Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
UKO salama faraja ya moyo wangu? Maana nina wasiwasi sana usije ukaugua kwa wakati huu. Maana kuugua kwa wanene na kwa wakondefu tofauti sana.
Juzi Bosi alijisikia vibaya, kajipeleka hospitali gani ya binafsi sijui, bila shaka kwa kutumia posho yake mpya ya waheshimiwa wa makalio. Nafikiria kumwomba Mama Bosi anipatie kiti jikoni niwe ninakaa wakati napika au kukosha vyombo na mimi nipate posho ya kitako huku nafanya kazi niliyoajiriwa. Itakuwa raha sana.
Hata hivyo, Bosi alirejea kutoka hospitalini akiwa amefura ajabu, hadi alilazimika kurudi hospitali tena apewe vidonge vya shinikizo la damu. Kwa hali hii atamaliza posho yake ya makalio haraka sana.
Kwa maelezo yake yaliyojaa matusi ya kila aina, wakati wa kurudi kutoka hospitali, aliitwa kwenda kuchangia na yeye kwenye suala la hawa wanaotakiwa kulinda afya yetu. Yeye si waziri wa mikiki na makeke. Na mgomo wowote ni wa makeke kwelikweli.
Sasa alipokwenda akakuta hakuna wakuongea nao, maana wenzetu wameona mgomo maana yake ni kugomea hata kuongea na mtu. Hivyo, Bosi aliamua kuuza sera kwa wananchi pale nje ya hospitali.
Lakini ajabu ni kwanza alipotaka kuzungumza watu wote walimpa kisogo. Na kila alipojaribu kusema wakamzomea hadi ilibidi mafanyafujo waingilie kati kwa misingi yao ya kwamba ukimpiga mtu kichwani atabadilika. Wananchi kuona hivyo wakasambaratika huku wakiimba:
MSITUPASHE NA MIPOSHO YENU
Na wengine walinyanyua bango:
HATUKO TAYARI KUWASIKILIZA WATU WANAOZIDI KUJIONGEZEA ULAJI WAKATI SISI TUNA NJAA.
Hapo sasa! Bosi alikasirika hadi mishipa ya damu ilikuwa inadunda kama ngoma ya wagobogobo nakuambia.
Ndiyo maana wakati anamwelezea MB akajisikia vibaya tena na kukimbizwa kwa hospitali ya wanene ambako madaktari wanalipwa tofauti kabisa kwa kazi zao. Na aliporudi ilibidi apumzike kabisa. Hata wiski haikuruhusiwa.
Kesho yake alisikia nafuu lakini aliamua kubaki nyumbani ndiyo maana baadhi ya wageni wake waliambiwa waje nyumbani badala ya kwenda ofisini. Tena waliambiwa wasimshitue Bosi maana shinikizo lolote lingepandisha shinikizo lake la damu. Lakini mmoja kidogo atibue kila kitu na kumlazimisha Bosi atibiwe tena.
Alianza vizuri kwa kusema kwamba anaona makeke yamezidi nchini hivyo ameanzisha shirika lake la TIMA yaani TIBU MAKEKE. Bosi alicheka.
‘Yaani nyie watu. Kila kitu kinaundiwa AZAKI yake. Na umepata fedhuli gani wa kuwafadhili.’
Mgeni naye akacheka.
‘Hatuhitaji mfadhili mheshimiwa. Mtatulipa nyinyi. Unajua usuluhishi wa migogoro ni taaluma pia. Na bila taaluma hii mtazidi kupata matatizo.’
‘Una maana gani?’
‘Unisamehe mheshimiwa maana sitaki kutibua tiba. Uko tayari kusikiliza bila kukasirika?’
Bosi kwanza alikunja uso lakini baadaye alijitahidi kucheka pia.
‘Usiniambie unaanza kutumia mbinu hizo kwangu! Eti samahani! Samahani ni neno la wanyonge tu.’
‘Ahaa, hapo umeleta suala muhimu sana. Kwanza utafiti unaonyesha kwamba wenye uwezo wa kuomba msamaha badala ya kuendeleza ubabe ni wale wanaojiamini kabisa.
Wanajua kwamba kuomba radhi baada ya kufanya kosa hakuwapunguzii kitu chochote bali kunawaongezea heshima na hekima. Wasiojiamini ndio wanaozidi kutumia ubabe katika kujaribu kuficha kosa.’
‘Unataka kusema kwamba serikali haijiamini? Tunajiamini sana. Tunajua kwamba tuko sahihi asubuhi, mchana, jioni hadi usiku ndiyo maana hatuna budi kuwashughulikia wasiotambua usahihi huo.’
Mgeni alicheka tena.
‘Sawa mheshimiwa. Lakini tamko kama hilo linadhihirisha nilichosema. Hakuna aliye sahihi kila wakati. Na ukiangalia duniani, wanaofanikiwa kuongoza bila mikiki wala makeke ni wale wanaosikiliza vema upande wa pili badala ya kuudharau, kuukejeli na kuutusi.’
‘Huu muda utapata wapi?’
‘Bila kutumia muda kidogo mwanzoni, itabidi utumie muda mwingi zaidi mara elfu baadaye. Hebu angalia mgomo wa sasa.’
‘Kwani wao wamefuata ushauri wako? Mbona wakati sisi tumekuwa tayari kuwasikiliza na wao wanasusa?’
‘Nawaendea baadaye pia. Lakini kwa nini wamefikia hali hiyo? Hivyohivyo ninavyokuambia. Kwanza wakajibiwa na dharau na kejeli na vitisho. Sasa kama mtu amekasirika tayari, kumdharau na kumtisha ni njia bora kabisa ya kumfanya akasirike zaidi na matokeo yake ni madhara makubwa zaidi. Na kutoamini lugha laini inayotumika baadaye. Wanaona kama ni unafiki kwa sababu bado ni majeruhi wa dharau na vitisho vya awali.’
‘Usianze kuwatetea hawa mahayawani! Wapu ….’
‘Ngoja, ngoja mheshimiwa. Unaona umeshaanza kutukana tena. Hasira hasara hasa katika kutafuta muafaka wa suala gumu kama hilo.’
Bosi alishusha pumzi kwa nguvu ya ajabu. Akakaa kimya kwa muda. Lakini mgeni aliendelea.
‘Ndiyo maana nasema bora mtumie watu kama sisi ambao tumebobea katika kumaliza migogoro. Tunasikiliza pande zote mbili bila hasira wala hasara na kuwezesha pande zote mbili zinazoonyeshana ubabe hatimaye watafute suluhu bila kuwaumiza watu wengine tena.’
Bosi bado hakusema neno, sijui kama maneno yalimwingia au alikuwa anaomba tu mgeni aondoke, maana ukishazoea upumbavu wa mabavu huna mbavu za kuachana na ubovu huo. Kumbe mgeni alikuwa hajamaliza.
‘Halafu mheshimiwa mkitaka kuwashawishi watu kwamba wewe uko sahihi na wenye makosa ni wale wa upande wa pili, lazima uonyeshe mfano. Kwa mfano, kutangaza miposho mipya ya kwenu huku unawatisha na kuwakejeli wanaodai posho ndogo zaidi ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto. Hakuna atakayewaelewa.’
Hatimaye Bosi alisema.
‘Wewe bwana umekuja kunichokoza makusudi au …. Unanitukana ndani ya nyumba yangu.’
‘Hapana mheshimiwa sikutukani hata kidogo. Nimesikia watu walivyokususa pale hadi umeumwa. Mimi nisingependa uumwe tena, ndiyo maana inabidi uwaelewe wale.
Nakumbuka zamani suala hili liliibuka na baada ya mvutano wa muda mrefu, Baba wa Taifa aliwaambia waheshimiwa kwamba wawe na uchaguzi mkuu mpya, waheshimiwa wakijieleza na kujitetea kwa nini wanapaswa kuongezewa posho na Baba wa Taifa akieleza kwa nini anapinga. Kwani walisema tena?
Walijua kabisa kwamba watakuwa wamejichomea utambi kwa njia hiyo, wakalalamika kichinichini na kumwita Mwalimu dikteta, lakini ukweli ni kwamba wananchi wasingeelewa. Na leo hii hawaelewi pia na hawataelewa. Kisha mnajidai kutaka kumaliza mgogoro wa wengine wanaotaka posho huku mnang’ang’ania posho zenu. Kweli mheshimiwa mwenye akili ataelewa hapo?’
Bosi alisimama.
‘Toka katika nyumba yangu. Wewe unajidai mtalaamu wa kumaliza migogoro huku unazidishia migogoro ndani ya kichwa changu? Nakuambia usiingilie visivyokuhusu ama sivyo …’
Mgeni naye alikuwa amesimama pia na kuanza kuelekea mlangoni
‘Unaona! Vitisho tena. Nakutakia afya njema lakini nakuambia wazi, kwa mbinu hizi za mbavu na vitisho, hautapata afya njema na nchi yetu haitapata afya njema pia.’
Bosi akapaza sauti.
‘Toka nimekuambia. Hatuwezi kuvumilia ujinga wa watu na daima tutasimama imara …’
Lo, mpenzi ilikuwa senema kabisa maana wakati Bosi anasema watasimama imara akaanguka puuuu! Kumbe presha kibao tena ikabidi akimbizwe hospitali tena na hata kulazwa.
Lakini ingawa naona haikuwa wakati muafaka kumwambia Bosi hivi, mgeni kasema ukweli. Na ukweli ukiuma na unazidi kuupiga si utazidi kuongeza maumivu.
Mkubwa akifuata njia fulani si wengine watafuata? Mipasho ya posho itaishia wapi? Oh susasusa na zomeazomea itazidi kupamba moto hadi wanaokaa angani wanasikiliza hali ya sisi tulio duniani.
Akupendaye bila posho yoyote,
Hidaya wako
Toa maoni yako