Makala
Tafakuri Jadidi
Waziri wa viwanda bila viwanda, wa kilimo bila kilimo!
Johnson Mbwambo
Toleo la 241
30 May 2012

MACHI  2008, mshauri mmoja wa viwanda kutoka Japan aliletwa nchini  na Rais Jakaya Kikwete kuishauri serikali yake namna inavyoweza kuleta “Mapinduzi ya Viwanda” hapa nchini.

Kitendo kile cha Rais Kikwete kuleta mshauri  huyo kutoka Japan kulinifanya, wakati ule, nijenge imani kuwa rais wetu alikuwa amepania kweli kweli kuifanya Tanzania kuwa tena nchi ya viwanda na kilimo.

Miaka minne na nusu sasa imeshapita tangu mshauri yule wa viwanda kutoka Japan amalize kazi yake  ya kumshauri Rais Kikwete juu ya suala hilo, na bado hakuna dalili yoyote  ya kujengwa viwanda vipya hapa nchini; achilia mbali kufufua vile vilivyokuwa vya umma vilivyouzwa kwa wawekezaji binafsi, na kisha vikatelekezwa au vikageuzwa maghala.

 Sina hakika na hili, lakini naamini ya kuwa tangu Rais Kikwete aingie madarakani, karibu miaka saba iliyopita, hakuna kiwanda kipya chochote kikubwa kilichojengwa nchini, na hapa naamanisha kiwanda kikubwa (heavy industry),  na si hivi vya kusindika matunda au nafaka vya Bakhressa na Mohamed Enterprises.

Miaka saba ya utawala wa Rais Kikwete bila kujengwa viwanda vipya vikubwa nchini kumenikumbusha kauli iliyotolewa na mshauri yule wa viwanda wa Japan kabla hajaondoka nchini.

Mshauri yule, Yoshiyasu Mizuno, alinukuliwa na gazeti la Serikali la Daily News, toleo la Machi 6, 2008, akisema kwamba kuyafikia Mapinduzi ya Viwanda si lelemama.

Alisema ya kuwa,  ili Tanzania iweze kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea katika  Visheni 2025 (ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda), ni lazima uchumi ukue kwa asilimia 15.6 kwa mwaka na iendelee kwa kiwango hicho hicho kwa miaka 18 mfululizo!

Lakini wiki iliyopita tuliambiwa na Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Benno Ndulu, kwamba uchumi wa Tanzania, kwa mwaka jana, ulikua kwa kiwango cha asilimia 6.5 tu. Sasa, asilimia 6.5 na asilimia 15.6 za Mjapani huyo ni wapi kwa wapi?!

Mimi si mchumi, lakini kwa kiwango changu kidogo cha elimu bado  natambua kwamba si lelemama uchumi wetu kukua haraka kutoka kiwango chake cha sasa cha takriban asilimia saba na kufikia asilimia 15.6 alichokitaja Mjapani huyo;  achilia mbali lile sharti jingine la uchumi kusimama katika kiwango hicho hicho cha asilimia 15.6 kwa miaka 18 mfululizo.

Ukizingatia nidhamu yetu mbovu ya uchapaji kazi,  na ukizingatia hali ya kushamiri kwa ufisadi katika karibu kila sekta serikalini, na bila kusahau kuwa sekta ya viwanda ni kama vile haipo hapa nchini, na ukizingatia ukweli  pia kwamba mawaziri wengi na ma-DC hujishughulisha zaidi na kusaka utajiri kuliko kulichapia kazi taifa, utaelewa ni kwa nini si rahisi kwa Tanzania hii, chini ya chama tawala CCM, kufikia kiwango cha kukua kwa uchumi cha asilimia 15.6 katika miaka ya karibuni.

Na ndiyo maana miaka karibu minne na ushee hivi  imeshakatika tangu Mjapani yule aishauri Serikali ya Kikwete namna ya kufikia Mapinduzi ya Viwanda hapa nchini, lakini mpaka sasa bado hakuna viwanda vyovyote vikubwa ambavyo vimeanza kujengwa.

Sana sana tunachokisikia ni majuto au tuseme ni kujikosha kwa watawala wetu na dhambi ile kubwa waliyoifanya inayoendelea kuwatafuna ya kuuza na kuua viwanda vilivyoanzishwa enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Mwanzoni mwa mwaka huu, kwa mfano,  tulimsikia aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, akikiri kwamba kama kuna kitu alichokisahau wakati wa utawala wake ni kuendeleza kilimo! Huyo huyo Mkapa, baadaye, akanukuliwa tena akisema ya kuwa haiwezekani Tanzania kumaliza tatizo la ajira bila kujenga viwanda.

Hebu fikiria: Rais wa nchi anawezaje kukisahau kilimo; ilhali asilimia 85 ya wananchi wake wanajishughulisha nacho? Hebu fikiria: Mkapa atasemaje kuwa hatuwezi kumaliza tatizo la ajira bila kujenga viwanda wakati ndiye aliyesimamia kuviuza, kwa bei poa,  tulivyokuwanavyo kwa wawekezaji wababaishaji ambao wamevitelekeza?

Ndiyo maana huwa najiuliza: Hivi Rais Kikwete alifikiria nini kumleta Mjapani yule mwaka 2008 kuishauri Serikali yake namna ya kufikia Mapinduzi ya Viwanda wakati tulikuwanavyo tukaviua?

Nina shaka kwamba hata chuma kilichovumbuliwa kule Liganga kitaishia Beijing kwenye viwanda vya Wachina badala ya kitusaidie kuyafikia haraka Mapinduzi ya Viwanda.

Ingekuwa ni enzi zile za utawala wa Mwalimu Nyerere ambapo tayari tulikuwa na viwanda kemkem, vikiwemo vilivyotumia mazao ya wakulima kama vile Mwatex, Sunguratex na Mutex, ni dhahiri chuma cha Liganga kingeharakisha zaidi safari yetu ya kuwa nchi ya viwanda vikubwa. Nasema hivyo; maana tulikuwa na pa kuanzia.

Lakini  kwamba sasa watawala wanayatamani Mapinduzi ya Viwanda baada ya kuwa wameua viwanda vyote, ni kitu ambacho, kwa hakika, kinakaribisha maswali mengi hadi sasa juu ya umakini wetu na uwezo wetu wa kufikiri.

Na ndio maana, binafsi,  sishangai kwamba miaka minne na nusu imepita tangu aletwe mshauri yule wa viwanda kutoka Japan, na bado hakuna kiwanda kikubwa hata kimoja ambacho kimejengwa nchini.

Kwa hakika, kuna wakati huwa najiuliza kama bado kuna umuhimu wowote, kwa sasa, kuwa na wizara ya viwanda yenye mawaziri wawili. Wizara ya viwanda inayosimamia viwanda vipi hasa?

Hivi kazi ya kila siku ya waziri wetu wa viwanda ni ipi? Vyovyote vile; waziri anayeisimamia wizara hiyo kwa sasa namshauri atembelee Kiwanda cha Nguo cha Urafiki cha Dar es Salaam ajionee kinavyogeuzwa,  kidogo kidogo, kuwa yadi ya kuuzia magari!

Aidha, katika hali ya kawaida, mtu angetaraji kwamba baada ya Serikali ya CCM kusambaratisha viwanda na ndoto ya Mapinduzi ya Viwanda kuyeyuka licha ya ujio wa mshauri huyo kutoka Japan, sasa nguvu zote zingeelekezwa katika kampeni ya kufikia Mapinduzi ya Kilimo (Green Revolution), lakini wapi! 

Licha ya kwamba asilimia 85 ya Watanzania ni wakulima wadogo wadogo wanaoishi  vijijini, serikali bado imewatelekeza ingawa ina programu yake maarufu ya kinadharia zaidi inayoitwa Kilimo Kwanza. 

Rais Kikwete aliibuka na hicho kinachoitwa Kilimo Kwanza, lakini matunda yake mpaka sasa hayaridhishi. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,  kila nilipopata bahati ya kutembelea vijiji vya mikoa kadhaa nchini nimekuwa nikijitahidi kutafuta ushahidi wa mabadiliko ya kilimo chetu yanayotokana na ujio huo wa Kilimo Kwanza. Nikiri kuwa sikuyaona.

Na hata watawala wenyewe ni mara chache mno utawasikia wakienda vijijini kuhimiza Kilimo Kwanza au angalau kwenda kufanya tathmini zao wenyewe za papo kwa papo za  mafanikio ya huo ujio wa Kilimo Kwanza. Lakini sivyo wanavyofanya; kwani wanapapatikia zaidi safari za Ughaibuni kuliko za vijijini, na hasa Rais Kikwete.

Hivi ni mara ngapi umepata kuwasikia watawala  wetu wakitembelea vijiji vyetu kuhimiza kilimo kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Nyerere enzi zake? Hivi ni mara ngapi umepata kuziona juhudi za wazi wazi za watawala wetu za kuwaelemisha wakulima wetu vijijini kuhusu kilimo bora?

Ndugu zangu, ninachosema ni kwamba, chini ya Serikali ya CCM, ni ndoto kwa Tanzania kufikia Mapinduzi ya Kilimo, na ni ndoto zaidi kufikia Mapinduzi ya Viwanda.

Ni kweli tunao mawaziri wa kusimamia sekta hizo mbili, lakini ukweli ni kwamba wapo kama hawapo! Mambo yakienda hivi hivi, kuna hatari huko mbele ya safari tukawa na Waziri wa Kilimo asiyesimamia kilimo chochote, na tukawa pia na Waziri wa Viwanda asiyesimamia viwanda vyovyote!

Hayo, ndugu zangu,  ndiyo mavuno ya hadaa za ushauri wa mabeberu wa dunia. Tulihadaiwa na asasi za Bretton Woods za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tukauza viwanda vyetu na kuiua sekta ya viwanda. Tena watawala walifanya hivyo kwa ukaidi mkubwa; huku wakiwakejeli wale waliowapinga akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Tukumbushane: Akihutubia kwenye sherehe za Mei mosi, 1995, mjini Mbeya, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hivi kuhusu uuaji huo wa sekta ya viwanda nchini: “Nchi haiwezi kuendelea hata kidogo kwa kupuuza viwanda. Nchi tajiri duniani zenye viwanda huvibana vinchi vidogo viache mambo ya viwanda. Taabu yetu ni kwamba wala viongozi wetu hawakatai. Wanakubali tu. Lakini sisi ni madodoki?”

Lakini walimsikiliza  Mwalimu Nyerere, wakampuuza. Wakaendelea kuviuza viwanda vyetu kwa wawekezaji wababaishaji. Baada ya kumaliza kuviuza na kuviua na nchi kugeuka kuwa dampo la bidhaa hafifu za nje, eti sasa ndo wanayatamani Mapinduzi ya Viwanda! Eti sasa ndo wanazinduka na kutambua kuwa bila kujenga viwanda hatuwezi kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu nchini!

Lakini jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba bado wanaendelea kuuamini ushauri wa mabeberu kuhusu sekta yetu nyingine – sekta ya kilimo. Majuzi hapa Rais Kikwete aliitwa Marekani na Rais Obama ili kupewa “mwongozo” wa namna ya kuendesha sekta ya kilimo nchini.

Kina Obama walimwambia kwamba eti mkombozi wetu ni kilimo cha wawekezaji wakubwa kutoka nje, na kwamba hilo ndilo tulipe kipaumbele badala ya kung’ang’ania kuwaendeleza wakulima wetu wadogo wadogo nchini! 

Kwa ushauri huo wa Washington ambao tayari watawala wetu wameshaukubali, miaka si mingi sehemu kubwa ya ardhi yetu yenye rutuba nchini itaangukia mikononi mwa umiliki wa wawekezaji hao wa kigeni – mambo yale yale ya zama za ukoloni!

Na japo tunapozwa hivi sasa na watawala wetu kwa kupigiwa kibwagizo cha wimbo wa land for equity, yaani kwamba tutabaki na asilimia 25 ya hisa katika kila mradi  wa kilimo kikubwa cha biashara kitakachoanzishwa na wawekezaji wa kigeni, shaka yetu  iko pale pale.

Na shaka yenyewe  ni kwamba, mwisho wa yote, sehemu kubwa ya ardhi yetu yenye rutuba itamilikiwa na Wazungu (mwenye asilimia 75 ya hisa ndiye mmiliki), na kwamba wazawa wengi watakuwa manamba  (vibarua) tu katika mashamba hayo makubwa yatakayomilikiwa na Wazungu.

Hilo likihitimishwa, je sisi kama taifa tutakuwa tumeshika wapi?  Nauliza hivyo; maana kwenye viwanda tulifuata ushauri wao tukaviuza vyote na kuiua sekta hiyo, na kisha tukageuka  kuwa soko la bidhaa za viwanda vyao.

Na sasa hao hao wanataka tuachane na kukiendeleza kilimo cha wakulima wadogo wadogo ambao ndio wengi Tanzania, na badala yake tutegemee kilimo kikubwa kitakachoendeshwa na Wazungu kutoka Ughaibuni! 

Hebu niambieni: Hayo yakihitimishwa, je, hatma ya uchumi na usalama wa taifa letu bado utakuwa mikononi mwetu wenyewe?

Tafakari!

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Johnson Mbwambo
mbwambojohnson@yahoo.com

Maoni ya Wasomaji

Mipango ya wawekezaji wakubwa mbele ya safari iatkuwa ni balaa tupu.Kama serekali haijui watu wake wanaongezeka na ardhi haiongezeki inaweza kuanza mpango wa kumega ardhi yake kwa wawekezaji wakubwa.
Kwa nini walenge wawekezaji wakubwa wasiwasaidie
wakulima wadogowadogo kwa kutumia wataalamu wa vyuo.
Nchi ina kilio cha cha uchumi lakini haiweki mipango ya kuenenda na uweza wake kiuchumi.
Mimi nakuambia ardhi ya Tz imesetiri aibu kubwa ya Watanzania.Jambo linalofanyika hapa ni mtu mvivu anatafuta mtu wa kumlimia ili apate chakula.Ardhi yaTanzania hutumika kwa kilimo,ufugaji na hifadhi za taifa hivyo ardhi ni ajira kubwa ya Watanzania.Tukifanya hivi tutakuwa hatujatenda haki kwa vizazi vijavyo.Mwekezaji katika ardhi akiisha kulima atataka aone kilimo hicho kinampa faida na sio kwamba ni kwa ajili ya Watanzania.Hebu tufikiri kwamba ni juhudi gani za makusudi za kilimo zilizofanyika lakini hatujafanikiwa.Mkileta wakulima
wakubwa mtakuwa mmeuza sehemu ya uhai wataifa hili.

Hii ni hatari sana kupuuza ya watu wanaoona mbali.
Viwanda ni muhimu sana kwa uchumi wetu na pia tatizo la ajira litakuwa halipo.
Katika makosa ambayo tutakuja kuyajutia maishani ni hili wanalotaka kuwapa hao wawekezaji ARDHI YA KULIMA, eti wao wamiliki asilimia 75 na sisi asilimia 25. Huu ni ujinga mkubwa na ni kitu kisichowezekana kufanywa.
ARDHI ndiyo mali yenye thamani kubwa zaidi kuliko hata hayo madini tunayowapa wachimbe bure.
Hao wanaojiita wawekezaji wamefuatilia sera zetu za KILIMO KWANZA na wamegundua hii ni NADHARIA na si vitendo,sasa wao wameingia kwa gia ya uwekezaji ili kutupora ARDHI YETU kwa ujanja wa kulima. Na ninajua udhaifu wa utawala wetu katika huo uwekezaji watawekeana mikataba ya miaka 100. Na ukishafanya hivyo ni sawa umekabidhi bure ARDHI YETU.
TUEPUKANE NA WIZI HUU WA MCHANA KWEUPE, hautatusaidia watanzania wengi,huu ni mpango wa kuwasaidia watu wachache hasa hao watakaofanya makubalianomya mikataba.

Viongozi wakienda vijijini siku hizi ni kununua mashamba na siyo kuwaelimisha wananchi  juu ya kilimo bora.
Kama hujaona wananchi manamba katika nchi yao nenda Arusha, Mbulu kwenye mashamba makubwa ya ngano- uone maisha ya waajiriwa wa huko yalivyo.
ndivyo viongozi wetu wanavyotaka tuwe tena.
Zimbabwe nyingine itatokea hapa Tanzania kama uuzaji wa nchi yetu utafanyika- tutaanza kudai tena uhuru.

Toa maoni yako