Wimbi la mabadiliko

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anaweza kufanya mabadiliko ya uongozi katika Jeshi la Polisi, pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), gazeti hili limeelezwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya gazeti hili, uwezekano huo wa Rais Magufuli kufanya mabadiliko hayo ‘pacha’ unazingatia mambo mbalimbali muhimu kwa taifa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha zaidi kasi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji.

Uwezekano huo unajitokeza ikiwa ni takriban miezi miwili tangu Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu kumteua Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) baada ya kustaafu kwa Jenerali Davis Mwamunyange. Rais Magufuli alimpandisha cheo Venance Mabeyo kutoka Luteni Jenerali hadi Jenerali na kumteua mkuu wa majeshi.

Gazeti hili limeelezwa kwamba kuna uwezekano mkubwa Rais Magufuli akamteua Valentino Mlowola kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi Tanzania na Mkuu wa sasa wa Polisi (IGP) Ernest Mangu akapewa majukumu mengine ya kitaifa kwa kadiri Rais atakavyoona inafaa.

Mlowola anaweza kupata uteuzi huo akitokea Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambako aliingia kwa mara ya kwanza kwa kuteuliwa na Rais Magufuli katika nafasi ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kisha baadaye kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu na hatimaye kuthibitishwa na Rais Magufuli kuwa Mkurugenzi Mkuu, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na mtangulizi wake, Dk. Edward Hosea.

Kabla ya kuteuliwa na kuingia Takukuru, Mlowola alikuwa Kamishna wa Polisi na Mkurugenzi Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi. Pamoja na majukumu mengine mbalimbali ya kitaifa, Mlowola pia amepata kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.

Endapo Rais atamteua Mlowola kushika nafasi ya IGP, nafasi atakayoiacha wazi ya ukurugenzi mkuu wa Takukuru inatajwa kuweza kushikwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa sasa, Zelothe Stephen, ambaye naye amepata kuwa mmoja wa viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi nchini. Zelothe amepata kuwa Mkuu wa Polisi (RPC) Mkoa wa Mtwara na kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma.  Gazeti hili pia limeelezwa uwezekano wa kufanyika mabadiliko katika moja ya idara nyeti nchini katika masuala ya usalama wa nchi.

Raia Mwema limezungumza na mmoja wa makamanda wastaafu wa Jeshi la Polisi ambaye anawafahamu vizuri Zelothe na Mlowola.

Kuhusu Zelothe

Huyu ni askari kwa maana zote za askari. Ana nidhamu, hapendi kuonea watu na hakaribishi upendeleo katika sehemu yoyote anayofanyia kazi. Ni askari wa kweli.

Lakini sifa kubwa kuliko zote ya Zelothe ni ile ya kuchukia rushwa. Kwenye utendaji wake haijawahi kutokea kwamba kuna harufu ya rushwa katika mahali pake pa kazi. Anachukia rushwa.

Ameanzia uaskari katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP) na amepanda vyeo kutokana na umahiri katika utendaji kazi wake.

Yeye ndiye aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kukomesha mauaji ya albino mkoani Mwanza wakati alipopelekwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Ile ilikuwa ni kazi ngumu sana lakini kwa sababu ya weledi wake wa kiaskari, kazi ile ngumu iliweza kufanikiwa na sasa hatusikii tena mambo ya kuua maalbino. Zelothe ni mhitimu wa Shahada ya Sheria.

Kuhusu Mlowola

Huyu ni askari aliyepata mafunzo yake katika Chuo Kikuu cha Polisi Moshi akianzia kazi katika cheo cha chini cha Konstebo wa Polisi.

Alianzia ngazi katika Idara ya Uchunguzi (Forensic) pale Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam ambako alikaa kama miaka minne hivi.

Sifa kubwa ya Mlowola ni kwamba yeye ni askari na kachero mbobezi aliyepata mafunzo ndani na nje ya nchi na rekodi zake zipo hadi katika Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Yeye ameonyesha uwezo mkubwa tangu alipopelekwa Takukuru ambapo ingawa hakuwahi kufanya kazi pale, alishirikiana vizuri na aliowakuta na amesaidia kuweka rekodi nzuri za utendaji.

Katika Jeshi la Polisi kuna mambo mawili ambayo yanamtambulisha. Mosi ni namna alivyoshiriki katika upelelezi wa tukio la kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani hapa nchini mwaka 1998. Walichunguza vizuri na kutoa ripoti ambayo hadi leo inatumiwa na Wamarekani kwenye kuchunguza mambo ya ugaidi.

Pili, yeye aliongoza operesheni ya kumkamata muasi mmoja wa Uganda ambapo alikamatwa na kupelekwa kwao kushitakiwa.

One thought on “Wimbi la mabadiliko”

  1. Hellen says:

    Je taarifa yako hii inamsaidia nini mtanzania? Kuna changamoto nyingi za kuelimisha umma,hususan mazingira, namna ya kuwa wajasiriamali afya nk 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *