Watumishi hewa wazua vilio benki

HATUA ya serikali kuwatimua wafanyakazi hewa imeleta mtikisiko katika taasisi za fedha nchini ambako inadaiwa watumishi hao walikopa zaidi ya shilingi bilioni 20, Raia Mwema limedokezwa.

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Dk. Yahaya Msigwa alisema mpaka sasa mbali ya athari kujitokeza kwa kupoteza wanachama kwenye vyama vinavyounda shirikisho hilo, changamoto nyingine ni taasisi za benki kupata hasara kutokana na mikopo waliyopewa kushindikana kurejeshwa.

Anasema Msigwa: “Vyeti feki ni burning issue kwa nchi nzima, tangu asubuhi nazungumza takribani na mikoa 15 kuhusu hilo suala la wafanyakazi kwani athari iliyojitokeza ni kubwa mno. Mpaka sasa kuna waliofariki na wengine kushindwa kupeleka watoto shuleni. Wameshindwa kurejesha mikopo mbalimbali waliyokopa kwenye benki nchini, tatizo ni kubwa mno. Kwa takwimu za haraka haraka kuna deni linakadiriwa kufikia kati ya shilingi bilioni 20 hadi 30.”

Dk. Msigwa aliahidi kufafanua zaidi suala hilo baada ya kukamilisha majukumu yake nje ya nchi ambako wakati akizungumza na Raia Mwema alikuwa akielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya safari yake hiyo : “Niko safarini nitakuja tuzungumzie suala hili kwa kina zaidi lakini ni jambo kubwa, kubwa sana,”alisema

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Henry Mkunda, alisema chama cha TUGHE kimeathirika kwa namna mbili: “ Kuathirika kwa wanachama wenyewe kwa kuondolewa kazini. Na namna ya pili ni kuathirika kutokana na mambo yenyewe yanavyoshughulikiwa. Tunashindwa kupata majibu yao kwa wakati kutoka kwenye mamlaka za serikali.”

Hata hivyo, Mkunda amesema TUGHE haina taarifa za moja kwa moja kutambua ni wanachama wao wangapi wameathiriwa na zoezi hilo la kuwaondoa kazini wafanyakazi waliodaiwa kuwa na vyeti feki kutokana na majadiliano yanayoendelea kufanyika hivi sasa: “Hatuwezi kuwa na data kutokana na kwamba mchakato kuwa endelevu kwa sababu, kuna watumishi ambao tunajenga hoja wanarudishwa kazini na wengine bado majadiliano yanaendelea.

“Hatuwezi kuwa na taarifa kamili na sahihi kwa sasa ila ndio hivyo tumeendelea na vikao na serikali na kujenga hoja mbalimbali ambazo nyingi zinaweza kuzaa matunda,” alisema.

Kwa upande wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA), Katibu Mkuu, Jonathan Musoma, amesema kwamba hali kwa chama hicho ni shwari kutokana na kukosekana kwa watumishi hewa, kikubwa ambacho chama hicho kimeathirika ni kutokana chama hicho kuwa miongoni mwa vyama vinavyounda TUCTA.

“Hali kwetu ni shwari. DOWUTA ina wanachama kwenye taasisi tatu (Mamlaka ya Bandari za Tanzania-TPA), Marine Service Ltd (Mwanza) na TICS (Tanzania International Container Terminal). Bahati nzuri katika taasisi hizi hakuna watumishi hewa. Athari iliyopo kwa ujumla ni kwamba sisi tunashirikiana na TUCTA, kwa hiyo ikiathirika TUCTA, tunaathirika vyama vyote,”alisema Musoma.

Pamoja na TUCTA kuibua changamoto ya hasara iliyopo kwenye taasisi za benki, mmoja wa maofisa wa mikopo  kwenye moja ya benki kubwa nchini ameliambia Raia Mwema kwamba benki zina miiko yake, hivyo asingeweza kuzungumza chochote kuhusu suala hilo.

Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki nchini, Dk. Charles Kimei, kutoa maoni yake kuhusu suala hilo hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni juzi Jumatatu.

Hali ilivyo

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Raia Mwema kwa muda sasa kwa wastani, takribani walimu 200 wamepoteza kazi katika kila mkoa wa Tanzania Bara tangu kuanza kwa zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wa serikali.

Takwimu za watumishi wa serikali zinaonyesha kwamba walimu ndiyo kundi kubwa zaidi la watumishi na kwa taarifa ambazo gazeti hili limepewa na vyanzo vyake, huenda takribani walimu 6000 wamekumbwa na fagiafagia hiyo ya watumishi hewa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Angela Kairuki, aliwahi kutoa taarifa rasmi iliyoeleza kwamba hadi sasa, takribani watumishi wa serikali 20,000 wamekutwa na matatizo katika vyeti vyao walivyoviwasilisha serikalini wakati walipokuwa wakiomba ajira.

Kwa kawaida, taasisi nyingi za kifedha nchini, zikiwamo benki, zimekuwa zikipendelea kukopesha watumishi wa serikali ambao ajira zao zinaonekana kuwa salama kwa vile mara nyingi ajira zake huwa ni za kudumu tofauti na wale wa sekta binafsi ambao ajira zao ni za mkataba.

Maelezo ya Msigwa yanabebwa na ukweli kwamba taarifa za mwaka huu za kibenki zinaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la mikopo isiyolipika kwa wakati, maarufu kwa jina la mikopo chefuchefu, ambayo imeziweka baadhi ya benki katika hali mbaya.

Katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema;  “Takwimu pia zinaonyesha kuwa ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chefuchefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia tano”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *