KATIKA sehemu ya pili ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi mataifa makubwa ya Magharibi kwa maana ya Marekani na Uingereza kwa upande mmoja, na yale ya Mashariki, kwa maana ya Urusi na China kwa upande wa pili, yalivyokuwa yakishindana kuteka siasa za Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Tuliona jinsi Marekani, kupitia Shirika lake la Ujasusi (CIA) ilivyoshika hatamu katika kudhibiti Zanzibar isiangukie kambi ya Mashariki kwa kutekwa na sera na siasa za Kikomunisti na kijeshi zilizokuwa zikitetewa na wanaharakati wa Kikomunisti Visiwani humo wakiungwa mkono na kupewa nguvu na nchi za Mashariki, zikiwamo Urusi, China, Ujerumani Mashariki na Czechoslovakia.
Tuliona jinsi baada ya Mapinduzi hayo, China ilivyomwaga kama msaada, mabilioni ya fedha na silaha za kivita nzito nzito, kubwa na kali kwa Serikali mpya ya Mapinduzi, huku Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara, Abdulrahman Mohamed Babu, akiratibu na kusimamia kwa makini kuingia kwa Ukomunisti Visiwani na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Ili kuepusha Zanzibar isiangukie kambi ya Mashariki (Ukomunisti) enzi hizo za vita baridi, Marekani ilibuni mikakati miwili ya ama kuundwa kwa Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki, ambapo nchi hiyo ingemezwa isifurukute; au Uingereza kuivamia Zanzibar kijeshi na kuweka watawala vibaraka ili kuzima fikra za Kikomunisti kutawala Zanzibar, kama juhudi za kuunda Shirikisho zingeshindwa.
Tuliona pia jinsi Waziri wa nchi (Usalama) wa Marekani, Dean Rusk, alivyoongoza juhudi za kuzuia ushawishi wa “Wakomunisti” Visiwani kwa kuwashirikisha mabalozi wa nchi yake nchini Tanganyika, Uganda na Kenya pamoja na watawala wa nchi hizo.
Ushahidi wa harakati hizi unafifisha ile dhana kongwe kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa hiari (bila shinikizo), ambapo inadaiwa kwa kupotosha kwamba Rais wa Tanganyika, Julius Kambarage Nyerere alipendekeza suala la Muungano kwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, naye bila kusita, akakubali na akapendekeza Mwalimu Nyerere awe Rais wa Muungano huo.
Dhana hii inapingana pia na ukweli kwamba, wiki chache tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Serikali ya Tanganyika iliwatuma Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Kambona na Bibi Titi Mohamed, Naibu Waziri na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama tawala cha “Tanganyika African National Union” (TANU), kumshawishi Karume akubali Muungano kati ya nchi zao mbili, lakini Karume alidai alihitaji muda zaidi kufikiri juu ya jambo hilo. Kama ni kweli kwamba Karume ndiye aliyependekeza Muungano, ilikuwaje awagomee mawaziri hao wawili waliotumwa na Mwalimu, na TANU?
Hata ule ujumbe wa pili uliowahusisha Mawaziri wa Tanganyika, Tewa Said Tewa na Job Lusinde, Februari 9, 1964, haukuweza kumgeuza mawazo Karume akubali haraka suala la Muungano, ulipokwenda Zanzibar kuwasilisha ujumbe wa Nyerere siku hiyo.
Bado hapajatolewa ufafanuzi yakinifu, ni kwa sababu gani Mwalimu Nyerere, mwaka mmoja tu kabla ya Uhuru wa Tanganyika, alisema, kama angekuwa na uwezo wa kukisukuma Kisiwa kile (Zanzibar) katikati ya Bahari ya Hindi, angefanya hivyo bila kusita?
Hii inathibitisha hofu ya Nyerere juu ya Zanzibar tangu mwanzo kwamba, moja ya matatizo makubwa kwa Tanganyika kwa miaka mingi lingekuwa Zanzibar. Je, haikusemwa tangu zama za enzi za utumwa kwamba, “Zanzibar inapopiga chafya” Bara hupata mafua? Je, si kweli hadi leo kwamba Zanzibar inapokohoa Tanzania Bara na Muungano hutikisika?.
Je, tuseme kwamba Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa katikati ya vita baridi kati ya mataifa ya Magharibi na mataifa ya Mashariki, ulikuwa ni kutimia kwa utabiri wa Mwalimu Nyerere, kwa kisiwa hicho (Zanzibar) ‘kutuumiza kichwa hadi leo?”.
Aprili 1, 1964, Balozi wa Marekani (na jasusi pia) nchini Zanzibar, Frank Carlucci, alipendekeza kwa Serikali yake ibadili mbinu za propaganda Visiwani.
Alisema: “Wakati ni wajibu wetu na kwa manufaa yetu kupiga kampeni dhidi ya (Abdurahman) Babu ambaye ni tishio kwa sera za kutofungamana na upande wowote (Magharibi au Mashariki), ningependekeza pia ziletwe silaha kwa wingi; hivyo washauri wanadiplomasia nao, kwamba, badala ya kuendelea kutegemea wenyeji pekee juu ya hali tete ya Zanzibar, wahusishe jamii ya kimataifa pia.
Swali lililoulizwa na wengi, ni kwa nini Kisiwa kidogo kama Zanzibar kipelekewe silaha na jeshi la kigeni, wakati tayari kulikuwa na kikosi cha Polisi 300 kutoka Tanganyika, kama kwa kufanya hivyo haikuwa mipango ya uvamizi wa kijeshi ya Marekani? Na kwa nini mtu mchangamfu, mcheshi na mwenye visheni kubwa kama Babu, awe tishio kwa sera za Marekani na Uingereza za kutofungamana na upande wowote?
Wakati huo, Waziri Dean Rusk alikuwa amekwishakuanza kupoteza subira pamoja na washirika wake wa Kiingereza. Alitaka mpango wa ZAP (uvamizi wa kijeshi) utekelezwe mara moja. Ndipo Machi 29, 1964 alipomwandikia Balozi wa nchi yake mjini London akisema: “Tumeshitushwa na ulegevu, udhaifu na kutojali kwa Uingereza juu ya hali tete nchini Zanzibar…… Zanzibar pekee si tatizo kwetu, lakini Zanzibar kama kituo cha harakati za Kikomunisti dhidi ya nchi za Afrika Mashariki ni jambo jingine; tunashindwa kujua kwa nini Waingereza wanashindwa kulielewa hilo”.
Dean Rusk alimaliza kwa kushauri kwamba, kama Uingereza haikuwa tayari kwa uvamizi basi, Marekani itume wanajeshi wake, na mara tu watakaposhambulia, bila shaka Uingereza nayo itaona aibu na kujiunga katika uvamizi huo.
Machi 30, 1964, Carlucci alituma taarifa kwa Dean Rusk akishauri Marekani imhonge Karume na kile alichokiita “hongo kubwa” ya kutosha, alisema: “Ni vyema tumpe Karume zawadi kubwa itakayomgeuza nia. Wazo linanijia kwamba, tumpe Helikopta na rubani wa Kimarekani……kukataa kwake (rushwa hiyo) kutamaanisha hayupo pamoja nasi na hivyo kutufanya tuchukue uamuzi mwingine na makini zaidi”.
Hata hivyo, Uingereza iliendelea kukaa kimya juu ya mipango ya Marekani, pengine kwa kusubiri matokeo ya mazungumzo ya wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika juu ya uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, yaliyopangwa kufanyika Aprili 10, 1964.
Mazungumzo ya wakuu hao yalivunjika bila kufikiwa mwafaka juu ya Shirikisho, hapakuwa wala na dalili za uwezekano wa mazungumzo hayo kurudiwa.
