Wazazi wana wajibu kuboresha Shule za Kata

MSOMAJI wa safu hii kutoka mkoani Mwanza aitwae Joseph, wiki iliyopita aliniandikia ujumbe  mfupi wa simu (SMS) akinitaka niwe pia nazungumzia masuala ya kitaifa kuliko yale ya Mkoa wa Kilimanjaro tu kila wiki.

Baadaye nilimpigia simu na kumweleza kuwa mwandishi wa habari anayejikita kwenye uandishi wa safu (columnist) huwa anajaribu kuelezea na kuchambua kwa undani jambo ambalo ameliona katika jamii, na kisha kutoa maoni yake kuhusu nini kifanyike ili kutafuta suluhu ya hicho alichokijadili.

Nilimwambia ndugu Joseph kuwa ni vigumu kwa mwandishi aliyepo mkoani Kilimanjaro kuchambua mambo yanayoendelea Katavi au Rukwa, Mikoa pekee nchini ambako bado sijafika, na kama akijitokeza mwandishi wa maeneo hayo akaandika kuhusu mambo ya maeneo hayo, basi huenda akawavutia zaidi wasomaji wa mikoa hiyo.

Kwa kufuata ushauri wa huyu msomaji wangu wa Mwanza, leo nimeamua kuandika kuhusu shule zetu za kata nchi nzima, na ni kitu gani kinaweza kuziboresha , na kuwafanya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo kupata matokeo mazuri ya mitihani ya kidato cha nne na cha sita, tofauti na sasa ambapo nyingi huwa zinapata matokeo mabaya sana.

Ninafanya uchambuzi huu kwa vile mwaka 2012 nilibahatika kutembelea mikoa mbalimbali, kuangalia mazingara ya shule za kata, na kitu gani kingeweza kufanyika ili kuziboresha shule hizo ambazo zilianzishwa na serikali zaidi ya miaka 10 iliyopita, ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi wanaomaliza elimu ya msingi kupata elimu ya sekondari.

Bahati nzuri ni kwamba shule hizo zimeenea kila Kata Tanzania Bara, na ukitembelea maeneo ya Wilaya ya Rombo, kwa mfano, kuna Kata imepiga hatua na ina shule nne za sekondari.

Mkoani Mwanza pia kuna Shule nyingi za Kata, ikiwamo ile ya Kitangiri ambayo kwa miaka kadhaa ilikuwa inafanya vizuri sana kwenye mitihani ya kidato cha nne,  na ninashangaa ni kwa nini siku hizi hatuisikii tena ikifanya vizuri. Huo ni mjadala mwingine.

Bahati mbaya sana ni kwamba baadhi ya shule nyingi za kata hazina walimu wa kutosha na hasa wale wa masomo ya sayansi, na katika maeneo mengine kama Mkoa wa Shinyanga kuna shule nilitembelea hivi karibuni ilikuwa na wanafunzi 400 lakini walimu walikuwa ni wanne tuu.

Unaweza kuwaza na kujipa jibu mwenyewe ni kitu gani kinaweza kutokea wakati wanafunzi ambao wapo kwenye umri kati ya miaka 14 na 18, wanapoachwa wenyewe bila usimamizi wa karibu wa walimu na walezi wengine, na hii inaweza kuwa sababu ya wanafunzi kupata ujauzito bila kutarajia.

Serikali ya awamu ya tano kwa makusudi kabisa imeondoa ada kwenye Shule za Kata ili kutoa unafuu kwa wazazi kwani baadhi yao walikuwa wanashindwa hata ile 20,000/- kwa mwaka waliyokuwa wanapaswa kulipa ili kurahisisha uendeshaji wa shule hizo.

Ukweli ni kuwa baadhi ya wazazi kwa sasa walio na watoto wanaosoma Shule za Kata si wawajibikaji, na pia hawaoni umuhimu wa kuziboresha shule hizo ambazo zimejengwa katika vijiji na kata zao, ili kusaidia wanafunzi wa kizazi cha sasa na kile kijacho.

Hebu tujiulize maswali yafuatayo. Je, kuna haja gani ya kuwa na shule ya sekondari ya kata ambayo haina walimu, vitabu au maabara?

Je, haingekuwa bora zaidi kwa wanafunzi hao kubaki nyumbani na kujishughulisha na mafunzo mengine kama vile kilimo, ufugaji, useremala na hata ushonaji badala ya kutoka nyumbani asubuhi kwenda shule na kurudi nyumbani bila kusoma somo lolote?

Tukumbuke kuwa kuna idadi kubwa ya wahitimu wa kozi za ualimu kwa ngazi ya shahada na stashahada ambao wapo mitaani kwa maelfu wakisubiri ajira za serikali.

Wakati wakisubiri neema hiyo, je, kata na vijiji hawawezi kuwatumia kwa njia moja au nyingine kuwapa kazi ya kufundisha katika maeneo yao huku wakiwalipa posho kidogo?

Mimi naona viongozi wetu wa maeneo hayo wamelala kidogo na wanahitaji kuamshwa ili watafute njia mbadala za kuwapata walimu wa muda katika shule zao, wakati wakisubiri serikali kupeleka walimu kwenye shule zao kama ilivyofanya wiki iliyopita kupitia TAMISEMI ambapo walimu wa sayansi wamepelekwa shule mbalimbali nchi nzima.

Kwa maoni yangu, Shule za Kata zinapaswa kutafuta njia muafaka kuwapata walimu wa muda, na nadhani serikali ingefurahi kusikia kuwa kata fulani imetafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuwalipa ‘posho’ walimu wanaojitolea kufundisha katika shule hizo.

Hebu tuzungumze kwa vitendo zaidi.

Mfano, kama shule fulani ya kata yenye wanafunzi 600 ingeamua kumwambia kila mzazi achangie shilingi 5,000 kwa mwezi ili kusaidia kuwapata walimu wa muda katika shule hiyo, jumla zingepatikana shilingi 3,000,000/-.

Na ikiamuliwa kila mwalimu alipwe posha ya 500,000/-, basi shule hiyo inaweza kupata walimu sita ambao wanaweweza kupunguza kwa kiwango kikubwa upungufu wa walimu katika shule zetu mbalimbali nchini.

Hebu fikiria mwalimu aliyehitimu mafunzo miaka mitatu iliyopita na kwa muda sasa amekuwa akikaa mtaani muda wote huo bila kuweka katika matendo kile alichojifunza, je, uwezo wake si unaendelea kupungua?

Najua kuna shule zinaweza kuogopa kufanya ninachokipendekeza hapa, lakini vijiji na kata vikifanya maandiko maalumu (proposals) na kuziwasilisha kwa mamlaka husika za juu serikalini, nadhani wanaweza kuruhusiwa kufanya hizo ‘ajira’ za muda kwa ajili ya wahitimu wetu wa ualimu na hivyo kuwasaidia wanafunzi wetu.

La muhimu kufanya hapa ni kutoa elimu kwa wazazi vijijini na mitaani, kuwaelimisha umuhimu wa elimu kwa watoto wao, na kama watapata mtaalam wa kuwanoa vyema, mchango wa 5,000/- kwa mwezi hautawashinda, kwani pesa hiyo kwa sasa inaweza kununua kilo mbili tuu za maharage au sukari.

Nimefanya uchunguzi hivi majuzi kwenye shule  moja ya binafsi ambapo kwa mwaka ada ni kama milioni mbili, na ukiangalia utakuta wengi wa wazazi wenye watoto katika shule hizo si matajiri, ila huwa wanajinyima mambo mengi ili watoto wao wapate elimu bora na yenye kiwango.

Wengi wa wazazi hao wamefanya hivyo baada ya kujifunza kutoka kwa marafiki na jirani zao ambao watoto wao wamesoma huko na baadaye kuendelea na masomo kwenye baadhi ya vyuo vikuu nchini.

Huko huko vijijini ambako kuna Shule za Kata wazazi wengi si hohehahe kama tunavyoweza kufikiria, kwani unawakuta wanakunywa bia na kula ‘kiti moto’ lakini wakiambiwa wachangie maendeleo ya shule yao wanaanza kuguna.

Wengi wao wana uwezo wa kupata elfu tano kwa mwezi kama nilivyopendekeza hapo juu, fedha ambayo itamsaidia mwanae kupata elimu bora, na mwisho wa siku aje kuyamudu maisha yake.

Nadhani Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikishirikiana na taasisi kama vile Haki Elimu na Twaweza wanaweza kupanga mipango madhubuti ya kuwaelimisha wazazi umuhimu wa kuchangia elimu ya watoto wao kwa kiwango kidogo kabisa.

Kuna taasisi kila mwaka zinakuja na ripoti zinazoonyesha hali mbaya ya elimu nchini bila kupendekeza nini kifanyike ili shule zetu ziwe za viwango na zinazotoa elimu sahihi kwa wanafunzi wake, na ni muda muafaka sasa kushirikiana katika kuziboresha shule hizi.

Elimu bora na sahihi inahitaji uwekezaji ambao utaziwezesha shule kuwa na majengo mazuri na ya kutosha, walimu, maabara, maktaba yenye vitabu vya kiada na ziada, na chakula cha kutosha kwani mwanafunzi anayehisi njaa hawezi kumsikiliza mwalimu barabara.

Shule za Kata zina wanafunzi wenye vipaji sana, na kama wangepata mazingara ya kujifunzia kama yale ya Feza Boys, Feza Girls, Marian, Saint Francis, Mazinde Juu, Maria Goretti na nyinginezo za binafsi zinazofanya vizuri, nina uhakika nyingi ya Shule zetu za Kata zingekuwa zinajitokeza katika ile nafasi ya kumi bora wakati matokeo ya mitihani yanapotangazwa kila mwaka.

Nimalizie kwa kuwapongeza walimu wanaofundisha Shule za Kata ambao wanajitahidi kutoa elimu kwa watoto wetu katika mazingara magumu yasiyo rafiki kwa wanafunzi kujifunzia, ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitabu, maabara na madarasa ya kutosha.

Wazazi wakijitoa vilivyo, Shule za Kata zitaimarika kitaaluma, na miaka ijayo zikaanza kutoa ushindani mkubwa kwa shule zinazomilikiwa na taasisi au watu binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *