KUNA kila dalili kwamba Yanga itaanza vibaya mwaka mpya ulioko mbele yetu. Lakini hiyo itakuwa ni kwenda kinyume na kauli mbiu yake inayosema Yanga imara. Kwa kweli Yanga si imara sijui tuseme itakuwa ni ‘Yanga mdebwedo?’
Kocha wa klabu hiyo, Kostadian Papic, juzi Jumatatu alipasua jipu. Usaha uliotoka ulikuwa wa kukatisha tamaa. Ulionyesha kwamba hakuna la maana linalofanyika katika klabu hiyo katika kipindi hiki muhimu ambacho wachezaji wa klabu hiyo walipaswa kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya mechi ngumu dhidi ya Zamalek ya Misri.
Katika mchezo wa ndondi, kocha anapoona bondia wake amezidiwa na anaendelea kuteswa na mpinzani wake, anaruhusiwa kutupa taulo ndani ya ulingo kuashiria kwamba pambano lisimamishwe na mwamuzi anayechezesha ili bondia wake asipate madhara zaidi.
Katika mpira wa miguu hakuna kutupa taulo. Kuna kle kinachoitwa na watoto wa mjini, kuingia mitini kwa kuzua visingizo na hiyo inatokea timu inapokuwa inazidiwa. Mambo yakizidi kuwa mabaya na juu yake ikatokea na penalti dhidi yao, kocha au nahodha anatoa wachezaji nje akisingizia mwamuzi anawaonea.
Au timu inajitoa mapema ikiona kwamba itakuwa inafanya kazi ya bure kucheza na mpinzani wake katika pambano lililopangwa kucheza. Hivyo mpinzani hupata ushindi wa chee na kusonga mbele katika mashindano husika.
Lakini tatizo ni kwamba uamuzi wowote utakaochukuliwa kati ya hayo maamuzi mawili, yanakuwa na gharama yake. Waandalizi wa mashindano husika huchukua hatua ya kuilima faini timu iliyoingia mitini ama kujitoa kwa sababu ambazo hazina mashiko.
Sababu zinazokubalika ni zile ambazo kweli ziko nje ya uwezo wa timu kama vile kufikwa na janga la kidunia kama la kufiwa na wachezaji kadhaa au nchi inayotoka timu hiyo kuwa vitani lakini si kwa vile timu imekosa nauli au haikufanya maandalizi vizuri kama Yanga ilivyojikuta hivi sasa.
Papic amesema wazi kwamba hatarajii timu kufanya vizuri katika mechi hiyo dhidi ya Zamalek kwa vile hapati ushirikiano wowote kutoka kwenye uongozi wa klabu hiyo. Licha ya yeye binafsi kutolipwa mshahara na nyumba anayoishi kukatiwa umeme na maji kwa sababu ya madeni, hata wachezaji hawajalipwa mishahara yao.
Kibaya zaidi wachezaji hawajafanya mazoezi si ya uwanjani wala ya viungo kwenye gym na siku za kueleka kwenye mchezo huo zikiwa zinasogea taratibu. Kwa maelezo yake, ni kama amesusiwa wachezaji hao na yeye hajui afanye nini.
Alisema aliomba timu icheze mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya timu za hapa nyumbani na za nje katika maandalizi yake, lakini hakujibiwa lolote na uongozi na wala hakuna dalili kwamba timu itacheza mchezo wowote wa kujipima nguvu kutokana na kimya kilichopo kutoka upande wa uongozi.
Ajabu nyingine ya Yanga ni kwamba pamoja na timu ya klabu hiyo kuorodheshwa kushiriki kwenye michuano ya Mapinduzi ambayo kilele chake ni Januari 12 mwakani, Papic hana habari za michuano hiyo kwa sababu uongozi wa Yanga haujamfahamisha lolote kuhusu timu yao kushiriki kwenye michuano hiyo..
Lakini tatizo liko wapi? Yanga haina uongozi? Gazeti hili ilijaribu kuwasiliana na mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga kuhusiana na suala hilo bila ya mafanikio yoyote. Namba mbili za simu za kiongozi huyo zilikuwa hazipatikani hadi gazeti hili linakwenda mtamboni.
Je, kwa angalizo alilolitoa Papic, Yanga icheze na Zamalek isicheze? Kocha ameshainua mikono, morali ya wachezaji iko chini, kuna uhalali wa kupoteza fedha nyingi kusafiri hadi Cairo kucheza mchezo dhidi ya Zamalek uliopangwa kufanyika kati ya Februari 17 na 19?
Hatari iliyopo mbele ni kwamba ‘jeshi’ hili lililokata tamaa linaweza likatupatia aibu ya mwaka! Nani asiyezijua timu za Misri? Kama huko nyuma pamoja na kufanya maandalizi yanayoridhisha timu zetu zilikuwa zinapigwa hata mabao matano, safari hii Yanga inaweza ikapigwa mabao mangapi?
Ni bora basi kupiga mahesabu ya faini itakayotozwa na gharama ya kwenda Cairo na kurudi na gharama ya aibu ambayo Yanga Itaingia huko kuona ni kipi kitakuwa nafuu. Mahesabu hayo ndiyo yatuongoze juu ya suala la kwenda au ‘kukacha’ kwenda Misri.
Kwa kweli hali ikiendelea kuwa hivi ya maamandali ya kubahatisha, ni bsara kujitoa lakini kama kuanzia sasa timu itajifua kweli kweli baada ya uongozi kujitoa kutoka huko walikojificha, basi timu iende huko Cairo. Vingenevyo kujitoa ni muhimu.
Yanga kwa mara nyingine imejikuta katika hali hii licha ya ukongwe wake, utajiri wake unaokaliwa tu na uzoefu wake wa miaka chungu mbovu wa kushiriki michuano ya kimataifa.
Imejikuta katika hali hiyo kutokana na msemo ule wa ‘ndege mjanja hunaswa katika tundu bovu.’ Hakuna maelezo mengine mbali ya ukweli kwamba inakwama kwa sababu ya kutegemea ‘ufadhili’ wa mtu mmoja wa kikundi fulani cha watu.
Hali hiyo si endelevu. Laiti kama mapato ya Yanga yangetokana na rasilimali zake, mapato ya mlangoni ambayo kila senti inayoingia inaingizwa kitabuni na inapotoka inaonekana kitabuni kwamba imetolewa kwa shughuli gani iliyoidhinsihwa, hali hii ya sasa ingekuwa ni historia. Yanga yahitaji kubadilika.
Toa maoni yako