Aprili 18, 1964, Oscar Kambona alimweleza Balozi wa Marekani nchini Tanganyika, Leonhart, juu ya mpango wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar. Naye Leonhart aliitaarifu Washington kama ifuatavyo: “Kinachoendelea sasa kinaendana na uvumi ulioenea mjini London….. kwamba Babu hataruhusiwa kurejea Zanzibar. Hata hivyo bado, Zanzibar ya akina Hanga na Twala si ile tunayotaka, lakini huenda Kambona akahitaji msaada kwa njia moja au nyingine kutoka kwetu kwa niaba ya Hanga juma lijalo”.
Uamuzi wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, ulifikiwa wakati Babu akiwa safarini Indonesia ambapo kabla ya kuondoka alimtahadharisha Karume wakakubaliana kwamba, suala la Muungano liachwe kwa sababu lilikuwa na harufu ya ubeberu na ukoloni mamboleo wa Kimarekani na Uingereza. Kassim Hanga alipendelea Muungano, Babu aliupinga na Karume akababaika kwa miamba hao wawili kutofautiana kimitizamo.
Yapo maelezo yasiyothibitika kwamba, Babu alikwenda mbali zaidi kwa kuleta wakili kutoka Tanganyika kutetea hoja yake kwamba, chini ya Serikali ya Muungano, Zanzibar ingemezwa na Tanganyika, na kwa sababu hiyo Muungano ungezima historia ya Mapinduzi. Ni kwa sababu hii Nyerere alikwepa sana kuzua dhana ya Zanzibar kumezwa kipindi choche cha Muungano.
Leonhart alitahadharisha akisema: “Lazima tuchukue hatua haraka…….Jaribio lolote la kumwondoa Babu, Rashid na wafuasi watiifu kwao, linaweza kuleta ghasia na machafuko yanayoweza kuhitaji nguvu za kijeshi za ziada kutoka nje kutuliza hali au kuzuka kwa vita”.
Akijibu taarifa ya Leonhart, Naibu Waziri wa nchi wa Marekani, George Ball alisema: “Marekani inatoa baraka zote, na inaunga mkono juhudi za Tanganyika juu ya Shirikisho au Muungano wa Tanganyika – Zanzibar……..Kwa sasa hatujafahamu bado kiwango cha msaada Marekani itatakiwa kutoa kama upo, ambao Kambona huenda akahitaji atakapokuona Aprili 20, 1964”.
Tena akasisitiza: “Ni muhimu Kambona akashauriwa aanzilishe maombi ya msaada atakaohitaji kutoka kwetu ili ionekane juhudi za Muungano huu ni za Kiafrika kuweza kuficha ukweli (kwamba ni shinikizo) isije ikaonekana kwamba Marekani imeshinikiza Muungano huo, au kwamba tunataka kunyakua madaraka”.
Naibu Waziri huyo, George Ball, aliendelea kumwelekeza Balozi Leonhart akisema: “Pamoja na hayo, iwapo itaonekana inafaa kujitolea kwa yafuatayo ili kutimiza malengo yetu, waweza kufanya hivyo: moja, ukubali mpango uliotolewa na Kambona kuwezesha kuundwa kwa umoja (Muungano) wa Tanganyika na Zanzibar ambao utamwengua Babu na wenzake.
Pili, ashiria na onyesha utayari wa Serikali ya Marekani wa kuunga mkono juhudi zote za muda mfupi kwa Serikali ya Muungano; tatu, mhakikishie Kambona kwamba, Serikali ya Marekani iko tayari kufikiria mara moja maombi yoyote ya msaada”.
Kadri siku zilivyopita kuelekea kwenye Muungano, Balozi Leonhart alijipa kazi ya kutoa taarifa Washington juu ya matukio kila siku. Aprili 20, 1964, alituma taarifa ifuatayo: “Mradi wa Tanganyika – Zanzibar umefikia hatua ngumu. Matukio ya mwisho wa juma ni kama ifuatavyo:
“(a) Kambona aliondoka kwenda Tabora na Kigoma Aprili 18, mchana. Saa chache baadaye amri ilitolewa kukodi ndege za Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA) kuwaondoa Polisi 300 wa Tanganyika kutoka Zanzibar waliokwenda kuimarisha usalama. Haifahamiki kama hatua hii imetoka nje ya Serikali ya Tanganyika au ndani ya Serikali hiyo ili kumshinikiza Karume (akubali Muungano).
“(b) Karume alitua Dar es Salaam peke yake Aprili 18, mchana kwa Ndege ya Serikali ya Tanganyika iliyotumwa Zanzibar kumchukua Hanga. Tunavyofahamu, Karume alibakia Dar es Salaam siku nzima ya Aprili 19. Kuwapo kwake Dar es Salaam hakukutangazwa.
“(c) Kambona alirejea Dar es Salaam Aprili 19, siku moja kabla ya alivyotarajiwa na aliwaambia waandishi wa habari uwanja wa Ndege kwamba Nyerere alimwita.
“(d) Amri ya kusitisha kuondolewa kwa Polisi 300 wa Tanganyika huko Zanzibar ilitolewa baadaye Aprili 19. Kambona amesema ataitisha baadaye mkutano haraka iwezekanavyo”.
Hapa ifahamike kwamba, kusitishwa kwa amri ya kuondolewa kwa askari hao 300 Zanzibar, ilikuwa ni kufuatia Karume kusalimu amri kwa shinikizo la Nyerere la kutaka Muungano, ambapo mwanzo alikataa na Nyerere akatishia kuwaondoa ili Karume anyukwe na mahasimu wake.
Siku chache baadaye hata hivyo, mwandishi wa habari mashuhuri wa Kiingereza, Colin Legum, alibainisha katika gazeti la “The London Observer” kwamba, baada ya kushindwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) Nyerere alielekeza juhudi zake kwenye Muungano finyu zaidi, kati ya Tanganyika na Zanzibar, ima faima.
Legum alisema: “Hatua yake (Nyerere) ya kwanza ilikuwa Aprili 11, 1964 ambapo, katika kumtibua Karume aelewe kilichokuwa kikitokea, alitishia kuwaondoa Polisi 300 wa Tanganyika huko Zanzibar……Karume alisalimu amri. Alikubali kufanya mazungumzo na Nyerere ili kulinda nafasi yake. Mipango ya hawa wawili ilisukwa kwa umakini mkubwa na harakati za kuitekeleza zikaanza”.
Hapa, huenda Legum alichanganya tarehe, kwa sababu Aprili 11, ilikuwa siku ya mwisho ya mazungumzo juu ya Shirikisho mjini Nairobi, na Karume alikuwa Zanzibar. Huenda Legum alimaanisha Aprili 18, kama ilivyoonyeshwa katika taarifa ya Balozi Leonhart.
Aprili 21, Carlucci alitoa taarifa Washington akisema: “Viongozi wakongwe wamemshawishi Karume kwamba, Serikali ya Marekani na ile ya Uingereza ni marafiki wa zamani ambao wameisaidia sana Zanzibar siku za nyuma, na hivyo ameshawishika kuzipa nafasi serikali hizo zionyeshe kwamba bado ni marafiki…..”.
Aliendelea kusema, “Vyanzo vyetu vinasema, Karume ameshukuru sana kwa zawadi za majengo ya Mradi wa Zebaki (Project Mercury Buildings) na jenereta (za umeme) alizopewa na Marekani. Huu ni wakati mwafaka wa kutoa misaada zaidi kwa Serikali ya Zanzibar. Ombi la Karume la kumsomesha mtoto wake (nchini Marekani) ni ishara kwamba ana imani kubwa na Serikali ya Marekani”.
Mpaka hapo, Karume alikuwa njia panda: tishio la Nyerere la kuondoa Polisi 300 wa kulinda amani Visiwani lilikuwa kibano tosha kwake kukubali Muungano, huku Marekani nayo ikimliwaza kwa zawadi.
Je, ni kwa sababu hizi alikubali kutia sahihi Hati ya Mkataba wa Muungano hapo Aprili 22, 1964?. Ni aina gani ya Muungano uliokusudiwa?
Toa maoni yako