Wastaafu wala mabilioni sawa na wizara

SHERIA ya mafao ya viongozi wa umma ya mwaka 1999, iliyosainiwa na rais wa wakati huo Benjamin Mkapa na kufanyiwa marekebisho Juni, mwaka 2005, inaendelea kuleta neema  kwa wastaafu.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinabainisha ya kwamba kwa mwaka ujao wa fedha, vigogo wastaafu wa kitaifa ambao ni tisa na wajane wanne, wametengewa Sh bilioni 12.2.

Kwa kuzingatia idadi hiyo na kiwango cha fedha walichotengewa, ukipiga hesabu kwa kila kichwa, kila mmoja ataweza kuvuna takriban shilingi milioni 900 kwa mwaka.

Viongozi wastaafu kwa sasa ni Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa ambao walikuwa marais katika awamu ya pili na tatu. Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya, Salim  Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Wajane wanaoguswa na sheria hiyo ni wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, wa Mzee Rashidi Kawawa, wa Eward Sokoine na Dk. Omar Ali Juma.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo mwandishi wetu ameziona, Bunge tayari limepitisha kiwango hicho cha fedha ambacho kinatarajiwa kuwa ni zaidi ya bajeti ya Wizara ya Afrika Mashariki, inayoongozwa na Spika wa zamani, Samuel Sitta na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inayoongozwa na Sophia Simba.

Wizara hizo hata hivyo bado hazijawasilisha bajeti zao bungeni na bajeti hizo zinatarajiwa kuwasilishwa Mei 10, mwaka huu kwa upande wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na kwa upande wa Wizara ya Afrika Mashariki, bajeti yake inatarajiwa kuwasilishwa Mei 24, mwaka huu.

Taarifa ambazo hazijawa rasmi zinaeleza ya kwamba Wizara ya Afrika Mashariki imetengewa bajeti isiyozidi bilioni 10, wakati ile ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto inatajwa kuweza kutengenewa bajeti isiyozidi Sh bilioni 13.

Sheria iliyosainiwa na Mkapa

Kwa sasa ni kama vile Mkapa anakula matunda ya saini yake iliyodhinisha marekebisho ya Sheria ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1999, yaliyopitishwa mwaka 2005.

Katika sheria hiyo kiwango cha mafao kwa kiongozi husika hukokotolewa kwa kutumia kanuni za kiwango cha asilimia itakayopangwa na mamlaka husika.

Kwa upande wa marais wastaafu, mbali na kupata mafao yao ya kazi, wanapaswa kulipwa posho ya kila mwezi kiasi cha asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani. Kwa lugha nyingine, kiasi hicho cha asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani ni sawa na kusema anapata Sh 80 kwa kila Sh 100 ya mshahara anaopewa rais aliyeko madarakani.

Huduma nyingine anazopewa rais mstaafu ni pamoja na ulinzi, msaidizi, katibu muhtasi, mhudumu wa ofisi, mpishi, dobi, mtumishi wa ndani, mtunza bustani, madereva wawili na gharama za mazishi atakapofariki.

Anapewa pia pasi ya kusafiria ya hadhi ya kidiplomasia, yeye pamoja na mke au mume wake, sambamba na kugharimiwa matibabu iwe ndani au nje ya nchi.

Anapewa huduma ya kutengenezewa magari mawili yenye uzito usiopungua tani tatu, ambayo hutolewa na serikali na hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Rais mstaafu pia hujengewa nyumba mpya, yenye vigezo maaalumu ambavyo ni kuwa vyumba angalau vinne, viwili kati ya hivyo ni lazima viwe na huduma zote ndani (self-contained).

Vigezo zaidi kwa upande wa nyumba hiyo vinatajwa kuwa ni iwe na ofisi iliyokamilika, makazi maalumu ya mfanyakazi wake.

Makamu wa rais na mawaziri wakuu

Tofauti ni ndogo tu kati ya stahili za rais mstaafu na makamu wa rais mstaafu, na tofauti yao ni kwamba wakati rais mstaafu anajengewa nyumba, kwa upande wake, makamu wa rais hajengewi nyumba pia hupewa gari moja.

Wajane na wagane

Sheria hiyo pia inatambua kuwalipa mafao wajane au wagane wa viongozi wakuu wa kitaifa kama rais, makamu wake na waziri mkuu.

Rais mstaafu akifariki dunia, mke au mume wake hupewa nyumba, posho kiasi cha asilimia 40 ya mshahara wa rais aliye madarakani.

Aidha, mjane au mgane huyo hutengewa fedha za matibabu ndani ya nchi na matengenezo ya gari analopewa na serikali.

Hulipiwa pia  mshahara wa kima cha chini kwa dereva na mtumishi wa ndani pamoja na hupewa usafiri wa kwenda mahali atakapoishi maisha yake yaliyosalia.

One thought on “Wastaafu wala mabilioni sawa na wizara”

  1. Nkwazi Mhango says:

    Ukisikia ujambazi na ukoloni wa wakoloni weusi ni huu. Kwanini wafanyakazi wengine wa umma wastaafu na kuachwa wajimalizikie wakati hawa viongozi wapendelewe? Inashangaza kuona mtu kama Lowassa naye anaitwa mstaafu wakati alitimliwa tokana na ufisadi? Tunaipeleka wapi nchi ambapo tuna watu wasioona mbali zaidi ya matumbo na pua zao? Kwa lipi walilofanya hadi wamalize pesa ya umma wa watu maskini hivi? Hii maana yake ni kwamba demokrasia tunayoimba ni zana ya kuuibia umma na kunufaisha genge la watu wachache. Huu nao ni ufisadi wa kimfumo na ukoloni mambo leo unaopaswa kupigwa vita kwenye katiba mpya kama itaandikwa na kuwa mpya badala ya kuwa sanaa za CCM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *