Watanzania waelimishwe kuhusu hisa

KATIKA Robo ya Kwanza ya mwaka ujao, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) linatarajiwa kushuhudia ongezeko kubwa la thamani baada ya makampuni ya simu ya Tanzania kuanza kuuza hisa zake.

Kampuni ya Vodacom, kwa mfano, ambayo inaonekana itakuwa ya kwanza kuanza zoezi hilo miongoni mwa makampuni yaliyopo hapa nchini, inatarajiwa kuuza hisa zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 500.

Kwenye historia ya DSE, hiki kitakuwa kiwango kikubwa zaidi cha hisa kuuzwa na kampuni yoyote tangu kuanzishwa kwa soko hilo zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Hii ni habari nzuri kwa uchumi wa nchi yetu. Baada ya muda mrefu wa kulalamika kuhusu makampuni yenye faida kubwa kumilikiwa na wageni, sasa Watanzania watapata fursa ya kuyamiliki japo kwa sehemu.

Hata hivyo, hatudhani kama Watanzania kwa ujumla wao wanajua ukubwa na umuhimu wa hatua hii. Mpaka sasa, jambo hili halijaibua mijadala mikubwa popote pale.

Watanzania wengi hawana uelewa mpana wa masuala ya masoko ya hisa. Jambo hili la makampuni ya simu kuuza hisa zao linapaswa kutumika vema kuibua uelewa na ufuatiliaji wa mambo haya.

Kuna Watanzania wengi wenye uwezo wa kuwekeza kwenye eneo hili lakini hawatafanya hivyo kwa sababu hawajajua soko la hisa ni kitu gani na wanaweza kupata faida gani kujiunga nalo.

Hawa ni watu ambao wanaamini katika ufugaji wa kuku, ujenzi wa nyumba nyingi za kupangisha, kilimo na biashara za aina mbalimbali.

Kuna waajiriwa wengi ambao wamewahi kujiingiza kwenye ufugaji au kilimo na kwa vile hawana muda wa kusimamia shughuli hizo, wameishia kudhulumiwa na kukata tamaa.

Soko la Hisa ni biashara wanayoweza kuifanya na kuisimamia wakati wakiwa wanaendelea na ajira zao. Hawataweza kuibiwa wala kudhulumiwa kwa sababu wanaweza kupata taarifa za hisa zao kila wakati wanapotaka. Tena taarifa zenyewe ni sahihi.

Kama fursa hii ya kuelimisha wananchi isipotumiwa vema, taifa linaweza kujikuta limepoteza fursa kubwa ya wananchi wake kumiliki makampuni haya yenye faida kwa maendeleo yetu.

Muda ungalipo, ni wajibu wa serikali na makampuni haya kutumia muda uliopo na rasilimali walizonazo kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu masuala haya ya umiliki wa hisa za makampuni kupitia DSE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *