MAJUZI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangaza kwamba serikali imeamua kuikopesha Kampuni ya Serikali ya Kusimamia Mali za Reli (RAHCO), kwa ajili ya kulipa mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ambao walianza mgomo wiki iliyopita na kuathiri usafiri wa reli.
Waziri Mkuu alisema kwamba serikali itatoa fedha hizo ili kuwawezesha wafanyakazi kulipwa kiwango kipya cha mishahara, cha Sh. 160,000 badala ya kile cha Sh. 87,000.
Hatua hiyo inakuja baada ya wawekezaji wa TRL kutangaza kwamba hawana fedha za kulipa viwango vipya vya mishahara ya wafanyakazi hao, jambo ambalo lilisababisha wafanyakazi wa kampuni hiyo kuanza mgomo Alhamisi iliyopita, ili kushinikiza walipwe mishahara mipya.
Wakati hayo yakitokea katika kampuni ya TRL, wiki takribani moja iliyopita, serikali hiyo hiyo, kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Stephen Wassira, ilitangaza kuwalipa kifuta machozi cha Sh. bilioni 1.7 wakazi wa Tabata Dampo, Dar es Salaam, kufuatia ubomoaji haramu wa nyumba 88, uliofanywa na Manispaa ya Ilala.
Kutokana na uzembe huo, sasa serikali italazimika kulipa Sh. milioni 20 kwa kila nyumba iliyobomolewa na kutoa viwanja bure eneo la Buyuni, Wilaya ya Ilala, kwa kila mkazi aliyebomolewa nyumba yake.
Tukiangalia tukio hilo la TRL tunabaini kuwa ni kiwakilishi kingine cha mikataba mibovu, kutokuwajali wananchi na maslahi ya taifa, uzembe na ukosefu wa umakini katika kufanya kazi na kutoa maamuzi.
Hata tukio la ubomoaji wa Tabata Dampo linaonyesha udhaifu huo huo, jambo ambalo, sisi tunaona ni kutokuzingatia haki za msingi, ni la kusikitisha na kuwakatisha tamaa wananchi.
Kwa mtazamo wetu, tunaona kwamba serikali inapaswa kuchukua hatua kali zaidi kwa wahusika ambao wanashiriki katika kuingia mikataba mibovu, isiyozingatia maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Inafaa watu wanaoiingiza serikali katika kutoa fedha nyingi za walipa kodi, kwa ajili ya kugharamia matukio ya uzembe na ukosefu wa umakini, wachukuliwe hatua kali zaidi ili kujenga uadilifu.
Vinginevyo, taifa litaendelea kupoteza mabilioni katika mambo ambayo yanaweza kuepukika. Yaliyotokea TRL na Tabata Dampo yanapaswa kuwa funzo kwa wote na ikiwezekana serikali ipunguze huruma dhidi ya uzembe na ukosefu wa umakini.
Toa maoni yako