- Ni kweli ex Africa simper aliquid novi?
INASHANGAZA kwamba miaka zaidi ya 1,800 tangu yule mwanafalsafa wa kale wa Kiyunani, Ptolemy, atoe ile kauli yake kwamba kila uchwao kitokacho Afrika ni kituko kingine (Ex Africa simper aliquid novi), mambo bado hayajabadilika.
Wiki iliyopita wakati dunia ikiadhimisha sikukuu ya Krismas, ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mfalme wa Amani, Yesu Kristo, wauaji wa Boko Haram walilipua mabomu katika makanisa huko Nigeria na kuua watu 40 waliokuwa kwenye misa ya sikukuu hiyo.
Mauaji hayo katika Afrika, kwa mara nyingine tena, yakapamba vichwa vya habari vya magazeti makubwa kote duniani. Badala ya vyombo vya habari duniani kukita katika maadhimisho ya sikukuu hiyo, vikakita katika mauaji hayo ya kikatili barani Afrika.
Afrika ikawa tena kwenye chati kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, na kama ilivyozoeleka imepanda chati kwa mambo ya ovyo na maovu, na si kwa mambo mazuri na ya neema. Hakika ex Africa simper aliquid novi.
Moyo wangu unaungana na Wanigeria wote waliopoteza ndugu na jamaa zao katika mauaji hayo ya kinyama. Inatia simanzi kwamba Wanigeria wale walikwenda kanisani “kutafuta amani mioyoni mwao” lakini maisha yao duniani yakakatishwa na wauaji hao wa Boko Haram.
Tangu mauaji hayo yatokee, nimekuwa nikijaribu kufikiria nini hasa kilikuwa kinaendelea katika vichwa vya wafuasi hao wa Boko Haram kilichowachochea kufanya si tu mauaji hayo, lakini ndani ya kanisa.
Nauliza hivyo; maana kanisa, kama ulivyo msikiti, ni nyumba za ibada kwa Mwenyezi Mungu, na hivyo ni nyumba za amani. Si mahali pa kuteketeza roho za binadamu wenzako; hata kama binadamu tuna ushetani huo wa kuuana.
Lakini ni vigumu kuelewa nini hasa kiliingia vichwani mwa wafuasi wale wa Boko Haram kufanya mauaji yale kanisani, kama ambavyo ni vigumu kuelewa ni nini hasa kilikuwa kinaendelea ndani ya vichwa vya wale Wahutu waliowafuata Watutsi (tena Wakristo wenzao) kanisani na kuwaua katika mauaji yale ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Hata hivyo, jambo moja ni dhahiri; nalo ni kwamba mauaji ya sampuli hiyo huwa yanatendeka baada ya wauaji kufinyangwa bongo zao kwa muda mrefu na ‘kutekwa’ kabisa akili zao na ‘mabingwa wa ufinyangaji wa bongo za binadamu’.
Wakishafikia ile hatua ya ‘kuiva’ kabisa, basi, huwa tayari kutekeleza lolote watakalotumwa na ‘mabingwa hao wa ufinyangaji’ iwe ni kuwaua watu wa imani nyingine au ndugu zao wenyewe au hata kujiua wenyewe. Haya, dunia imeyashuhudia si tu katika nyanja za imani za dini lakini hata katika masuala ya kisiasa na utawala.
Kwa hakika, dunia imejaa mifano kemkem ya mabingwa hao wa ufinyangaji wa bongo za binadamu wa kila sampuli kuanzia kwa kina Adolph Hitler, David Koresh, Kibwetere hadi kwa kina Osama bin Laden na wengineo.
Kwangu mimi, nawaona watu wa namna hiyo, licha ya vipaji vyao vikubwa vya ushawishi, kuwa ni wendawazimu na wasiostahili kuishi (misfits) katika dunia ya wastaarabu na ya waungwanana na ya wapenda amani na wacha Mungu.
Chukulia, kwa mfano, kiongozi yule wa Boko Haram aliyejitokeza na kujisifu kwa mauaji hayo ya binadamu wenzake waliokuwa wakisali kanisani, Abul Qaqa. Qaqa alitamba kwamba walifanya mauaji hayo ya kikatili kushinikiza wenzao waliokamatwa na polisi waachiwe huru!
Jamani, kuna mantiki hapo kwa mtu anayemwabudu kweli Mungu kufanya hivyo? Unaua watu wasio na hatia ili wauaji wenzako waachiwe huru? Kama unathamini uhuru wa wenzako kiasi hicho, je, roho (maisha) ya binadamu si zaidi ya uhuru huo?
Lakini si hivyo tu, Abul Qaqa alitamba pia kwamba walifanya mauaji hayo ili kushinikiza Shariah itumike kote Nigeria na pia ili kushinikiza katiba na demokrasi visitishwe katika nchi hiyo. Je, huo si uendawazimu mwingine?
Lakini pengine mwendawazimu mkubwa ni mwanzilishi wa Boko Haram (maana yake Kihausa ni “Elimu ya ki-Magharibi ni Haram”), Ustadhi Mohamed Yusuf. Huyu alianzisha kikundi hiki mwaka 2002 ili kuendesha jihad itakayohakikisha Nigeria inatawaliwa kiislamu na kwa kufuata Shariah.
Si hivyo tu, Ustadhi Mohamed na Boko Haram yake inawakataza watoto na vijana wa kiislamu wa Nigeria wasiende kusoma katika shule za serikali au za binafsi zinazofundisha elimu ya ki-Magharibi; akimaanisha elimu hii tunayoijua sote inayotolewa kote duniani.
Je; naye utamwitaje huyu kama si mwendawazimu? Katika dunia hii ya sayansi na teknolojia utahimizaje watu wasipate elimu ya ki-Magharibi? Wasiende sekondari au vyuo vikuu? Yaani anataka watu waendelee kuishi katika zama za giza na ujinga? Hivyo ndivyo kweli uislamu unavyofundisha?
Kwangu mimi, watu wa aina ya Ustadhi Mohamed ni wendawazimu (misfit), na ni wa kufuatilia kwa karibu popote pale wanapochipukia duniani ili wasije kuleta maangamizi ya binadamu wenzao.
Nina hakika kwamba mwaka 2002 wakati Ustadhi Mohamed Yusuf anaanzisha Boko Haram na ajenda yake hiyo, watawala nchini Nigeria walimpuuza kwa kumuona ni punguani tu. Na kweli ni punguani, lakini madhara yanayoweza kuletwa na punguani wa aina hiyo ni makubwa.
Kama tunavyofahamu sote, kikundi cha Boko Haram kilichoasisiwa na Ustadhi Mohamed mpaka sasa kimeshasababisha vifo vya watu 502 katika Nigeria, yakiwemo mauji hayo ya wiki iliyopita kanisani.
Ni dhahiri roho hizo zisingepotea kama watawala wa Nigeria wangekuwa wamemfuatilia na kumdhibiti Ustadhi Mohamed na Boko Haram yake mwaka 2002 alipokiasisi kikundi hicho cha kigaidi.
Kwa hiyo, somo tunalolipata Watanzania kutoka katika mauaji hayo ya wiki iliyopita ya Nigeria ni kwamba; tusiwapuuze kila wanapoibuka misfits katika jamii zetu wanaochochea chuki za kila ‘dizaini’ miongoni mwetu – ziwe ni za kidini, ziwe ni za kikabila, ziwe ni za kisiasa, ziwe ni za rangi.
Tusiwapuuze kwa sababu mwisho wa yote chuki hizo zitasababisha umwagaji damu, na haijalishi kama chuki hizo ni za kidini, kikabila au kisiasa.
Na kwa upande wa watawala wetu, kilichotokea Nigeria wiki iliyopita kinapaswa kuchukuliwa kama kengele ya uamsho. Ni kweli Boko Haram kipo Nigeria na Nigeria ni mbali mno na Tanzania; lakini je; hatuna vikundi vingine katika eneo letu vyenye mwelekeo huo huo wa Boko Haram?
Je, hatuna viongozi wa kidini wenye mitazamo mikali kama Ustadhi Mohamed Yusuf wa Boko Haram? Je, hakuna mazingira katika Tanzania yanayowezesha vikundi vya aina hiyo kuchipuka?
Je, si kweli kwamba tuna redio binafsi za kidini ambazo kutwa nzima huchochea chuki za kidini kama pia yalivyo magazeti yao? Je, si kweli kwamba baadhi ya wahubiri katika nyumba zetu za ibada nao ni mawakala wa kueneza chuki hizo kupitia mahubiri yao?
Tukitafakari kwa undani maswali hayo, tutatambua kwamba nasi katika Tanzania sio salama sana; maana jirani tu na sisi. Lakini hata kama utapuuza hayo, bado hapo Somalia kuna kikundi kinaitwa Al Shabaab (maana yake ni Vijana - The Boys) ambacho nacho kimepania kupigana jihad kuhakikisha nchi za eneo letu zinatawaliwa kiislamu na kufuata Shariah.
Ninachojaribu kueleza hapa, ndugu zangu, ni kwamba tunapitia kipindi kigumu mno duniani na chenye majaribu makubwa yakiwemo ya kidini. Kwa maana hiyo, tunahitaji viongozi imara watakaosimamia umoja wetu wa kitaifa na kuhakikisha kamwe hatubaguani kwa misingi ya dini, rangi, ukabila au siasa.
Jambo muhimu la kukumbuka na kuzingatia ni kwamba ‘mabingwa hawa wa kufinyanga bongo za binadamu’ ambao huwatuma wafuasi wao kuua binadamu wenzao wasio na hatia, hushamiri zaidi katika jamii zilizokumbwa na umasikini mkubwa.
Watu waliokata tamaa ya maisha kwa sababu ya umasikini ndio huwa wafuasi wa mwanzo kabisa wa ghiliba za kina David Koresh, Kibwetere, Osama bin Laden, Ustaz Mohamed na wengine wengi. Hawa huwa ni rahisi sana kuwaghilibu kwa kuwadanganya kuwa matatizo yao chanzo chake ni uislamu au ni ukristo wakati ukweli ni kwamba chanzo ni umasikini na pengine ujinga.
Historia inatukumbusha kwamba wakati muuaji Hitler anaibuka katika siasa za Ujerumani, nchi hiyo ilikuwa imekumbwa na hali ngumu ya maisha iliyosababisha umasikini mkubwa. Hitler akawaongopea Wajerumani kwamba chanzo kikubwa cha umasikini wao ni Wayahudi. Kilichotokea baada ya ‘sumu’ hiyo ya uongo kumwagwa na Hitler wengi miongoni mwetu tunakijua – Wayahudi karibu milioni tano waliuawa na wafuasi hao wa Hitler.
Kwa hiyo, njia kubwa ya Tanzania kujihami ili mabingwa hawa wa kufinyanga bongo za binadamu wasiibuke nchini mwetu au wakiibuka wasipate wafuasi, ni kuhakikisha tunaupiga vita umasikini na kutenda haki katika kila ngazi.
Na ukizingatia hali ilivyo hivi sasa nchini mwetu ya ukosefu wa ajira kwa vijana wetu (majuzi Zitto Kabwe alizingirwa na vijana 400 jimboni mwake wakimlalamikia ukosefu wa ajira), hatuwezi kujidai kwamba tuko salama.
Na kwa hali ilivyo hivi sasa, tatizo kubwa sio udini; bali ni ukosefu wa ajira. Ukosefu huu mkubwa wa ajira ndio unaoweza kuzalisha matatizo mengine kadhaa likiwemo tatizo la udini ambalo ni la hatari zaidi.
Ndio maana, pamoja na upungufu wake wote, Edward Lowassa, amekuwa mkweli kwa kusema kwamba tatizo la ajira katika Tanzania ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote; hata kama hakuyasema maneno hayo alipokuwa waziri mkuu.
Ndugu zangu, ni kweli kwamba kila kukicha kiibukacho Afrika ni kituko kingine (ex africa simper aliquid novi), lakini Watanzania tuna wajibu wa kuiepusha nchi yetu kuwa kituko kingine cha Afrika kwa kudhibiti mazingira yanayoweza kusababisha umwagaji damu.
Na kwa sasa, ukosefu wa ajira ni tatizo namba moja na hivyo tuwabane watawala wetu walishughulikie tatizo hili, na kama hawawezi; wawapishe wengine wanaoweza.
Tafakari.
Maoni ya Wasomaji
TUNAPOYATAZAMA MAMBO HAYA
TUNAPOYATAZAMA MAMBO HAYA TUJARIBU KUTUMIA MACHO YOTE NA AKILI YOTE BADALA YA KUWA NI NDUMILAKUWILI {DOUBLE STANDARDS} KATIKA KUANDIKA/KUZUNGUMZA. WANAPOULIWA WAISLAMU DUNIANI HUWA SI HABARI BALI WANAPOULIWA WENGINEO HUWA NDIYO HABARI. SITETEI MAUAJI YOYOTE BALI NINASIKITISHWA NA UPOGO WA UONI PINDI WANAPOULIWA WAISLAMU. TANGU MWAKA 2003 HADI 2011 WAISLAMU AMBAO NDIYO WENGI MIONGONI MWA RAIA WA IRAQ WALIKUWA WANAULIWA KILA SIKU UCHAO NA UCHWAO LAKINI NI WACHACHE SANA WALIOWAHURUMIA WAIRAQ WALE.JE WAKRISTO WA NIGERIA WANA MIILI YA DHAHABU?? NA WAISLAMU WA IRAQ NA AFGHANISTAN WANA MIILI YA MITI?? HADI LEO HAKUNA USHAHIDI WOWOTE WA KUWEPO SILAHA ZA MAANGAMIZI NCHINI IRAQ AMBACHO NDO KILIKUWA KIGEZO KIKUBWA CHA MAUAJI YA WAISLAMU WA IRAQ, WAANDISHI MBONA MLIKAA KIMYAAAA??
Ni kukoswa tu uelewa na mang
Ni kukoswa tu uelewa na mang'amuzi. Hata kubishana na watu wa namna hii ni kupoteza muda kwani hawafundishiki. Wanaongozwa na jaziba zisizokuwa na msingi!
Watu kama wewe ndugu GWOTTA
Watu kama wewe ndugu GWOTTA ndio mnaoturudisha watanzania nyuma. Kwanini kila kila unakitafsiri kwa lensi ya usilamu na ukristo? KWanini usiseme so and so kakosea hata kama akiwa wa dini yako? Watu kama nyie ndio mnaochekelea Kikwete akiendelea kuimaliza nchi na mkiulizwa mnasema anapingwa kwasababu ni muislamu. Hivi anapojineemesha yeye, familia yake na mafisadi wengine huwa anausaidia vipi uisilamu? Kwanza hata kwa kanuni za uisilamu mufti nae yumo? Acheni kufikiria kwa kutumia makalio jamani.