Wengine tunalia, wengine wanafurahia

WAKATI tumejawa na simanzi kubwa juu ya tukio lililompata rafiki, ndugu na Mtanzania mwenzetu, Absalom Kibanda ambaye aliyefanyiwa unyama kwa kupigwa na kuumizwa hadi kutolewa jicho lake, wakati familia ya Kibanda inapitia wakati mgumu na wakati Kibanda mwenyewe analia na kuumia kwa maumivu makali kutokana na unyama aliofanyiwa, kuna wanaoshangilia tukio hilo na kuendelea kusambaza ujumbe wa kejeli kwenye mitandao ya kijamii.

Watu hao wanaoashiria kushangilia unyama aliofanyiwa Kibanda, wanahoji kama tukio la Kibanda nalo limetendwa na Rama.

Tunakumbuka sote kwamba kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Dk. Steven Ulimboka, sehemu ya lawama zilielekezwa kwa Rama, ambaye inadaiwa ni mtumishi wa Ikulu. Hadi leo wapo baadhi wanaoamini Ikulu ilihusika  kwa njia moja ama nyingine kwa kitendo cha kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Dk. Ulimboka.

Kejeli ni kwamba, kwa vile Kibanda, alipigwa akiingia nyumbani kwake; je hao majambazi waliomvamia ni wa Ikulu? Umezuka mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii. Hoja ikiwa  swali lililoulizwa na watu hawa, linaonyesha aina ya kejeli?

Pia kuna baadhi ya magazeti yaliyoandika yakiwashambulia watu hawa kwa tabia yao ya kutenda kinyume cha maadili ya Watanzania tuliyozoea. Na wengine wameenda mbali kusema kwamba watu hawa ambao wanashangilia maumivu na mateso ya wenzao, hapana shaka wanafahamu kwa kiasi kikubwa chanzo cha maumivu ya Kibanda na kwamba ipo siku kinga yao itayeyuka na watajikuta njia panda wakiisubiri hasira na hukumu ya wananchi.

Sipendi kutaja majina ya watu hawa, maana mitandao ya kijamii ina mengi. Ni vigumu kuthibitisha pasipo shaka kwamba hawa wanaotajwa ndiyo waliotuma ujumbe wa kejeli. Mtu anaweza kujiita Karugendo, kumbe ni Onyango, mtu anaweza kuweka picha ya msichana kwenye ukurasa wake, kumbe yeye ni mvulana. Hivyo hapa majina si muhimu, bali ukweli ni kwamba kuna watu wametuma ujumbe wa kukejeli tukio la kupigwa na kuumizwa kwa Kibanda kwenye mitandao ya kijamii.

Inawezekana, wale waliomtesa Kibanda ni wale wale waliomtesa Dk. Ulimboka na inawezekana kwamba hawa wanaokejeli kupigwa kwa Kibanda, wanafahamu ukweli huo na labda walishiriki kwa namna moja ama nyingine. Pia inawezekana waliomtesa Kibanda, ni tofauti na  waliomtesa Dk. Ulimboka. Vyovyote vile hiki ni kitendo kibaya, ni unyama na wala si tukio la mtu kufanyia kejeli au kushangilia.

Kama Jeshi la Polisi lingekuwa makini,  basi lingeanza upelelezi wa sakata la Kibanda kwa kuwahoji hawa wanaokejeli tukio hili. Tumeambiwa wale waliowatumia sms za matusi Spika na Naibu wake, wamesakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Kama hilo limewezekana, kwa nini hili la watu kutumia mitandao kukejeli maumivu na misiba ya wengine liachwe hivi hivi?

Ina maana Jeshi la Polisi lina uwezo wa kufanya kazi sehemu fulani na kushindwa kufanya kazi upande wa waheshimiwa na vigogo? Ni vizuri jambo hili likiwekwa wazi, ili watu walifahamu vizuri Jeshi lao la Polisi, hili liwe jibu la polisi kushindwa kulinda usalama wa raia.

Si utamaduni wa Watanzania kushangilia misiba, kufurahia na kushangilia wakati majonzi. Hata ukiachia mbali utamaduni huo wa Watanzania, kila anayejali utu hawezi kushangilia msiba wa jirani yake. Kibanda, alipigwa, ameumizwa hadi jicho lake limetolewa; mtu ambaye alizaliwa akiwa na viungo vyote vya mwili wake, sasa ataishi maisha yake yote na ulemavu wa kulazimishwa; kuna lipi la kushangilia hapa? Ni maadili gani tunataka kujenga katika taifa letu? Haya si maadili waliotuachia waasisi wa taifa letu.

Juni 28, 1962, wakati Mwalimu Nyerere akiwasilisha bungeni muswada wa kuifanya iliyokuwa Tanganyika kuwa Jamhuri, alisema:

“Hoja lazima ijengwe kwamba hatimaye kinga madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini, hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa. Taifa linapokuwa halina maadili yanayowezesha Serikali kusema hatuwezi kufanya hivi, huu si Utanganyika. Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama wangekuwa na Katiba iliyoandikwa vizuri sana. Bado raia wanaweza kukandamizwa…. Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya Rais yeyote yule kusema ninayo madaraka ya kufanya jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si Utanganyika. Au kwa watu wa Tanganyika, iwapo wamekosea na kumchagua mwendawazimu kuwa Rais, mwenye madaraka ndani ya Katiba ya kufanya XYZ, akijaribu kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme hatukubali hili lifanyike, hata alitake Rais au Rais maradufu, hatulikubali, maana huu si U-Tanganyika."

 Tujiulize, U-Tanzania, unanyesha kama mvua? Inatosha kuzaliwa Tanzania, mtu akatenda na kuishi ya U-Tanzania? Mtanzania, hawezi kuisaliti nchi yake, hawezi kuipora nchi yake. Mtanzania wa kweli ni mzalendo. Mtanzania wa kweli hawezi kuishangilia misiba na mateso ya ndugu zake. Mtanzania wa kweli hawezi  kushangilia kupigwa na kuumizwa kwa Kibanda na wengine wanaoteswa na mfumo huu wa majambazi.

Mtanzania wa kweli analitanguliza taifa bila kuangalia kwanza maslahi yake binafsi, analitanguliza taifa bila kutanguliza tumbo lake. Huyu yuko tayari kuyapoteza maisha yake kwa kutetea uhai wa taifa lake. Ili kuujenga U-Tanzania, Mwalimu Nyerere na waasisi wengine, walibuni mbinu na mifumo mbalimbali: Lugha moja, siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa, kuwasambaza watoto kwenye shule za mikoa mbalimbali, jeshi la kujenga taifa, mwenge wa  uhuru.

La msingi, ambalo ni muhimu kujiuliza, ni tunaendelea kuwepo na kuendelea kuishi ili  kufanya nini? Mungu, anaendelea kutuweka tu kama mapambo ya dunia? Mapambo ya Afrika? Mapambo ya Tanzania au mapambo ya familia zetu? Tupo tu kama maua yanayochanua na kupendeza kisha kunyauka? Au tupo kuleta mabadiliko? Tupo kutoa mchango wetu? Tupo kuonyesha kwamba sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu?; kwamba tuna akili na utashi; kwamba tunatambua mema na mabaya; kwamba tupo ili kusambaza haki, wema na huruma duniani kote? Tupo kulijenga taifa la Tanzania au kulibomoa?

Tumeambiwa waliomteka, kumpiga na kumuumiza Kibanda, watasakwa na kukamatwa. Tuliambiwa hivyo hivyo alipotekwa, kupigwa na kuumizwa Dk. Ulimboka, tuliambiwa hivyo hivyo alipopigwa risasi padri kule Zanzibar na tuliambiwa hivyo hivyo alipopigwa risasi na kupoteza maisha padri mwingine kule Zanzibar.

Inawezekana tukaambiwa hivyo hivyo kesho na keshokutwa likitokea kwa Mtanzania mwingine. Kama tukio la kutekwa, kupigwa na kuumizwa linageuzwa kejeli, hapana shaka likatokea tena.

Inaelekea kuna kundi la watu ambao wamejipanga kutumia nguvu walizo nazo kuwanyamazisha wale wote wanaojitokeza kuwasemea wanyonge. Kundi hili linajiaminisha kwamba baada ya kumaliza wabaya wake, litaishi kwa starehe milele – ni kujidanganya!

One thought on “Wengine tunalia, wengine wanafurahia”

  1. edward N says:

    father umesema kweli watu wengine mawazo yao ni mafupi sana wanfikiri kuua wengine kwao ni faraja ya muda tu lakini tutawaonea huruma punde tu,kwani tumeona kina Gadafi waligeka kuwa watu wa kuonewa huruma wakati walikua tishio hata akikutazama tu unaingiwa na hofu,

    mungu yupo na yetu macho na masikio kwa jinsi mungu atakavyotupendelea hadi kuyashudia haya,inawezekana kabisa kuna kundi la wahalifu ndani ya dola wanatumwa kufanya hayo ya kihalifu na kulindwana pengine wamehakikishiwa hakuna wa kuwagusa,lakini bahati nzuri kila wanalofanya liashindwa na wanajulikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *