Wawekezaji wa ndani waanza kurejea soko la hisa

BAADA ya kuadimika kwa muda, hasa kipindi cha mwisho wa mwaka jana na wiki ya kwanza ya mwaka huu, wawekezaji wa ndani wameanza kurejea kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

Hali hii inaonyesha kwamba, pamoja na kuwa na majukumu ya kifedha ya mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka, wawekezaji bado wanashiriki kwenye biashara.

Pamoja na hali hiyo, uchambuzi wa soko umeonyesha kwamba bado idadi ya hisa zinazopelekwa kuuzwa sokoni haiendani na idadi ya maombi ya kununua hisa hizo.

Ripoti za soko kwa wiki iliyopita zilionyesha kwamba idadi ya wawekezaji wa ndani ilionekana kuongezeka kwenye pande zote za kununua na kuuza, japokuwa idadi bado ni ndogo ikilinganishwa na wawekezaji wa ndani.

DSE imesema kwenye ripoti zake za wiki jana kwamba, idadi kubwa ya wawekezaji wa ndani ilionekana siku ya Jumatatu, ambapo asilimia 100 ya hisa zote zilizokuwa sokoni kwa ajili ya mauzo zilikuwa za wawekezaji wazawa.

Katika ripoti ya siku hiyo, wawekezaji wa ndani walishiriki ununuzi wa hisa kwa asilimia 33.08 kutoka wastani wa asilimia 0.76 za wiki mbili za awali. Mauzo ya hisa kwa siku hiyo yalikuwa ni shilingi milioni 107.

Siku ya Jumanne, ripoti zinaonyesha kwamba kiasi cha shilingi milioni 575.51 zilipatikana kutokana na biashara ya hisa na ushiriki wa wawekezaji kutoka nje ya nchi ulikuwa ni shilingi milioni 719.59.

Kwa siku hiyo, asilimia 5.01 ya kiasi hicho cha fedha za manunuzi ilichangiwa na uwekezaji wa ndani ya nchi huku wawekezaji kutoka nje ya nchi wakichangia asilimia 94.99 ya mauzo yote.

Kwa upande wa uuuzaji wa hisa, asilimia 18.71 ilitokana na wawekezaji kutoka ndani ya  nchi, huku wawekezaji kutoka nje ya nchi wakichangia asilimia 81.29 ya uuzaji wa hisa zao.

Ripoti ya siku ya Jumatano ilionyesha kwamba jumla ya fedha zilizopatikana kutokana na biashara ya hisa ilikuwa ni shilingi milioni 450.65, ambapo wawekezaji kutoka nje ya nchi walichangia mauzo hayo kwa shilingi milioni 432.24.

Katika siku hiyo, ushiriki wa wawekezaji wa ndani ya nchi kwa upande wa ununuzi ilikuwa ni asilimia 4 huku upande wa uuzaji asilimia 21.12 ilichangiwa na wawekezaji kutoka ndani ya nchi.

Hata hivyo, wawekezaji kutoka nje ya nchi bado wanalitawala soko la hisa kwa kiwango kikubwa na kwa mujibu wa madalali na washauri wa uwekezaji wa DSE, wawekezaji kutoka nje ndio wanashikilia kiwango kikubwa cha biashara ya soko.

Kwa siku ya mwisho wa wiki, ripoti zinaonyesha kwamba wawekezaji wa ndani ya nchi walianza kutoweka kwani ushiriki wao kwenye biashara siku hiyo haukuvuka hata asilimia mbili kwa pande zote.

Ripoti imeonyesha kwamba, siku hiyo, kiasi cha shilingi bilioni 4.184 zilipatikana kutokana na biashara ya hisa, lakini ushiriki wa wawekezaji wa ndani ulikuwa ni mdogo kwa chini ya asilimia moja.

Katika siku hiyo, wawekezaji wa ndani walishiriki kwa asilimia 0.18 kwa upande wa ununuaji na asilimia 0.32 kwa upande wa ununuaji. Kampuni zilizofanya biashara siku hiyo ni CRDB, NMB, DSE, TBL na Swissport.

Hata hivyo, hakukuwa na wawekezaji kwenye kampuni zilizoorodheshwa kutoka masoko ya nje ya nchi kwani hakukuwa na mwekezaji yeyote aliyeuza wala maombi ya kununua hisa hizo.

Kwa ujumla, mauzo ya hisa kwa wiki jana yanaonyesha kushuka kwani kiasi cha shilingi bilioni 5 kilikusanywa kutokana na kuuza na kununua hisa ikilinganishwa na shilingi bilioni 13 za wiki ya awali.

Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa pia zilipungua hadi kufikia hisa 500,000 wiki iliyopita kutoka hisa milioni 2.8 za wiki ya awali.

Kampuni zilizoongoza kwa biashara ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo iliongoza kwa asilimia 98.3 ikifuatiwa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ambayo ilikuwa na asilimia 0.7 na NMB ilifuatiwa kwa asilimia 0.6 ya mauzo yote ya hisa.

Hadi kufikia mwisho wa wiki, kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa awali DSE cha TSI kilipungua hadi kufikia pointi 3.550.11, kwa asilimia 70.17 huku kiashiria cha jumla sha soko DSEI kikiongezeka kwa asilimia 47.40 hadi pointo 2,197.82.

Kampuni zilizoongoza kwa ongezeko la hisa hadi kufikia mwishoni mwa wiki jana kwa mujibu wa ripoti za DSE ni Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) kwa asilimia 11.98 ikifuatiwa na Shirika la Ndege la Kenya (KQ) ambalo bei ya hisa iliongezeka kwa asilimia 8.33.

Bei ya hisa za Acacia, kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu iliongezeka kwa asilimia 2.47 huku bei ya hisa za Benki ya Biashara Kenya (KCB) ikiongezeka kwa asilimia 1.72.

Hadi mwishoni mwa wiki jana, bei za hisa za NMB, Jubilee Holdings na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) zilipungua, lakini hazikufikia asilimia nne.

Meneja wa miradi na masoko wa DSE Patrick Mususa alisema kwamba ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko uliongezeka kwa shilingi bilioni 500 kutoka shilingi trilioni 18.6 wiki ya awali hadi shilingi trilioni 19.1 wiki iliyopita.

Katika taarifa yake mwanzoni mwa wiki hii, Mususa alisema kwamba kwa upande wa kampuni za ndani, mtaji wake umebakia kwenye kiwango kile kile cha shilingi trilioni 7.5.

Kiashiria cha kampuni za ndani kiliendelea kubaki kwenye wastani wa pointi 3,500 wakati kiashiria cha sekta ya viwanda nachi kilibakia kwenye wastani wa wiki ya awali kwenye 4,508.

Hata hivyo, kiashiria cha sekta ya huduma za kibiashara (CS) wiki iliyopita kilibakia pale pale kwenye 3,158.

Madalali wa soko wanasema kwamba kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji kutoka nje ya nchi inatokana na kupungua kwa thamani dola ya Marekani, kwani wakiuza hisa zao wakati huu wanapata fedha za ziada.

Pia wakati thamani ya dola ikiongezeka dhidi ya shilingi ya Tanzania, wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi hufurika kununua kwani wanapata idadi kubwa ya hisa ikilinganishwa na kipindi ambacho fedha ya Tanzania inakuwa imara.

Wakati huo huo, wawekezaji mbalimbali wa ndani sasa wameanza kujiandaa kwa ajili ya ujio wa hisa za kampuni za simu ambazo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa kuorodhesha hisa zao.

Awali ilipangwa kuwa, hadi kufikia Desemba mwaka jana, kampuni zote za mawasiliano na simu, zipatazo 80, zingetakiwa kuwa tayari zimeshaorodhesha hisa zao kwa ajili ya kuuzwa kwenye soko.

Hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi huu, ni kampuni tatu tu za Airtel Tanzania, Vodacom na Tigo tayari zimeshajiandaa kwa utaratibu huo kwa kuwasilisha maombi kwenye mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA).

Mamlaka ya Mitaji na Dhamana tayari imethibitisha kupokea kwa maombi ya kampuni hizo na taarifa za awali zinaonyesha kwamba kampuni hizo za simu huenda zikaanza kuuza hisa zao katika robo hii ya kwanza ya mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *