Michezo
Yanga na Simba: Bado ni yale yale ya miaka nenda rudi
Chesi Mpilipili
Toleo la 177
16 Mar 2011

TUMESIKIA, kuona na kuambiwa kuhusu yote yanayopaswa kusikiwa, kuonwa na kuambiwa kuhusu mpambano wa watani wa jadi wa Yanga na Simba uliofanyika  Jumamosi ya Machi 5 mwaka huu.

Katika pambano hilo ambalo watani hao wa jadi walitoka sare kwa kufungana bao 1-1, wengi wa waandishi wetu wa habari za michezo nchini wamejibainisha juu ya timu wanazoshabikia kupitia kwa jinsi walivyoripoti mechi hiyo.

Wakati mwandishi mmoja akisema kuwa tuta walilopewa Yanga halikustahili kwa vile faulo ilifanyika nje ya 18, mwingine hakuoliona hilo na akaishia kutueleza tu kuwa Yanga walipata penalti dakika ya 54 baada ya mshambuliaji wake kuangushwa ndani ya eneo la hatari la Simba, basi!

Tumesoma pia kuwa mchezaji wa Simba aliyepiga kichwa mpira uliokwenda kugonga mwamba na kuingia golini alikuwa ameotea kama vile tulivyosikia kwa mtangazaji mmoja wa redio kuwa mpira ule ulikuwa umegonga mstari wa goli na sio ndani ya goli.

Tunashukuru kwamba marudio ya picha za televisheni yalionyesha wazi kabisa kuwa mpira ule ulikuwa umegonga ndani ya goli la Yanga na sio kwenye mstari!

Hakika zingekuwa zile enzi ambapo tulikuwa tukitegemea mtangazaji wa redio tu pekee ndio atuhabarishe kinachoendelea uwanjani, basi tungekuwa tumeliwa!

Tumesoma maelezo yanayoonyesha kuwa mechi ile ilikuwa iwe sare ya kutofungana mabao kama sio refa wa mchezo huo mwenye beji ya FIFA, Oden Mbaga kuamua kuipa kila timu bao moja la zawadi kwa makosa ya kufikirika na hivyo matokeo ya mwisho kuwa sare ya bao 1-1.

Mtanange ule umemalizika na tukafahamishwa juu ya mapato yaliyopatikana. Sh. milioni 243 katika kipindi cha dakika 90 tu kwa maana ya kwamba kila dakika moja ya mchezo ule ilikuwa karibuni Sh. Milioni mbili na laki saba!

Makampuni mengi ya biashara sio hapa nchini tu bali ulimwengu mzima yangeshukuru sana kuwa na biashara inayoingiza faida ya Sh. milioni mbili na laki saba kwa dakika!

Tumeelezwa pia kuwa wazalishaji wakuu katika ‘biashara’ hiyo, yaani timu za Yanga na Simba, zimejipatia jumla ya Sh. milioni 102i, kwa maana ya kila timu ikiambulia tu milioni 51,194,793/=  kati ya milioni 243,000,000/= zilizokusanywa!

Tunaweza tukasema mengi sana kuhusu hili, kama ambavyo tumekwisha kusema mara nyingi huko nyuma.

Tuishie tu kusisitiza kuwa ili timu mbili hizi kubwa ziweze kuondokana na ‘zulumati’ hii ya kusikitisha, zile ‘kelele’ za kila siku za kujenga na kumiliki viwanja vyao wenyewe zisiishie kwenye kurasa za michezo za magazeti na kwenye shubaka za meza za viongozi.

Waama, zisigeuzwe pia kuwa taarifa za kila mara za viongozi wa klabu hizo kujiongezea ujiko kila pale wanapohisi umaarufu wao miongoni mwa wanachama na wapenzi wa klabu husika umeshuka.

Kauli za timu zetu hizi kubwa za kujenga na kumiliki viwanja vyao wenyewe hazipaswi kuishia kuwa ile hadithi ya nyani kuahidiana kujenga nyumba kesho kila baada ya kunyeshewa na mvua. Naam, ‘mvua’ kama hii ya kuambulia tumilioni hamsini na moja tu kati ya milioni 243 walizotengeneza katika muda wa dakika tisini tu.

Aghalabu, baada ya mchezo mkubwa ule kuna maswali kadhaa ambayo viongozi, wanachama, wapenzi wa vilabu hivyo vikubwa vya soka nchini na wadau wa mchezo wa soka tunapaswa kujiuliza.

Je, timu zetu hizi mbili kubwa za soka nchini zimecheza soka ya kiwango kinachostahili majina yao makubwa?

Je, timu zetu hizi zimeweza kucheza pasi kumi hadi 15 bila kupoteza mpira kwa adui na kutengeneza nafasi za mabao na kuzitumia bila kuepuka kutegemea mabao ya zawadi kutoka kwa waamuzi?

Je, wachezaji wa nyumbani wa klabu zetu hizo mbili kubwa ambao kwa asilimia kubwa ndio wachezaji wetu wa timu za taifa wameonyesha kiwango kinachostahili sifa tunazowapa?

Je, mchezo huo ulikuwa mgumu sana na ngome za timu hizo kuwa ngumu mno kufunguka kiasi cha timu hizo kusubiri ‘huruma’ ya mwamuzi Oden Mbaga ‘kuzizawadia’ ba moja moja kila timu ili angalau ubao wa matangazo angalau usomeke Simba 1 Yanga 1?

Baadhi ya waandishi wetu wa habari za michezo wametuambia kuwa wachezaji walishindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na tension ya mchezo huo. Haya ni maneno ambayo tumekuwa tukiyasikia mara kwa mara kutoka kwa waandishi wa habari kila baada ya mchezo unaozikutanisha klabu hizo.

Kwa hakika, tunaaminishwa katika kuwasamehe wachezaji wa timu hizo wanaposhindwa kufanya vitu tunavyotatarajia kutoka kwao katika mchezo unaozihusu timu hizo mbili kubwa kutokana na hiyo tension ya big game lao!

Idadi kubwa ya wachezaji waliokutana kwenye mchezo wa Jumamosi si tu kwamba walikuwapo pia kwenye mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Kirumba, Mwanza  na Yanga kushinda kwa bao 1-0 bali wamekuwapo kwa misimu mitatu hadi minne ya nyuma na wameshiriki katika big match zinazokutanisha timu hizo. Hivyo hicho kinachoitwa tension kinatoka wapi?

Saa 24 baada ya big match inayozikutanisha timu zetu kubwa hapa nchini, kule Uingereza kulikuwa na big match nyingine inayozihusu timu kubwa katika ligi ya Barclays ya Uingereza za Liverpool na Manchester na Liverpool kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1.

Tuliona wachezaji na timu zao wakicheza mchezo wao wa siku zote sana sana sasa ukiwa na msisitizo na msisimko mkubwa zaidi kutokana na ukubwa wa mechi hiyo.

Kilichokuwa wazi ni kuwa hakuna mchezaji aliyeshindwa kuonyesha kiwango chake cha soka tulichomzoea kumuona nacho kwa kile kinachoitwa tension ya mchezo mkubwa.

Tunapojiaminisha kuwa ni sawa kwa wachezaji wetu kushindwa kuonyesha kiwango chao cha juu cha soka tunachokitatarajia kutoka kwao kwa kisingizio cha tension ya big match baina yao na watani wao wa jadi wa miaka nenda rudi, tutarajia nini kwa mfano pale wanapokutana na klabu bingwa ya Afrika?

Iwapo tunajiamisha kuwa ni sawa kwa wachezaji wetu kucheza chini ya kiwango tunachotarajia kutoka kwao kwa kisingizio cha tension ya big match dhidi ya timu pinzani yenye wachezaji wanaokutana nao kila siku mitaani, tutarajie nini pale wanapokutana na wachezaji pinzani wasiowajua wanaochezea klabu bingwa ya tatu ya dunia?

Ni vizuri iwapo wachezaji wa timu ya Simba wakaandaliwa pia kisaikolojia ili kuhakikisha kuwa kiitwacho tension ya big match inaishia pale wanapokumbana na watani wao wa jadi tu na sio watakapokutana na klabu bingwa ya tatu ya dunia, TP Mazembe ya Congo.

Waandaliwe kisaikolojia ili kuhakikisha kuwa katika suala la tension ya big match waione mechi yao na TP Mazembe kama vile wanavyoiona mechi baina yao na Toto Afrika, Majimaji na AFC ili wasishindwe kucheza kwa kiwango chao cha  juu kutokana na tension ya big match kama wanayokuwa nayo wanapokutana na Yanga!

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako