HAKUNA shaka kuwa msafara mrefu wa mabasi mapya ya kisasa ya usafiri wa jiji zaidi ya 25 uliotoka bandarini na kupita kwenye barabara za Mandela na Morogoro ukielekea Kigali, Rwanda, mwishoni mwa wiki iliyopita, ulisisimua idadi kubwa ya wakazi wa jiji la Dar es salaam waliobahatika kuuona. Hata mimi nilisisimka.
Nilikuwa nimeketi kwenye kituo kipya cha daladala Mbezi Mwisho nikijiuliza ni kwa nini, pamoja na kuonekana kukamilika kituo hicho, bado hakijaanza kutumika, na badala yake kimekaa barabarani pale kama sehemu maalumu ya abiria wanaotoka mikoani kushangaa, wakati mabasi hayo ya usafiri wa ndani wa jiji la Kigali na viunga vyake yakipita.
Ni watu wengi tu waligeuza shingo zao ama kusimama kabisa kuyaangalia mabasi hayo yaliyokuwa na mvuto wa aina yake yakienda na kusimama kutokana na foleni zetu zilizokosa ufumbuzi yakiwa na logo yenye maneno ya kiingereza yenye maana ya ‘Njoo Tusafiri Pamoja’.
Nina hakika kuwa idadi kubwa ya wakazi wa jiji la walioyaona mabasi yale walibaki na maswali mengi kichwani; bila shaka mojawapo likiwa ni iweje nchi ambayo ki-eneo imepitwa na mikoa yetu mingi tu, kama sio yote, kuwa na uwezo wa kuagiza magari yale ya kisasa kwa ajili ya usafirishaji wa abiria kwenye jiji lake kuu; huku sisi tukiikabidhi kazi hiyo kwa kila mwenye vishilingi vyake viwili vitatu kumuwezesha kununua mkweche wa kusafirisha abiria kwenye jiji kuu letu!
Waama hakuna shaka pia kuwa wengi wa wakazi wa jiji hili walijiuliza iweje miongoni mwa raia milioni 8 tu wa nchi hiyo, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2008, watoke viongozi wenye uthubutu na ubunifu wa kuboresha usafiri wa wakazi wa jiji lao kuu wakati sisi tunaokaribia milioni 40 ndio kwanza viongozi wetu wanapiga bei Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na pesa za mauzo hayo kuingia kwenye akaunti binafsi za watu!
Waama, Watanzania waliojiuliza maswali haya walichanganyikiwa zaidi iwapo walibahatisha kusoma gazeti litolewalo kila siku ya Jumapili kwa lugha ya Kiingereza ambalo katika toleo la mwishoni mwa wiki hiyo hiyo lilikuwa na habari zinazohusu Shirika la Ndege la Rwanda kununua ndege mpya ya abiria ya kisasa aina ya Boeing 737-800NG, na hivyo kuongeza idadi ya ndege za shirika hilo kutoka tano hadi sita.
Imeelezwa kuwa ndege hiyo ilikuwa ni ya muundo mpya ambao kampuni ya Boeing ilikuwa imebuni na kuunda, na hivyo Rwanda kuwa nchi ya mwanzo kabisa barani Afrika kumiliki aina hiyo ya ndege.
La kusisimua zaidi ni kwamba Rwanda inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kununua ndege kwa pesa taslimu moja kwa moja kutoka kiwanda cha Boeing huko Seattle, Marekani tofauti na kukodisha kama yafanyavyo mashirika mengi ya ndege barani Afrika na kwingineko ikiwemo Tanzania.
Ndege nyingine ya aina hiyo inategemewa kuwasili nchini humo mwezi Oktoba mwana huu na hivyo kulifanya shirika la RwandAir kuwa na ndege saba.
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Tupende tusipende, haya ni maendeleo makubwa sana katika sekta ya usafirishaji katika nchi ambayo miaka kumi na sita tu iliyopita raia wake waligeukana na kuchinjana kama kuku.
Ni nani miongoni mwetu sisi wa ‘Amani, Utulivu na Mshikamano’ ambaye wakati ule wa mauaji yale ya kimbari angeweza kufikiria kuwa miaka kumi na sita tu baadaye nchi hiyo ingekuwa imejivua gamba la ukabila lililosababisha raia kuuana na ingekuwa inaelekea kuwa miongoni mwa nchi chache sana za kiafrika ambazo sekta yake ya usafiri ni mfano wa kuigwa na kutuacha mbali sisi wa Amani na Mshikamano?
Wakati Rwanda ikilijenga shirika lake la ndege sisi ndio kwanza tunaua la kwetu; huku mamia ya wafanyakazi wake wakiendelea kupokea mishahara wakati shirika husika halina ndege hata moja inayopaa hewani! Mizaha mingine unashindwa kuamua ulie ama ucheke.
Kwa hakika, wakati wenzetu wa Rwanda, acha kwingineko, wakipaa, sisi ni kama ndio kwanza tunatambaa. Maamuzi yetu mengi kwenye sekta ya usafiri nchini ni mzaha mtupu.
Angalia mzaha kama wa SUMATRA kukurupuka na kufungia kampuni mbili za mabasi kutokana na mabasi ya kampuni hizo kuhusika kwenye ajali mbili tofauti zilizosababisha wananchi wetu kadhaa kupoteza maisha.
Ni mzaha kwa SUMATRA kukurupuka na kuzifungia kampuni hizi mbili tu; huku ikiacha kuifungia kampuni nyingine kubwa ya mabasi ambayo tokea mwaka huu uanze mabasi yake yamehusika kwenye ajali nyingi zilizosababisha upotevu wa mali na maisha ya Watanzania wenzetu!
Na kama hicho sio kichekesho tosha, hata baada ya kutangazwa kufungiwa mabasi ya kampuni hizo yaliendelea kuonekana yakidunda mzigo na ikawa kichekesho pale ilipotangazwa kuwa yametolewa kifungoni; huku Usalama Barabarani wa mkoani Morogoro wakisema kuwa walikuwa hawajapata hata barua rasmi ya mabasi hayo kufungiwa ili wachukue hatua zinazopaswa!
Angalau tunaweza kusema kwamba hawa wamejitahidi kuonekana wamechukua hatua kuliko waheshimiwa wetu ambao kila ajali inapotokea na kupoteza maisha ya Watanzania wenzetu wanaishia kuwaasa, kuwataka, kuwatahadharisha na nini tena sijui, madereva wetu kuepuka kuendesha kwa kasi magari yao, basi. Hadithi inaishia hapo hadi ajali nyingine Itakapotokea!
Ni vurugu na mizaha kama hii kwenye sekta yetu ya usafiri ndio maana tumeshindwa hata kuwapa watoto wetu wanaosoma shule usafiri wa uhakika ukiacha wale wanaosoma shule za binafsi na badala yake tumeiacha hatima yao kwenye mikono ya makondakta wa daladala jijini.
Naam, hawa hawa makondakta ambao kaulimbiu ya customer care kwao ni ki-China kitupu; ndio maana hawaachi kusimama kwenye vimlango vyembamba vya mabasi yao wakihimiza abiria kuingia haraka kwenye gari huku kijiti cha kuchokonolea meno kikiwa mdomoni na kuwa chanzo tosha cha mtu kutobolewa jicho!
Tukumbuke kwamba benki ya CRDB ilitoa mabasi kwa ajili ya kusaidia usafiri wa wanafunzi jijini. Bahati mbaya kauli ya kutaka makampuni na mashirika mengine kuchangia mabasi ili kupunguza matatizo ya usafiri kwa wanafunzi jijini haikupata muitikio mzuri kutoka kwa mashirika na makampuni yaliyoombwa kufanya hivyo.
Inawezekana pengine ni kutokana na kwamba waheshimiwa wenye maamuzi ya mwisho juu ya kuchanga ama kutochanga basi kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi jijini watoto wao wanasoma kwenye shule za binafsi ambako usafiri wa kwenda na kurudi shule ni wa uhakika.
Hata hivyo, inawezekana pia kuwa utaratibu uliowekwa wa kusimamia mabasi hayo kutoka CRDB kwa ajili ya wanafunzi unakatisha tamaa makampuni ma mashirika mengine kuchangia. Nitafafanua.
Baada ya CRDB kutoa mabasi hayo, iliyakabidhi kwa kampuni ya usafirishaji jijini UDA kwa ajili ya kuyapangia utaratibu unaofaa ili kusaidia wanafunzi.
Sina hakika kama ni kutokana na UDA yenyewe kuwa kama jahazi lisilokuwa na nahodha, lakini ukweli ni kwamba mabasi haya hayajasaidia sana wanafunzi wa shule za serikali jijini kama ilivyotegemewa.
Kuna basi moja kwa mfano ambalo mimi mwenyewe nimeshuhudia mara kadhaa likipita kituo cha Mbezi Mwisho kikiwa kimejaa wanafunzi wanaosubiri usafiri na kwenda kuchukua wanafunzi wa shule binafsi moja iliyo maeneo hayo tena sio wote.
Hauhitaji kuwa na intelijensia kama ya wale wenyewe ili kujua kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba shule hiyo ina utaratibu na kitengo cha mabasi hayo kuja kuchukua wanafunzi wa shule hiyo, tena wale waliotoa kiasi fulani cha ziada kwenye ada kwa ajili ya usafiri!
Binafsi nilidhani kuwa mabasi hayo yangekuwa yanatembea barabarani kama mabasi mengine yote lakini yakiwa ni maalumu kwa wanafunzi tu. Sikudhani kama lengo ni kukodishwa na baadhi ya shule za binafsi kwa ajili ya wanafunzi wake kama Inavyoelekea kuwa!
Haiishi kunishangaza kuwa katika jiji hili lenye matatizo makubwa ya usafiri wa wanafunzi sijawahi kuliona basi la CRDB la wanafunzi likisimama kituoni na kugombewa na wanafunzi kwa raha zao bila mpiga debe mmoja kuwataka wapande watano tu!
Pale ninapobahatisha kuliona linakuwa linapita wangu wangu vituo vilivyojaa wanafunzi wanaosubiri usafiri lakini lenyewe linapita juu kwa juu likiwa na wanafunzi waliokaa level seat kama vile basi la shule za binafsi! Hivi ndivyo ilivyotakiwa?
Lakini pia katika kizungumkuti hiki cha UDA kuuzwa ama kutokuuzwa tunapaswa pia kuelezwa wazi , je mabasi hayo kutoka CRDB kwa ajili ya wanafunzi nayo yameingizwa kwenye mkataba kama mali ya UDA na hivyo kuwa sasa mali ya muwekezaji ambaye kama matendo ya wawekezaji wenzake wa nchi hii ni kigezo, tusishangae kesho tukiyaona mabasi hayo yakipiga ruti ndefu za Arusha na Mbeya!
Hili la mabasi yaendayo kasi sitaki hata kulizungumzia; maana nitalazimika kuazima maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuhusu Azimio la Zanzibar kwamba ‘ili kulizungumzia inahitaji kuwa na akili za kiwenda wazimu hivi’!
Yatosha tu kusema kwamba kama kasi inayoonyeshwa katika kujenga miundombinu ya mabasi hayo ya kasi ni kigezo, itakuwa kazi kwa mabasi hayo kuwa ya kasi!
Haya ni sehemu ndogo sana ya matatizo ndani ya sekta yetu ya usafirishaji ambapo badala ya waheshimiwa wetu kutumia nguvu nyingi ili kuyatafutia ufumbuzi wao wanatumia nguvu zao kusukuma magari mapya yasiyokuwa na hitilafu ya waheshimiwa wanaoshukiwa kuingiza staili ya michango ya harusi serikalini!
Haishangazi basi mheshimiwa mmoja kupata jeuri ya kusimama kadamnasini na kutamka kuwa waheshimiwa wenzake wanafikiri kwa kutumia makalio na kwa vile mpaka leo hii hajachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kauli yake hiyo, pengine tukubaliane kwamba kuna ukweli fulani katika kauli yake hiyo?
Wakati namalizia kuandaa makala hii alfajiri ya Jumamosi tayari kwa kuituma kwa mhariri ndipo nilipopata taarifa ya ajali ya meli ya MV Spice Islander wakati ikitoka Zanzibar kwenda Pemba.
Natoa pole zangu za dhati kwa wote waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki na Mungu awape Amani katika kipindi hiki kigumu sana kwao.
Toa maoni yako