Makala
Watu hawawezi kuishi kisiwa cha kujitegemea bila kuhemea ujamaa
Deusdedit Jovin
Toleo la 007
12 Dec 2007

UFUATAO ni ufafanuzi wa kutetea tamko kwamba “Ujamaa na Kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru” kama tunavyosoma katika ibara ya nne, kifungu cha tatu, kwenye Katiba ya CCM (1977).

Sababu ya kwanza inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: kila binadamu anayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea binafsi kama ambavyo anayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika familia. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza hatua ya kwanza kabisa kwenye mvuvumko wa dola.

Hatua ya kwanza katika mvuvumko wa dola ni kuzaliwa kwa familia. Katika hatua hii watu binafsi wenye jinsia tofauti, mmoja akiwa na jinsia-ngeli-jike na mwingine akiwa na jinsia-ngeli-dume walilazimika kujiunga pamoja na kukamilishana kama mke na mume na hatimaye kupata watoto na hivyo kuunda familia.

Kila familia ilikuwa na majukumu angalau matano. Kwanza, kila familia ilishiriki katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuweza kutosheleza mahitaji yake ya msingi. Pili, kila familia ilikuwa ni kitovu cha elimu ya kuwandaa watoto kwa ajili ya kushika majukumu yao ya kiutu uzima. Tatu, kila familia ilikuwa ni kituo cha afya kwani ilikuwa na jukumu la kuhakikisha afya na tiba ya wanafamilia.

Nne, kila familia ilikuwa na jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa wanafamilia wote, wazazi wakiwalinda watoto na watoto wakiwalinda wazazi katika uzee wao. Tano, kila familia ilikuwa ni kanisa la nyumbani kama ambavyo ingeshuhudiwa na sala za pamoja kwa mfano kabla ya mlo.

Na kubwa zaidi, kila familia ilikuwa na bado ni kitovu cha kuzalisha uhai mpya ili kujaza nafasi za wale wanaokufa, ama kwa uzee au kutokana na majanga ya duniani, na hivyo kuhakikisha kwamba mfereji wa uhai unaendelea kutiririka kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Katika kila familia, baba au mama alihusika katika uongozi, kila familia ikiwa na kipande chake cha ardhi ambako watu wake walilima, kujenga nyumba na kufuga. Madaraka ya wazazi katika kuratibu maslahi ya pamoja katika ngazi ya familia yaliishia kwenye mipaka ya ardhi ya familia.

Kwa ufupi, katika maelezo haya tunajifunza kwamba, hapo mwanzo, watu binafsi wenye jinsia tofauti walilazimika kuungana na kuunda ndoa na hatimaye familia kwa sababu hakuna binadamu anayeweza kuishi kama kisiwa milele.

Yaani, pamoja na kwamba kila mtu katika upekee wake aliweza kuzalisha mahitaji yote muhimu kwake lakini bado hakuweza kujitosheleza kwa kila kitu.

Kwa mfano asingeweza kujipa mimba, akazaa watoto akamnyonyesha na kumkuza vizuri. Kusudi kujiwezesha kwa njia ya umoja, ujamaa wa namna fulani katika ngazi ya familia ndilo lilionekana kuwa ni jibu mwafaka.

Na hii ndiyo kusema kwamba watu walikubaliana kwa makusudi kuunda familia ili waweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kijamaa chini ya uongozi wa pamoja, yaani uongozi wa baba na mama. Hivyo ndivyo familia zote zilivyozaliwa. Na hatua ya kwanza katika mvuvumko wa dola inaishia hapa.

Sababu ya pili inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: Kila familia inayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea kijamaa kama ambavyo inayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika ukoo. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza hatua ya pili kwenye mvuvumko wa dola.

Hatua ya pili katika mvuvumko wa dola ni kuzaliwa kwa koo. Kadiri ukubwa wa familia ulivyoongezeka mahitaji ya ardhi zaidi, watu zaidi na uongozi bora zaidi yalijitokeza, na hivyo familia kuungana hadi ukoo kuzaliwa. Ardhi kubwa zaidi ilihitajika kwa ajili ya mashamba ya kuzalisha chakula zaidi, mavazi zaidi na malazi zaidi. Watu zaidi walihitajika kwa ajili ya kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi zaidi.

Na uongozi bora zaidi ulihitajika ili kutatua migogoro inayohusisha watu wa familia zaidi ya moja na pia kuonyesha njia ambako gurudumu hili lingesukumwa kupitia. Hivyo, watoto waliofikia umri wa kujitegemea wakalazimika kuoa na kuolewa na kuanzisha familia zao, lakini katika ujirani mmoja.

Baada ya vizazi kadhaa mchakato huu ukazalisha kundi la watu wanaofanana kwa mila na desturi kutokana na historia moja yenye kuwahusisha na babu mmoja. Kundi la aina hii liliitwa ukoo.

Historia inaonyesha kwamba, katika kila ukoo palitokeza mgawanyo wa majukumu, kila familia na kila mtu binafsi akifanya kazi tofauti tofauti zilizozalisha mahitaji tofauti kwa jamii nzima.

Kwa njia hii biashara ya kubadilishana ikazaliwa miongoni mwa familia mbalimbali za kikoo; wazee wa ukoo wakabeba majukumu ya kusuluhisha migorogoro kati ya familia na familia, na vijana wakawa na jukumu la ulinzi wa ukoo.

Hata hivyo, madaraka ya wazee katika kuongoza na kuratibu maslahi ya pamoja katika ukoo yaliishia katika mipaka ya ardhi ya ukoo.Kwa ufupi, katika hatua hii tunajifunza kwamba, hapo mwanzo, familia kadhaa zililazimika kuungana chini ya uongozi wa wazee wa ukoo kwa sababu hakuna familia inayoweza kuishi kama kisiwa milele. Yaani, pamoja na kwamba kila familia katika upekee wake iliweza kuzalisha mahitaji yote muhimu kwake lakini bado haikuweza kujitosheleza kwa kila kitu.

Na hii ndiyo kusema kwamba familia zilikubaliana kwa makusudi kuunda koo ili ziweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kijamaa chini ya uongozi wa pamoja, yaani wazee wa ukoo. Hivyo ndivyo koo zote zilivyozaliwa. Na hatua ya pili katika mvuvumko wa dola inaishia hapa.

Sababu ya tatu inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: kila ukoo unayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea kijamaa kama ambavyo unayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika kijiji. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza hatua ya tatu kwenye mvuvumko wa dola.

Hatua ya tatu katika mvuvumko wa dola ni kuzaliwa kwa vijiji. Kadiri ukubwa wa ukoo ulivyoongezeka mahitaji ya ardhi zaidi, watu zaidi na uongozi bora zaidi yalijitokeza, na hivyo koo kuungana hadi kijiji kuzaliwa. Kwa ufupi, katika hatua hii tunajifunza kwamba, hapo mwanzo, koo kadhaa zililazimika kuungana chini ya uongozi wa wazee wa kijiji kwa sababu hakuna ukoo unaoweza kuishi kama kisiwa milele. Yaani, pamoja na kwamba kila ukoo katika upekee wake uliweza kuzalisha mahitaji yote muhimu kwake lakini bado haikuweza kujitosheleza kwa kila kitu.

Na hii ndiyo kusema kwamba koo zilikubaliana kwa makusudi kuunda vijiji ili ziweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kijamaa chini ya uongozi wa pamoja, yaani wazee wa kijiji. Hivyo ndivyo koo zote zilivyozaliwa. Na hatua ya pili katika mvuvumko wa dola inaishia hapa.

Sababu ya nne inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: kila kijiji kinayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea kijamaa kama ambavyo kinayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika kabila. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza hatua ya nne kwenye mvuvumko wa dola.

Hatua ya nne katika mvuvumko wa dola ni kuzaliwa kwa makabila.Kadiri ukubwa wa kijiji ulivyoongezeka mahitaji ya ardhi zaidi, watu zaidi na uongozi bora zaidi yalijitokeza, na hivyo vijiji kuungana hadi kabila kuzaliwa. Kwa ufupi, katika hatua hii tunajifunza kwamba, hapo mwanzo, vijiji kadhaa vililazimika kuungana chini ya uongozi wa chifu mmoja wa kikabila kwa sababu hakuna kijiji kinachoweza kuishi kama kisiwa milele. Yaani, pamoja na kwamba kila kijiji katika upekee wake kiliweza kuzalisha mahitaji yote muhimu kwake lakini bado hakikuweza kujitosheleza kwa kila kitu.

Na hii ndiyo kusema kwamba vijiji vilikubaliana kwa makusudi kuunda kabila ili viweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kijamaa chini ya uongozi wa pamoja, yaani chifu wa kabila na baraza lake la wazee. Hivyo ndivyo makabila yote yalivyozaliwa. Na hatua ya nne katika mvuvumko wa dola inaishia hapa.

Sababu ya tano inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: kila kabila linayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea kijamaa kama ambavyo linayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika dola. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza hatua ya tano kwenye mvuvumko wa dola.

Hatua ya tano katika mvuvumko wa dola ni kuzaliwa kwa dola yenyewe kama tunavuofahamu leo. Dola ni muungano wa familia, koo na makabila. Hawa wote wakiwa chini ya uongozi mmoja unaoratibu mfumo rasmi wa sheria, mfumo rasmi wa ulinzi na mfumo rasmi wa biashara na fedha. Uongozi wa dola huitwa serikali.

Kwa kifupi, familia, koo, makabila, na asasi za kiraia, waliungana na kuunda dola kwa sababu zile zile zilizolazimisha watu binafsi kuungana na kuunda familia, familia kuungana na kuunda koo, koo kuungana na kuunda vijiji, vijiji kuungana na kuunda makabila. Na waliungana na kuunda dola kwa sababu zile zile zilizolazimisha wadau mbalimbali kuungana na kuunda asasi za kiraia.

Na hii ndiyo kusema kwamba kila familia, kila ukoo, kila kijiji, kila kabila, kila wilaya, kila mkoa, na kila asasi ya kiraia vilikubaliana kwa makusudi kuungana hatua kwa hatua na hatimaye kuunda dola ili viweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kijamaa chini ya uongozi wa pamoja, yaani serikali ya dola. Sababu ya sita na ya mwisho inayonisukuma kuifagilia siasa ya ujamaa na kujitegemea ni kwamba: Kila asasi ya kiraia inayo haki ya kuishi katika kisiwa cha kujitegemea kijamaa kama ambavyo inayo haki ya kukamilishwa kijamaa na majirani zake wa karibu katika dola. Hili linajidhihirisha wazi kama tukichunguza kuzaliwa kwa asasi za kiraia (civil societies) katika dola.

Kadiri ukubwa wa dola unavyoongezeka mahitaji fulani fulani yasiyoweza kutimizwa na dola hujitokeza. Kwa sababu hii wadau mbalimbali huungana kwa hiari, wakajitengenezea asasi za kiraia ili hatimaye waelekeze nguvu zao katika eneo hili chini ya uongozi wa asasi hizo.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Deusdedit Jovin
deus.jovin@gmail.com
+255-0758341483, +255-0684175182

Toa maoni yako