Wapenzi wa jinsia moja nchini Nigeria washtakiwa

KUNDI la watu 53 wamefikishwa mahakamani katika jimbo la kaskazini la Kaduna kwa kupanga kushiririki katika sherehe ya mashoga ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika katika hoteli moja nchini Nigeria, gazeti moja la Premium Times kutoka eneo hilo linaripoti.

Kundi hilo limekana kutokuwa na hatia kutokana na mashtaka ya njama, kukusanyika bila kibali na kujihusisha na jamii ambayo imepigwa marufuku wakati kesi hiyo ilipotajwa huko Chediya –Zaria kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwanasheria kwa upande wa utetezi Yunusa Umar alisema kwamba sehemu kubwa ya watuhumiwa ni wanafunzi na wamekuwa wakishikiliwa kinyume cha sheria kwa zaidi ya saa 24, gazeti hilo limeripoti.

Hakimu aliwaachia watu hao kwa dhamana hadi hapo shauri hilo litakapotajwa tena Mei 8 mwaka huu.

Vitendo vya kishoga ni kinyume cha sheria katika jamii ya kihafidhina ya Nigeria.

Mwendesha mashtaka Mannir Nasir alinukuliwa akisema kwamba watu hao 53 walikamatwa Aprili 15.

Mashoga nchini Nigeria wasakwa

Kaskazini mwa Nigeria, wanaume ambao ni wapenzi wa jinsia moja wanasakwa.

Mbele ya Tume ya Sheria ya Kiislamu yaani Sharia ya jimbo la Bauchi, wanaume wakiwa wamevalia mavazi ya rangi ya kijani wanasubiri amri kutoka kwa bosi wao.

Mtu ambaye anasimamia polisi wa kiislamu, au Hisbah kama wanavyojulikana huko, anasema kwamba msako ulianza wakati gazeti la Hausa Leadership liliporipoti mwaka jana kwamba mashoga huko Bauchi walikuwa wameunda chama. Makala hiyo pia ilijumuisha orodha ya majina ya watu.

Hisbah walijaribu kuwasaka, bila mafanikia. Hivyo wakatafuta msaada.

“Maimamu na wachungaji walipewa taarifa, ili wahubiri makanisani na katika misikiti juu ya suala hilo haramu,” alisema Jibrin Danlami Hassan, mtumishi mstaafu wa serikali ambaye sasa anasimamia Hisbah, ambayo pia inasimamia utekelezaji wa sheria ya kupiga marufuku mauzo ya pombe, umalaya na michezo ya kamari.

“Watu wanapaswa kuwaangalia watoto wao na wafahamu kwamba huwa wanajihusisha na nani,” alisema.

“Watu wanapaswa kutazama ni wapi matendo haya maovu yanafanyika, na iwapo wakifahamu tafadhali watoe taarifa kwa mamlaka.

“Tutakwenda na kuwakamata na kuwafanya waache vitendo hivyo,” alisema, na kuongeza kwamba anajivunia kufanya kazi ya Allah.

Jibrin Danlami Hassan anaongoza kampeni dhidi ya mashoga huko Bauchi

Watu wa Bauchi wanalinda tamaduni, pamoja na dini yao kwa nguvu

Dini zote, Ukristo na Uislamu, zimechukua nafasi kubwa katika kujenga mtazamo wa watu dhidi ya mashoga nchini Nigeria.

Nigeria ina jamii ya kihafidhina sana, makanisa ya kikristo yakiwa na nguvu zaidi kusini mwa nchi hiyo na uungwaji mkono mkubwa wa sheria za kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.

“Kulingana na Uislamu, kizazi kiliteketezwa na Mungu kwa sababu ya ushoga wakati wa Nabii Loti, hivyo naogopa kwamba kutakuwa na majanga hapa iwapo ushoga utaendelea,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo.

Msako mkali

Ishmael, mtu wa kwanza kukamatwa, alinaswa katika msako huo, baada ya kupata rafiki kwa njia ya mtandao wa internet. Baada ya hapo alilazimishwa kutaja majina na idadi ya marafiki wake wa karibu – na taarifa hizo kukabidhiwa kwa Hisbah.

“Wanaweza kwenda kazini kwa mtu na kusema ‘Unamfahamu Ishmael?’ na kumkamata mmoja baada ya mwingine,” anasema John, ambaye kwa sasa amejificha, akiogopa kukamatwa.

“Wanaweza kusema, ‘Kuna kitu kimempata Ishmael, tunahitaji msaada wako,’ na baadae wanamchukua.”

Kama sehemu ya msako huo, watu tisa sasa wako katika jela ya Bauchi wakisubiri kesi zao kutajwa. Maafisa katika Tume ya Sheria ya Kiislamu anasema wote walikiri makosa yao baada ya kukamatwa, japokuwa hili ni vigumu kuthibitisha na shirika la utangazaji la BBC limeelezwa kwamba baadhi ya wanaume walipigwa.

“Hatukuwakamata, ni jamii ndiyo imefanya hivyo,” alisema Hassan.

“Wakati walipoletwa hapa walikuwa salama, hawakuteswa. Tuliwahoji,” alisema, akilaumu “watu wasiotimiza wajibu wao katika ngazi ya kata” kutokana na fujo.

Wananchi wenye hasira

Wakati wa shauri la kuomba dhamana dhidi ya watu hao Januari 22 mwaka huu, umati wa watu wenye hasira ulikusanyika nje ya mahakama ya kiislamu, wakitaka hukumu kali na haraka dhidi ya watuhumiwa.

Mawe yalivurumishwa dhidi ya mahakama na shauri lilisitishwa. Polisi walilazimika kurusha risasi hewani ili kuwatawanya wananchi hao ili kuwarudisha watuhumiwa jela kwa usalama, japokuwa huko pia hawapo salama.

Hassan ni ndugu wa karibu wa mmoja wa watu wanaotuhumiwa.

“Niligundua kwamba mmoja wa watu hao alikuwa hawezi kutembea vizuri,” alisema baada ya kutembelea jela ambako nduguye ameshikiliwa.

“Kwa hiyo nilimwuliza nini kimetokea. Alinionyesha majeraha kwenye mguu wake, ambapo alipigwa. Sidhani kama ni wafanyakazi wa jela au wafungwa wenzake ndiyo waliofanya hivyo.

“Familia yetu inawasiwasi mkubwa juu ya hili. Ndugu zangu wamekuwa wananiuliza ni nini kinatokea, hasa wanawake walioolewa ambao hawajawahi kushuhudia kesi zinavyoendeshwa mahakamani, na wanategemea taarifa ninazowapa.

“Wanaendelea kuuliza ni lini ataachiwa, na naendelea kuwaambia waendelee kusali, na nawaambia mapema tu kesi itamalizika,” alisema, na kuongeza kwamba anatamani ndugu yake aachiwe kwa dhamana.

“Lakini kuna hali ya wasiwasi mjini, na watu wakimwona tu, pamoja na kwamba atakuwa ameachiwa kwa dhamana, watadhani ameachiwa huru.

“Labda mahafidhina watachukua sheria mikononi mwao. Kwa hiyo iwapo ataachiwa kwa dhamana itabidi tutafute sehemu salama kwa ajili yake,” aliongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *