Watengeneza mvinyo wafurahia bajeti

WATENGENEZAJI wa mvinjo na bidhaa zake wamesema sasa wameanza kuona kwa vitendo, dhamira ya serikali ya Tanzania kuwa na uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2020 kutokana na yaliyomo kwenye bajeti iliyowasilishwa wiki iliyopita.

Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2017/18 imefanya uamuzi wa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mitaji na kupunguza ushuru wa bidhaa za mvinyo uliotengenezwa kwa zaidi ya asilimia 75 na malighafi inayozalishwa ndani ya nchi.

Wafanyabiashara hao wanaamini kuwa uamuzi huo wa Serikali ni kichocheo kikubwa kwa wakulima wa zao la zabibu kuongeza uzalishaji tofauti na hivi sasa ambapo uzalishaji wao umekuwa hautoshelezi mahitaji ya viwanda vilivyopo.

Pia, uamuzi huo umetoa fursa kwa wawekezaji wa ndani wenye viwanda vya mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu kuhamasisha wakulima kutumia vyema  nafasi hii kuongeza uzalishaji ili kujiongezea kipato.

Mkurugenzi wa kampuni ya mvinyo ya Alko Vintages, Alchard Kato, ameliambia Raia Mwema kuwa hatua hiyo ya serikali imeangalia umuhimu wa zao la zabibu katika uchumi nchi ambao kwa sasa hauonekani kama ni mkubwa lakini ni sekta inayokua.

“Ili sekta inayokua hususan ya viwanda iweze kuendelea kukua na matokeo ya ukuaji wake yaonekane kwenye jamii, serikali haina budi kupunguza ushuru/ kodi hata kwa kiwango kidogo kama ilivyofanya tofauti na kuongeza kodi kila wakati bajeti kuu ya nchi inaposomwa.

“Bajeti zilizopita serikali ilikuwa na desturi ya kupandisha kodi kwenye vinywaji vikali ikiwemo mvinyo unaotengezwa ndani ya nchi,”alisema.

Aliongeza “Malighafi ya zabibu ni asilimia kati ya 25 na 30 tu ya gharama za uzalishaji wa mvinyo hivyo kupungua kwa ushuru kunaweza kutoleta mabadiliko makubwa sana kama inavyotarajiwa na wananchi.”

Katika bajeti ya mwaka 2017/18, serikali imeshusha ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa kutumia zabibu inayozalishwa ndani ya nchi (kwa kiwango kinachozidi asilimia 75) kutoka shilingi 202 kwa lita na kuwa shilingi 200 kwa lita.

Katika bajeti kuu ya serikali ya 2016/17, ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 uliongezeka kutoka shilingi 192 kwa lita hadi shilingi 202 kwa lita.

Wakati ushuru kwa mvinyo wa ndani ukishuka, ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 umeongezeka kutoka shilingi 2,236 kwa lita hadi shilingi 2,349 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita.

Wakulima wa zabibu wanena

Sehemu kubwa ya wakulima wa zabibu wanategemea soko kwenye viwanda vichache ya kusindika mvinyo vilivyopo nchini hususan mkoani Dodoma ambavyo ni Alko Vintages, Central Tanzania Wine Company (CETAWICO) na Dodoma Wine Company (DOWICO).

Kutokana na uhitaji mkubwa wa zao la zabibu utakaojitokeza na unaoendelea kujitokeza, wakulima wameanza kujipanga kuongeza mitaji yao kwa kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha zenye riba nafuu.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Ushirika wa Wakulima wa Zabibu na Masoko Mpunguzi (UWAZAMAM), Emmanuel Temba, mbali na kununua zabibu kutoka kwa wakulima wanachama na wasio wanachama kwa ajili ya kuchakata mchuzi wa zabibu na kuuza kwenye viwanda vinavyosindika mvinyo, wamejipanga kuwa na shamba la ekari 100 la ushirika ili kuondokana na adha ya ushindani wa bei msimu  wa kununua zabibu.

Ununuzi wa shamba hilo, utawawezesha kwa kiasi fulani kukidhi mahitaji ya lita milioni tatu za mchuzi wa zabibu (dulky wine) kwa mwaka unaohitajika kwa kuwa wanunuzi wao wakuu wa kiwanda Tanzania Distilleries Limited (TDL) kinachozalisha kinywaji cha Konyagi na vinginevyo.

Hivyo, hatua ya Serikali kushusha ushuru wa mvinyo na kuondoa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mitaji imewapa uhakika wa kuzalisha zaidi kwa kuwa kutaamsha soko la mvinyo na mahitaji zaidi ya malighafi (zabibu). Hivyo kwa sasa wamejipanga kutafuta eneo hilo la ekari 100 kwa ajili ya kilimo cha zao la zabibu.

Katika mwaka 2015/16, Ushirika wa UWAZAMAM  ulizalisha lita 48,000 na  msimu wa kwanza wa mwaka 2016/17 tayari wamezalisha 30,000 ambazo zote zimeuzwa kwenye kiwanda cha kutengeneza pombe kali cha TDL.

Iwapo ushirika huo utafanikiwa kupata mkopo wa shilingi milioni 75 kutoka katika taasisi za fedha, utakuwa na uwezo wa kununua zabibu ghafi tani 150.

Tani moja ya zabibu hutoa kati ya lita 750 na 800 ya mchuzi wa zabibu (dulky wine)  hivyo tani 150 zitakuwa na uwezo wa kutoa lita 112,000, lita moja huuzwa kwa shilingi 1800.

Mbali na kiwanda cha TDL, pia kiwanda cha Mega Trade kinachotengeneza kinywaji cha K. Vant mkoani Arusha kimeonyesha nia ya kuhitaji mchuzi huo kwa ajili ya kutengeneza mvinyo.

Kwa upande wake, mkulima wa zabibu wa kijiji cha Mpunguzi, Patrick Simbwi ambaye naye huuza zabibu zake kwenye viwanda vya kusindika mvinyo vya mjini Dodoma, anaona kuwa hatua ya serikali kupunguza na kuondoa kodi ni fursa kwa mkulima mmoja mmoja kuongeza uzalishaji kwa kuwa viwanda vitahitaji malighafi zaidi.

Hata hivyo, mkulima huyo alisema fursa iliyotolewa na serikali inafungua changamoto nyingine ya kutotegemea mvua kwenye kilimo cha zabibu na badala yake waanze kujipanga kwenye kilimo cha umwagiliaji kupitia miradi ya uchimbaji wa visima.

VAT kwenye bidhaa za mitaji

Hatua ya serikali kusamehe VAT kwenye bidhaa za mitaji (capital goods) itapunguza gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Alko Vintages, mashine za uzalishaji kwa wale wanaoanzisha viwanda ina matokeo makubwa ukilinganisha na ushuru  uliopunguzwa kwenye bidhaa za mvinyo kutokana na kwamba hata wazalishaji wa sasa wataendelea kupanuka kwa kuagiza mashine nyingine.

Kwa ujumla kwa mtu yeyote anayetaka kuanzisha kiwanda kidogo, cha kati ama kikubwa suala la  kuingiza vifaa kwa kulipia kodi ya VAT ilikuwa kikwazo.

Alisema wakati mwingine, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kilikuwa kikilazimika kutoa kivutio kwa kupunguza VAT kutoka 18 hadi 10 lakini bado ilikuwa kubwa, hivyo uamuzi wa serikali utavutia zaidi uwekezaji wa viwanda na ni wa kupongezwa.

Hata hivyo, vivutio kwa wawekezaji hutofautiana kati ya wawekezaji wa ndani na nje mfano uwekezaji katika sekta ya kilimo  si kivutio kwa wawekezaji wa nje wakati asilimia 70 ya Watanzania wanahusika na ufugaji na kilimo.

“Viwanda vingi vilivyowekezwa na wageni havihusiani na mkulima, hivyo tunapozungumza kukua kwa uchumi tunazungumzia mapato ya kodi na ajira za mijini lakini maisha ya wakulima hayabadiliki kwa sababu sehemu kubwa ya uwekezaji haumgusi mkulima moja kwa moja,” alisema.

“Kama serikali inataka ukuaji wa uchumi uguse hadi watu wa chini hususan wakulima haina budi kuweka vivutio kwa wawekezaji wadogo na kati wa ndani ya nchi ili wawekeze kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo ambapo faida itakayopatikana itatumika kuendelea kuwekeza ndani ya nchi.

“Tumeona kwenye zabibu, jinsi soko la zabibu lilivyo ambapo walikuwa wakinunua zabibu kwa shilingi 700 kwa kilo lakini mwaka jana bei imeongezeka na kufikia shilingi. 1200 kutokana na uzalishaji kuwa mdogo ukilinganishwa na soko”.

Kuhusu mvinyo toka nje ya nchi, alisema serikali imeongeza ushuru pasipo kutofautisha aina ya mvinyo uliokamilika na usiokamilika. Wote kodi yao ni moja na imeongezeka kwa shilingi 113 kutoka shilingi 2,236 mpaka 2,349 kwa lita.

Kwa maana nyingine, serikali inahamasisha kuingiza mvinyo uliokamilika kutoka nje wakati ule ambao haujakamilika(Mchuzi) ungependelewa ili ukamilishwe na viwanda vya ndani na kuleta mapato kwa njia nyingi ikiwemo kuongeza ajira na kodi katika vifungashio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *