MICHEZO maarufu ninayokumbuka tuliyocheza nikiwa mdogo ni mpira wa chandimu, gololi na kupinga. Chandimu chetu kilikuwa na maajabu yake kikanuni. Mtu anaweza kuwa refarii mchezaji lakini maamuzi yake tuliyaheshimu sana.
Kulikuwa pia na kanuni ya kudunda mpira timu ikinawa mpaka mara mbili, ya tatu na kuendelea ndipo adhabu ilipigwa! Tuliziheshimu sana kanuni hizo kwa sababu ndizo tulizokubaliana kuzitumia.
Zaidi ya mchezo huo wa kufungana, tulikuwa na mchezo unaoitwa "noka" ambao mnazunguka duara, mnapasiana mpira unaodundika na ukiwa nao na ukaburuzika kwako, unatoka kwenye duara. Hali inaendelea hivyo mpaka wanabaki wawili tu na mmoja kuibuka mshindi.
Tuliziheshimu sana kanuni zilizotawala mchezo huo wa kitoto. Hata ilipothibitishwa kuwa mmoja "amesakiziwa" kwa kupigiwa vibaya mpira, hatolewi. Mchezo huo ulijenga umiliki wa mpira kwa wachezaji wadogo na ndiyo maana haishangazi kupatikana wataalaam wa hilo wa wakati huo kama Nico Njohole, Hamis Gaga (marehemu), Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu) na wengine.
Aidha, tulikuwa na mchezo wa kona ambapo kanuni yake ni kufunga mpira wa kona moja kwa moja bila kupasiana mpira. Kipa akifungwa mabao matatu, anaingia kipa mwingine na mara nyingi mfungaji wa bao la tatu.
Mchezo huu ulituletea, tangu zamani sana, kina Kitwana Manara, Abdallah Luo (marehemu), Adam Sabu (marehemu), Martin Kikwa (marehemu), Jumanne Masimenti (marehemu), Richard Lumumba (marehemu) na Abeid Mziba, nikitaja wakali wachache wa vichwa wa tangu miaka ya nyuma.
Pamoja na huo, tulicheza machenga ya ovyo ambapo tulipigana chenga kwenye kikundi bila kupasiana. Anayekuwa na mpira anapiga chenga mpaka anyang'anywe. Huu ulitupatia, tangu zamani, kina Sunday Manara, Abdallah Kibaden, Yanga Bwanga, Malota Soma na wengine waliokuwa wataalam wa chenga.
Gololi ni mchezo uliokuwa maarufu sana wakati huo. Ni mchezo ambao chimbuko lake ni Uingereza ikithibitishwa na kuwepo kwa maneno mengi ya kiingereza ndani yake kama "first"(festi), wa kwanza, "last" (lasti) wa mwisho, "dead" (dedi), kuua kwa kuigonga kete ya mwingine na kuchukua gololi za dimbani, "over" (ova), kutoka nje ya mstari mnakotupa kete za kuchezea kumpata wa kwanza kulenga dimbani kwenye kete za kuliwa, "battle" (beto), mgongano "wa ajali" wa kete za kuchezea, ku-"newt" (kunyuti), kusogeza kete karibu na dimba kama mjusi wa kwenye mawe, "newt", anavyojisogeza kwenye windo na mengi mengineyo.
Kumbuka miaka hiyo ya sitini mwishoni na sabini mwanzoni, Waingereza walikuwa wameondoka si miaka mingi nyuma. Mchezo huo ulikuwa na kanuni tulizoziheshimu sana na kuzifuata.
Kuhusu mchezo wa kupinga, huu ndiyo ulikuwa mwisho wa mambo yote. Tulipinga "cha Mkononi" ambapo ukiwa na chochote mkononi, usipowahi kusema "cha mkononi poo "kwa uliyepinga naye, akiwahi kusema yeye "cha mkononiii" lazima umpe chote au mgawane kulingana na makubaliano yenu. Kulikuwa pia na "cha mfukoni".
Vile vile, kulikuwa na kupinga "ngumi nyuma" ambapo tulitembea mkono mmoja nyuma mgongoni. Ukiuacha tu bila kusema "ngumi nyuma poo" uliyepinga naye atakupiga bonge la ngumi na wewe usifanye lolote zaidi ya kuugulia maumivu! Hivyo hivyo kwa "hamsini kubong'oka" ambayo inakwenda kwa teke ukijisahau ukainama bila kusema "hamsini kubong'oka poo".
Mchezo huo wa kupinga ulikwenda kwa amani kwa kuzingatia kanuni na kila mtu alitekeleza vile alivyopaswa. Kumalizika kwake ni kupingulia. Hatua zote, kupinga kwa kunyongana vidole na kupingulia, hufanywa mbele ya shahidi anayefanya ishara ya kukata vidole hivyo.
Mchezo huo ulikuwa igizo la watoto la mkataba kwa kuwa na vitu vya kukubaliana, kufanyika kwa makubaliano mbele ya shahidi na kumalizika kwa mkataba kwa makubaliano ya pande husika.
Chandimu chetu nacho kilikuwa igizo la watoto la mchezo halisi wa soka unaoendeshwa kwa kanuni.
Nimeikumbuka michezo hiyo ya utotoni nikitafakari ukweli kwamba kila sehemu ya kazi ina mfumo wake na taratibu zake ambazo hufuatwa. Kanuni na taratibu hizo za kimfumo huwa hazibadilishwi kienyeji. Kwa hiyo michezo ya kitoto niliyoikumbuka hapa, ikiwekwa kwenye maisha halisi ya binadamu, basi ni sawa na maigizo kwa msingi kwamba watoto hawafanyi vitu halisi vya kiutu uzima kwenye michezo yao mingi.
Pamoja na michezo yao hiyo kuwa maigizo, watoto walizingatia kitu kimoja: Uhalisia wa mambo, kwa kuwa na kanuni walizozifuata kama shughuli za kiutu uzima zilivyo na kanuni. Waliigiza soka vizuri kwa kanuni zao walizoziheshimu kama soka halisi linavyoheshimu kanuni.
Waliigiza kuingia mikataba vizuri na kuiheshimu kwa kupinga na walicheza gololi kwa kufuata kanuni tu za mchezo huo na wala si vinginevyo. Wala hawakujitengenezea kanuni zao.
Ni wazi, kwa watoto kufanya hivyo, wanatoa funzo kwamba hata unapoigiza, usiache kumuaminisha anayefuatilia maigizo yako kwamba unachofanya ni kitu halisi.
Katika maigizo yetu mengi na filamu zetu nyingi, kuna matukio yanayohusu shughuli za askari polisi na shughuli za utabibu. Niliwahi kuangalia sehemu moja ya igizo fulani nikiwa na daktari. Yule daktari alilaani sana, tena kwa hasira, pale daktari wa maigizo alipoingia wodini kumhudumia mgonjwa bila kuwa na nesi (sista).
Mimi sikuelewa kama kipande hicho kilipotosha uhalisia wa shughuli za wodini kwa sababu sina uelewa wa shughuli za utabibu.
Kwa upande wa jambo moja ninalolielewa katika uhalisia wake, ninachokiona mara nyingi kwenye filamu nyingi na maigizo mengi ni upotoshaji wa neno "afande" wanapoigizwa askari na maafisa Polisi.
Wengi wa waandaaji wa maigizo hayo na filamu hizo hudhani "afande" ni jina wanalojiita askari kwa askari bila utaratibu wowote tofauti hata na mchezo wa watoto wa gololi ulivyokuwa na taratibu zake!
Kwa ufupi, afande wa jeshi lolote ni askari mwenye cheo kikubwa kuliko yule anayemuita hivyo. Yaani afande maana yake ni mkuu au kiongozi.
Kwa hiyo ni makaosa makubwa kwenye maigizo yetu mengi askari wa Maigizo wanapoitana "Afande Juma, njoo hapa" kisha Juma naye anajibu "nakuja Afande Tom". Hiyo haipo kabisa kijeshi na hata kwenye Sungusungu huikuti hiyo.
Katika mfano huu, Tom ndiye Afande wa Juma. Kwa nini? Kwa sababu ni kiongozi au mkuu tu jeshini ndiye mwenye mamlaka ya kumwita mdogo wake kwa amri. Haiwezekani hata siku moja kwa afande (kiongozi) kutumwa chochote na mdogo wake.
Hata kalamu ikimponyoka mdogo kicheo na kuanguka kwenye miguu ya afande wake, hawezi kumwambia "samahani Afande, naomba niokotee hiyo kalamu" hata kama kiumri, mwenye cheo kidogo ndiye mkubwa!
Ni aghalabu kwenye maigizo yetu kukuta askari mmoja wa maigizo akimwambia mwingine "Afande Martin, nenda ndani kaangalie kama mtuhumiwa hajajificha humo". Jeshi la wapi hili la Afande kuamrishwa?
Ni Afande tu ndiye anayetoa amri zozote, kubwa na ndogo, mara nyingi kwa kutaja vyeo vya wadogo zake kicheo, "Sajenti Andrew, mlete mtuhumiwa", "Koplo Vivian, mtazame koplo Kitogo kama kishaandaa gari", "Sajenti Sopi, hakikisha jambazi hilo mnalitia mikononi leo mkishirikiana na Konstebo Majeje na askari wengine" na kadhalika.
Lakini kwenye maigizo yetu utakuta kiongozi akisema,"Afande Sopi, shirikiana na maafande wengine kumnasa mhalifu huyo", jambo lisilo sahihi kabisa.
Katika mifano niliyoitoa hivi sasa, wote hao, Sajenti Andrew, Koplo Vivian na Sajenti Sopi wataitikia "sawa Afande" kwa sababu atakayewaamrisha atakuwa na cheo cha zaidi ya Sajenti na Koplo kama nitakavyovipanga vyeo hivyo.
Kwa mfuatano, vyeo vya polisi vinapanda ifuatavyo kutoka chini: Konstebo (constable) hana alama yoyote, Koplo (corporal) ana alama ya "V" mbili, Sajenti (sergent), "V" tatu na Staff Sergent, "V" tatu na ua.
Baada ya hapo kuna Mkaguzi Msaidizi (Assistant Inspector), nyota moja na Mkaguzi (Inspector), nyota mbili. Anayefuatia ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (Assistant Superintendent of Police), nyota tatu, Mrakibu wa Polisi (Superintendent of Police), mwenge na kuanzia cheo hicho "unga" wa kwenye kofia unaanza.
Baadaye anafuata Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (Senior Superintendent of Police), Mwenge na nyota moja. Juu yake ni Kamishna Msaidizi wa Polisi(Assistant Commissioner of Police), Nembo ya Taifa, Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (Senior Assistant Commissioner of Police), Naibu Kamishna wa Polisi (Deputy Commissioner of Police), Kamisha wa Polisi (Commissioner of Police) na juu zaidi ni Inspekta Jenerali wa Polisi(Inspector General of Police).
Miongoni mwa askari na maofisa hao, wanaostahili kupigiwa saluti ni maafisa wa kuanzia nyota moja, yaani wakaguzi wasaidizi kwenda juu. Wanaostahili saluti hupigiwa na kila waliowazidi cheo, tangu cheo cha chini kabisa.
Kwa mpangilio huo wa vyeo, kila aliye juu ni afande wa aliye chini yake au wa walio chini yake kicheo. Baada ya maelezo haya, sitatarajii kama ndani ya maigizo yetu na filamu zetu, afande ataitwa bila mpangilio.
Naamini wa kwanza kulitekeleza hilo watakuwa Kaole Sanaa Group kwa sababu Katibu wao, Simon Simalenga "Dimera" ni mfuatiliaji, msomaji na mchangia maoni mzuri wa safu hii.
Naomba nimalize kwa kushauri mambo matatu: Kwanza, tunapoigiza masuala ya kipolisi tujitahidi kujua nyadhifa za kipolisi zinazohusika sana na tunayoyaigiza. Ukiyaangalia maigizo yetu mengi, kuna askari wa vyeo vya chini, kuna mkuu wa kituo, OCS ambaye mara nyingi huwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya, OC CID ambaye havai sare na cheo chake mara nyingi ni kama cha OCS.
Mwingine ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya, OCD ambaye mara nyingi ni Mrakibu wa Polisi au Mrakibu Mwandamizi wa Polisi. Kwa uchache anaweza kuigizwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, RCO ambaye mara nyingi ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi asiyevaa sare pia.
Yakienda juu sana, maigizo yetu yatafika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, RPC ambaye huwa mwenye cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi au Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi. Ili tusogelee kwenye ukweli, si vibaya tukiwa tunataja nyadhifa hizo.
Kwa mfano tunaigiza OCD akiita kwenye simu,"OC CID njoo mara moja na OCS". Wakifika, mmoja mwenye nyota tatu na sare zake na mwingine bila sare, anasema,"tumefika afande", huku mwenye sare(OCS) akipiga saluti na mwenzake asiye na sare (OC CID) akibana mikono.
Pili, nawaomba mnapoigiza shughuli za taasisi yoyote ile, wasilianeni na watu wa taasisi hiyo kujifunza wanavyoendesha mambo yao ili msiigize vituko.
Kwa mfano, askari wa kiume haruhusiwi, kikanunu, kumkamata na kumpekua mtuhumiwa wa kike isipokuwa katika mazingira yatakayohalalisha hali hiyo. Kwenye maigizo yetu, hilo halizingatiwi.
Vile vile, mtu hapaswi kisheria kuwekwa mahabusu polisi kwa zaidi ya saa 24 bila ya sababu za msingi kama Jura alivyofanyiwa kwenye tamthilia ya Jumba la Dhahabu ya Fukuto Arts Promotions.
Katika tamthilia hiyo hiyo, kuna kosa jingine la kisheria. Kisheria, hakuna uwajibikaji wa kijinai kwa mtu endapo mwingine anajaribu kujiua kwa sababu ya kuchukizwa naye.
Katika igizo hilo, aliyepaswa kuchukuliwa hatua za kisheria alikuwa Winter kwa kosa la kujaribu kujiua na wala siyo Jura aliyesababisha Winter atake kujiua. Ilipotakiwa Jura awe ndani, ingeonyeshwa kwamba Jura, kwa nguvu za Jini Kabula, angekutwa akijaribu kumuua mchumba wake,Winter.
Hapo, kuwa ndani kwake kwa tuhuma ya Kujaribu kuua kusingekuwa na utata. Ukosefu wa kuwasiliana na wazoefu wa shughuli husika ulijidhihirisha pia katika igizo moja la miaka ya nyuma kidogo la Kaole Sanaa Group.
Katika igizo hilo nililolisahau jina, mshtakiwa wa mauaji, Kemmy, aliyemuua mume kijana wa mama yake kwa hasira ya kubakwa kwa binti yake Rayu na mume huyo wa baba yake, alisomewa shitaka hilo kwa kifungu cha sheria cha namba nyingi za ajabu ajabu wakati palipaswa pasomwe kifungu sahihi cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code) cha kosa la mauaji.
Vile vile, kwa sababu kosa hilo lilikuwa la kusikilizwa na Mahakama Kuu, basi Jaji angekuwa mtu wa umri mkubwa kidogo badala ya Jaji Metu aliyekuwa wa umri wa mika 20 na kitu tu, jambo ambalo haliwezekani kiuhalisia.
La tatu, nawaomba tena watengeneza filamu wa Tanzania muwe mnaomba kibali kwa majeshi yetu cha kutumia sare zao halisi angalau kwenye filamu tu na si kwenye maigizo ya kawaida.
Hii itaongeza uhalisia wa filamu zetu ambazo tunahitaji ziwe za kimataifa. Nadhani hilo linatekelezeka kama ilivyo huko India, Nigeria, Ulaya na Marekani.
Nadhani wasanii wetu sasa mmemjua Afande ni nani. Kwa msisitizo, naomba kurudia kusema Afande ni kiongozi tu, ni Mkuu. Mnaposema "Afande Juma njoo haraka" maana yake "Mkuu Juma njoo haraka" jambo lisilo na mantiki kabisa kijeshi na hata kwenye maisha mengine.
Mwenye cheo cha juu Jeshini ndiye anayewaita kwa amri na anayewaamrisha nini cha kufanya aliowazidi cheo. Huyo ndiye Afande.
Wiki ijayo: Kwa nini hatujali kuhusu ufashaha wa Kiswahili kama tunavyojali ufasaha wa Kiingereza?
Toa maoni yako