Watu ni ‘waoooga’ sana ndiyo maana wanasitasita utadhani chura mbele ya chui

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,

Uzitoni Street,

Bongo.

 

Mpenzi wangu,

VIPI hali yako huko?  Biashara inasemaje?  Mwendokasi wa biashara yako unaendana na mwendokasi wa sembe na sukari?  Nakumbuka wakati ule tulipoambiwa tule majani!  Tuombe mwezi mtukufu usigeuzwe na wengine kuwa mwezi kufuru kwa jinsi ambavyo watazidi kupandisha bei.

Lakini tuache hayo.  Kumbe Binti Bosi ni mpenzi sana wa fasihi, hasa fasihi ikimwimarisha katika maoni yake.   Juzi wakati wa kula akawa anamwelezea bosi kitabu kimojawapo, nadhani kiliitwa Adui wa Umma.

'Ni kitabu kizuri sana baba.  Tena najua kimeshatafsiriwa kwa hiyo nadhani inabidi kisomwe na watu wote.'

Bosi akacheka.

'Ohoo, kama ni kitabu unachokipenda wewe, nadhani kinapaswa kupigwa marufuku kabisa.'

BB akanuna.

'Siyo hivyo baba.  Ni kuhusu daktari bingwa ambaye kwanza anagundua maji ya mto karibu na mji wake yana madini mazuri sana kwa afya ya binadamu.  Basi alipigania watengeneze eneo maalum la kuogea haya maji ili watalii waje kwa wingi katika kutafuta afya bora zaidi huku wakineemesha mifuko ya wananchi.'

'Safi sana.  Hii ni kama nchi ya viwanda tunavyoongelea kila siku.'

BB hakusema kitu kwa muda, kisha akaendelea.

'Lakini haikuwa hivyo.  Meya wa mji ambaye ni kaka yake yule daktari alikataa kwa muda mrefu eti anaogopa kupoteza pesa.'

Bosi akaingilia tena.

'Yaleyale ya hapa.  Watu ni waooooooga sana ndiyo maana baada ya kukaa na kufanya maamuzi wanasitasita utadhani chura mbele ya chui ha ha ha.'

BB akacheka kidogo. 

'Lakini hayo yote yalitokea kabla ya mchezo kuanza.  Sasa eneo hili maalum limejengwa na watalii wa kwanza wanakuja.  Hapo Daktari akagundua kwamba wengine wanaugua baada ya kuogea, akafanya utafiti na kukuta kwamba maji yana uchafu kibao.'

'Daktari gani huyu?'

'Tatizo halikuwa daktari baba.  Tatizo Meya.  Daktari alimwambia Meya, kaka yake, kwamba wakijenga chini ya viwanda ambavyo vinatupa takataka kwenye maji, yale maji yatakuwa si salama tena.  Lakini Meya, kwa kutaka kusevu pesa, akaamua kufanya vilevile na kusababisha uchafuzi wa maji safi.'

Hapo bosi alikuwa ameanza kukunja uso.

'Kumbe hadithi hii yote lengo lake ni kuanza kutupakazia tena.'

'Hapana baba.  Kwani mnafanya mambo haya?  Sikujua.'

Bosi alivyomtupia mwanaye jicho kidogo ashindwe kudaka, lakini BB aliendelea.

'Sasa baada ya kugundua kwamba maji yale yanasababisha magonjwa, ungefanya nini?'

Bosi akatafakari.

'Mmm swali gumu.  Anapaswa kufunga kweli hadi eneo lisafishwe na labda mabomba yachukue maji kutoka juu zaidi.  Lakini wakati huohuo, itakuwa ni pigo kubwa sana kwa uchumi wa mji.  Watu wataathirika.'

'Na inaweza kuathiri nafasi yako katika uchaguzi ujao.'

'Sawasawa mwanangu.  Kumbe unajua.   Chama tawala kisiache hata mwanya wa wengine kuvuruga.  Sisi ni watawala kwa sababu ni watu wenye mawazo mazuri.'

'Na kujenga mabomba chini ya kiwanda ndiyo mawazo mazuri.'

'Kosa moja tu.'

'Babaaa.  Basi kweli kaka mtu alikataa.   Dokta, baada ya kuona mawazo yake ya kitaalam yanapuuzwa aliamua kutumia vyombo vya habari na alipozuiwa, akaamua kufanya mkutano wa hadhara ili kuwaelimisha wananchi juu ya hatari zilizopo.'

'Bila kibali?'

'Kibali ya nini baba wakati watu wanakunywa maji yenye uchafu?'

'Tatizo lako ni kwamba hujui siasa.  Hutangazi ovyoovyo hivihivi.'

'Na ndivyo alivyosema Meya.  Mpaka watu wote wakamwona Daktari adui wa umma na kumtupia mawe.'

Wacha bosi acheke.

'Unaona sasa.  Watu wanaangalia maslahi yao kwanza, na sisi tunapenda kuongoza kwa kuwafuata nyuma na maslahi yao.'

BB akakaa kimya kwa muda.

'Sawa baba, lakini hata kama utamchinja yule daktari, uchafu si bado upo?  Wananchi wote wakidanganywa ili wakane utaalam kwa sababu wataalam hawajui kuchezea siasa hivi, hawataugua.  Kwa hiyo, mwisho wa siku, wote watajua kwamba mtaalam kasema ukweli huku wengine wakiwa wameumwa au hata kufa kutokana na yale maji.'

'Kumbe ndiyo mambo mnayoyasema shuleni.  Utaalam ni muhimu lakini utaalam usiingilie siasa hata kidogo.'

Hapo BB akabaki mdomo wazi hadi nzi akaingia mdomoni.  Ilibidi atoke na kutafute kumtoa.  Sasa sijui kwa nini BB akaleta stori hii au ina mahusiano gani na mambo yetu.  Lakini kweli mipango mibovu ni mimba, haiwezi kufichwa na mkono, au maneno.  Itazidi kukua na kuleta athari hadi wote wataona.  Au vipi?  Bila shaka bosi na wenzie hawawezi kufanya kama yule Meya.  Duh!

Akupendaye kwa mpango thabiti kabisa

Hidaya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *