta pia ni ileile. Matokeo ya tabia hizi ni kuwaumiza wananchi wa kawaida ambao kusafiri kwao hakumaanishi kwamba wana fedha nyingi za kutumia.

Inafahamika kwamba wananchi wengi wamekuwa wakilia kuhusu hali ngumu ya kiuchumi iliyopo hapa nchini hivi sasa kwa takribani miezi sita sasa.

Wananchi hawa watakuwa wanakamuliwa damu zao, na si jasho pekee, kama serikali itaamua kuwaacha katika mikono ya wafanyabiashara mumiani wanaoamini katika kupata faida kwa gharama yoyote.

Tumeeleza kuhusu usafiri pekee lakini rai hii inahusu biashara za namna yoyote kwenye bidhaa na huduma. Badala ya kufikiria kuumiza wananchi, inabidi sasa ifikiriwe namna ya kuwakwamua.

Kwa namna ya kipekee kabisa, tunapenda kuziomba mamlaka husika zote; chini ya mwamvuli wa serikali, kuhakikisha kwamba wananchi walindwa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka na sikukuu zake.

Tunafahamu kwamba wajibu huu wa kuwalinda watumiaji wa huduma na bidhaa unatakiwa kuenziwa katika wakati wote wa mwaka lakini tunadhani kwamba kuna tabia ya kukithiri kwa vitendo hivyo mwishoni mwa mwaka kuliko wakati mwingine wowote.

Hii ni nchi yetu na wananchi wanaoumizwa na wananchi wenzetu pia. Serikali inatakiwa kuweka msimamo wake mapema na kwa uwazi kabisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *