Watafiti: Maliasili zikinufaisha jamii zitaepusha migogoro

MIGOGORO itokanayo ya rasilimali za taifa itaepukika iwapo zitanufaisha jamii zilimo rasilimali hizo.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Mazingira kwa Maendeleo (Environmental for Development) umebainisha kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya wananchi na rasilimali zilizopo katika maeneo yao, hivyo kuwaengua katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizo huzaa migogoro. 

Hata hivyo imebainika kuwepo kwa wasi wasi miongoni mwa mamlaka za serikali nchini kuzishirikisha jamii katika kuhifadhi na kuendeleza rasilimali zilizopo katika maeneo yao, hofu ambayo watafiti hao wanashauri inapaswa kuondoka.

Dr Edwin Muchapondwa kutoka EFD Afrika Kusini anaishauri serikali ya Tanzania kuepukana na mashaka kuihusisha jamii katika usimamizi na hifadhi ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao kwa msingi kwamba hatua hiyo huathiri utungaji wa taratibu na sheria zisizofaa.

Mtafiti huyo anasema kuwa badala ya Tanzania kuwa na mashaka, inabidi kubadilika kwa kutoa  haki ya matuzi, kusimamia na kugawa rasilimali hizo kwa jamii zilipo, na kwamba inahitaji kuhimiza matumizi ya soko badala ya mfumo wa sasa wa utozaji ada na leseni katika hifadhi ya maliasili.

Taarifa za tafiti hizo zilitolewa hivi karibuni mjini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Sera (Policy Day) ya taasisi ya EFD Tanzania ambapo watafiti mbali mbali kutoka nchi wanachama za Kenya, Ethiopia, Afrika Kusini, Coaster Rica na China, walihudhuria.

Pamoja na watafiti hao mkutano huo pia uliwashirikisha wawakilishi kutoka shirika wafadhili wa tafiti hizo la SIDA, kutoka taasisi za serikali kama vile MNRT, NEMC, COSTECH Marine Zanzibar na wawaklishi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali.

Miongoni mwa tafiti zilizowasilishwa ni pamoja na Katika uboreshaji usimamizi wa rasilimali za wanyama wa porini kwa ajili ya kupunguza umasikini (Improving wildlife management for poverty reduction). Mtafiti Dr. Francisco Alpizar, anabainisha kwamba hatua ya kuziachia jamii masikini sehemu ya mapato yatokanayo na wanyama wa porini pamoja na misitu, sio kwamba inazihamasisha tu jamii hizo kuhifadhi maliasili hizo bali inapanua zaidi shughuli za kiuchumi ikiwemo ukuaji wa ajira.

Utafiti huo uliobainisha umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika hifadhi na uendelezaji wa maliasili na ulifanyika katika nchi sita za Kusini mwa Afrika na matokeo yake yamelezwa kuwa na uhusiano mkubwa na mazingira ya Tanzania.

Mkurugenzi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dr. Julius Ningu anakubaliana na matokeo ya tafiti hizo kuhusu maliasili akisema hatua ya kuzitenga jamii ni chanzo cha migogoro inayohusu rasilimali za taifa nchini na kwamba njia pekee ya kuepukana na migogoro hiyo ni kwa kutekeleza ushauri unaotolewa na watafiti hao juu ya kuzishirikisha jamii hizo katika utunzaji na uendelezaji wa rasilimali za taifa.

“Focus ya watafiti hawa ni matumizi ya rasilimali zilizopo zinufaishe taifa na wahusika, kwa maana ya jamii zilipo rasilimali hizo, unapo-exploit na kuwaacha unatengeza migogoro,” anasema Dr Ningu katika mahojiano yake na Raia Mwema mjini Arusha hivi karibuni.

Naye Mkurugenizi wa Mipango na Utafiti kutoka Baraza la Hifadhi ya Mazingira nchini, Ruzika Muheto anakubaliana na watafiti hao akisema rasilimali ni fursa hivyo kama haziwanufaishi wananchi basi kuna tatizo mahali.

Anabainisha umuhimu wa kuwepo hatua za makusudi katika kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na maliasili katika hifadhi ya rasilimali nchini hivyo kuachana na utamaduni wa kuzisafirisha malighafi zitokanazo na maliasili nje ya nchi jinsi yalivyo.

MKUHUMI,

Miongoni mwa rasilimali zilizohusika katika tafiti hizo ni pamoja na misitu ambapo watafiti hao wanaonyesha mashaka yao kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa ukaa kutokana na ukataji Miti hovyo na Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI+), marufu kama REDD+.

Watafiti hao kutoka taasisi hiyo ya Mazingira kwa Maendeleo Tanzania wanabainisha kuwa iwapo watunga sera wataelewa jinsi ya usambazaji wa malipo ya MKUHUMI + katika kutoa motisha zinazohitajika katika kuleta mabadiliko ya jinsi watu wanavyotumia misitu, basi mkakati huo una uwezekano wa kuwa na mafanikio zaidi kuliko juhudi za awali za kuhifadhi misitu.

MKUHUMI ina manufaa makubwa ya  kifedha kwa Tanzania iwapo itatekelezwa ipasavyo. Kwa mujibu wa rasimu ya mkakati wa kitaifa kwa mfumo huu wa biashara ya hewa ya ukaa kwenye misitu ambayo inahusu hasa kupunguza uzalishaji wake kutokana na ukataji wa misitu, taifa litaweza kuingiza dola za Kimarekani milioni 630 kwa mwaka.

Hata hivyo mtafiti mwingine kutoka taasisi hiyo, Prof. Elizabeth Robinson anatoa angalizo kuhusu matumaini yaliyopo katika mkakati huo kwa nchi za Kiafrika akisema sio jambo rahisi kama inavyonekana kwa wengi kutokana na ugumu katika kufuatilia uharibifu wa misitu unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya shughuli kama vile mbao, kuni na uchomaji mkaa.

Prof. Robinson anasema uharibifu huo wa misitu kwa kuchagua miti ya kukata kwa ajili ya shughuli mbali mbali ni tatizo kubwa nchini lakini wakati huo huo ufuatiliaji wake pia ni mgumu, na kwa msingi huo misitu mingi itapoteza hadhi yake hivyo kutonufaika na mapato yatokanayo na mkakati wa MKUHUMI.

Kwa mujibu wa wataalamu wa misitu, uharibifu wa aina hiyo ni mbaya zaidi kutokana na kuchambua miti ambapo mwisho wake ni msitu kukosa sifa baada ya miti mingi kukatwa na kuachwa michache iliyosamba hapa na pale.

Taarifa za tafiti hizo zimekuja huku kukiwa na migogoro mingi itokanayo na wananchi kutonufaika kutokana na rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao, lakini wakati huo huo wakiona zikiwanufaisha wageni zaidi.

Katika salamu zake kwenye mkutano huo, Dr Ningu alibainisha jambo la msingi wakati wa kupanga matumizi ya rasilimali zilizopo kwamba mipango hiyo ilenge zaidi jinsi Watanzania watakavyonufaika na rasilimali hizo kama ilivyo kwa nchi zingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *