Wataka Magufuli, Majaliwa wasaidie walipwe Manyara

WAKAZI 16 wa Mtaa wa Negamsi katika Halmashauri  ya Mji wa Babati Mkoani Manyara wamemililia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwabana watendaji wa serikali Mkoani Manyara ili walipwe fedha za fidia baada ya ardhi yao kutwaliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya mahakama ya Mkoa wa Manyara.

Ardhi hiyo ambayo ina ukubwa wa zaidi ya ekari nane ilitwaliwa na serikali mwaka 2005  kwa ajili ya kupisha ujenzi wa majengo ya mahakama ya Mkoa wa Manyara.

Tayari sehemu kubwa ya majengo hayo ya Mahakama ya Mkoa wa Manyara yamekamilika  na muda wowote shughuli  za mahakama zitahamia katika majengo hayo.

Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi hao pamoja na nyaraka ambazo Raia Mwema imezipata, tangu mwaka 2005 ardhi hiyo ilipotwaliwa na serikali wananchi hao hawakuwahi kulipwa fedha zao za fidia kwa mujibu wa sheria za ardhi.

Katika ardhi hiyo  kulikuwa na nyumba za kuishi, mazao ya biashara na chakula, na  miti  katika madirio na tathmini ya awali walipaswa kulipwa zaidi ya shilingi milioni 300 mwaka huo wa 2005.

Taarifa  ambazo hata hivyo hazikuthibitishwa  zinadai kuwa  wakati wa utawala awamu ya nne kuna sehemu ya fedha hizo zilitolewa na serikali lakini huenda “zilitafunwa” na wajanja kwa njia za kifisadi.

Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kuhusu sheria ya ardhi ya Vijiji na mitaa, inafafanua kuwa kabla ya ardhi kutwaliwa  kwa matumizi ya serikali au binafsi  fidia inapatakiwa kulipwa ndani ya kipindi cha miezi sita.

Kifungu cha 4.5  cha sheria hiyo kipengele (a)  inafafanua kuwa  riba ya  usafiri, upangaji na kupoteza faida kuu au mamlaka ya Serikali ya Mtaa pale tu ambapo malipo ya fidia hayakulipwa kwa wakati na kipengele  (b) kinafafanua  kuwa  ukadiriaji wa riba kwenye fidia inayotakiwa “kulipwa kwa wakati” maana yake ni kulipa fidia katika kipindi cha miezi sita baada ya ardhi inayohusika kutwaliwa au hakimiliki kubatilishwa.

Sheria  hiyo kwa mujibu wa tovuti ya Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC)  inaendelea  kufafanua  kuwa  “Endapo kiwango cha fidia hakilipwi miezi sita baada ya ardhi kutwaliwa au hatimiliki kubatilishwa riba italipwa kwa wastani wa asilimia ya riba anayolipwa na Benki za kibiashara kwenye akiba  za muda maalum hadi fidia itakapolipwa”.

Akizungumza na Raia Mwema,  Mwenyekiti  wa wakazi 16  wanaodai fidia  katika mtaa huo wa Negamsii, Iddi Makange, alieleza kuwa mwaka 2005 ardhi yao ilitwaliwa na serikali kupisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Mkoa wa Manyara.

“Tulifanyiwa tathmani kabla ya maeneo yetu kutwaliwa, lakini cha kushangaza wakati huo hatukupewa tena mrejesho  wa kiasi ambacho kila moja wetu angepaswa kulipwa kama fidia ya eneo lake,” alisema Mzee Makange.

Aliongeza:” Tangu mwaka 2005 hakuna kilichoendelea hadi mwaka 2013 ambapo tathmini ya pili ilifanyika na mwaka 2016 na tathmini ya tatu  ikafanyika lakini hatulipwa fedha zetu za fidia.”

“Sasa ni miaka 12 tangu ardhi yetu imetwaliwa na hakuna fedha za fidia tulizolipwa  zaidi ya watendaji wa serikali  wa Mkoa wa Manyara kutupiga danadana. Sisi tunamwomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye anafahamu malalamiko  yetu  na Rais Dk.Magufuli ambaye kwa mujibu wa sheria ya ardhi ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuingilia  suala hili asikie kilio chetu na atusadie tupate haki yetu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Katibu wa kikundi cha wakazi hao, Anthony Umbe, aliongeza kuwa, kwa wakazi ambao bado maeneo yao hajaathrika na ujenzi unaoendelea wameshindwa kufanya chochote kwa kuwa hawajui hatma yao.

“Kuna wazee ambao ardhi yao imetwaliwa na bado wako ndani ya nyumba zao hadi sasa, kuna nyumba zimechakaa sana zinahitaji ukarabati lakini hawawezi kuzifanyia ukarabati kutokana na sheria kuwa ardhi ikishafanyiwa tathmini hurusiwi tena kuindeleza,” alisema Katibu huyo.

Aliongeza: "Katika kipindi chote tumelalamika sana katika ngazi mbalimbali za serikali  katika Mkoa wa Manyara kwa maandishi lakini hadi leo hakuna ngazi iliyoshughulikia  malalamiko yetu ndiyo sababu tunamlilia Mheshimiwa Rais ambaye tuna imani naye aingilie kati atusaidie.”

Kwa mujibu wa moja ya barua kwenda kwa Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Manyara ya Machi  21  mwaka huu, wananchi hao wameelezea kwa masikitiko makubwa  kwa taasisi hiyo kushindwa kulipa fidia zao.

Barua hiyo inaeleza:” Kwa masikito makubwa pamoja na kufuatilia mara kwa mara fidia yetu kwenye ofisi yako baada ya ardhi yetu kutwaliwa tangu mwaka 2005 hadi sasa mwaka 2017 bado hatujapata fidia, kulikoni? ”

Inaendelea barua hiyo: "Zimeshafanyika tathmini awamu tatu, 2005,2013,2016, lakini hakuna utekelezaji, rejea kikao cha Aprili 2016  mbele ya Katibu Tawala Mkoa wa Manyara na Mkurugenzi wa Mji wa Babati, ulitamka kuwa fedha za fidia zipo ila tathmini haijakufikia.”

Barua hiyo inaendelea kueleza kuwa Mei 6 mwaka 2016 tahmini ya mwisho ilifanyika na iliwasilishwa kwa Mtendaji huyo wa mahakama lakini cha kushangaza hakuna malipo ya fidia yaliyofanyika  ikiwa tayari ni zaidi ya mwaka moja.

Katika barua yao wakazi hao wanadai kuwa kuna uwezekano kama fedha za fidia zilikuwepo zilirudishwa hazina au  kuna jambo nyuma ya pazia kuwa fedha hizo “zimeliwa na wajanja” na wao kuendelea kulaghawiwa na watendaji wa serikali.

“Kwa barua hii tunakuomba utupatie mrejesho kwani baada ya tahmini kuna nyumba ambazo ziko hatarini kuanguka na vinginevyo tunashindwa kufanya maendeleo yetu,” inamalizia barua hiyo.

Nyaraka zinaonyesha kuwa katika kipindi chote cha madai hayo ya fidia viongozi wote wa serikali Mkoa wa Manyara kama Mkuu wa Mkoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa  zamani na wa sasa wamekuwa wakinakiliwa barua zote za malalamiko  hivyo kufahamu madai ya wananchi hao.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Manyara,  Jacob Swale,  alisema asingweza kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu na kumtaka Mwandishi kufika ofisini kwake siku ya Jumatatu.

“Siwezi kuzungumzia suala kwenye simu njoo ofisini Jumatatu na pia leo ni Jumapili muda huu niko Kanisani,” alisema Mtendaji huyo na kukata simu yake.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera hakuweza kupatikana mwishoni mwa wiki  lakini  kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara (RAS), Eliakim Maswi alisema suala hilo halimhusu kwa kiutendaji linaangukia chini ya Mamlaka ya Mahakama na Halmashauri ya Mji.

“Mimi sihusiki na suala hilo halinihusu, hayo mambo ya watu wa Halmashauri ya Mji na Mahakama, wasiliana nao,” alisema kwa kifupi Maswi ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Wizara Nishati na Madini.

Katika ziara yake ya kikazi iliyofanyika Machi Mkoani Manyara, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliulizwa swali na diwani mmoja katika mkutano wa hadhara kuhusu fidia ya wananchi hao ambapo naye alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera kujibu.

Katika majibu yake, Bendera alieleza kuwa anafahamu malalamiko ya wananchi hao kutolipwa stahiki zao baada ardhi yao kutwaliwa na kuongeza juhudi zilikuwa zinafanyika fedha zao za fidia zipatikane.

“Kama muda wote wa miaka 12 hamjaweza kuwalipa mtafanya miujiza gani kuwalipa katika kipindi hiki kifupi kabla mwaka fedha haujafungwa? alihoji Majaliwa na kusisitiza kuwa wananchi hao walipwe fedha zao za fidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *