Michezo
Yanga na Simba nani kucheka Jumamosi?
Chesi Mpilipili
Toleo la 209
26 Oct 2011

Njia zote zitaelekea kwenye Uwanja wetu wa kisasa wa Taifa mjini Dar es Salaam Jumamosi hii ya Oktoba 29 wakati watani wa jadi wa soka letu watakapokutana kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

Timu hizo zitaingia kwenye mchezo huo zikifukuzana kwenye msimamo wa Ligi huku Simba ikiongoza Ligi hio kwa pointi 27 na Yanga ikishika nafasi ya pili kwa pointi zake 21.

Yanga pia itaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 2-0 ilichokipata kutoka kwa mpinzani wake kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani wa kufungua msimu wa Ligi Kuu Agosti mwaka huu.

Swali kubwa wanalojiuliza wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hizi mbili kubwa nchini kuanzia pale filimbi za kumaliza michezo yao ya mwisho zilipolia ni juu ya nani atakayetoka uwanja wa taifa akichekelea huku basi la wachezaji wake likisukumwa na mashabiki wa klabu kwa furaha.

Swali la nani atashinda mchezo wa Jumamosi linakwenda sambamba na swali lingine ambalo japo haliulizwi wazi lakini ni muhimu sana.

Swali hilo ni lile linalohusu ni timu ipi ambayo itafungwa na hivyo kuashiria mwanzo wa vuta nikuvute na migogoro ya chini chini miongoni mwa viongozi walioko madarakani na wale wanaotaka kuingia kwa njia za panya.

Sio siri kwamba pambano baina ya Yanga na Simba ndio hutengeneza ama kuharibu uongozi wa klabu. Kwa timu zetu hizi, uwezo wa kiongozi hukubalika pale tu anapoweza kumfunga mtani wa jadi na sio vinginevyo.

Kiongozi aliye madarakani wa timu hizi kubwa anaweza kusamehewa iwapo timu itafungwa 3-0 hata na Villa Squad ya Magomeni inayocheza mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom lakini kamwe hatasamehewa iwapo timu itafungwa bao 1-0 na mtani wa jadi.

Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari viliandika habari kuhusu kurejea tena kwa mfadhili mkuu wa Yanga mwenye hadithi ya ya kutoka na kurejea klabuni hapo, Yussuf Manji. Alipokewa na viongozi wa Yanga akitokea kwenye shughuli zake za kibiashara ughaibuni.

Imeelezwa kuwa mara tu baada ya kupokewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, mfadhili huyo alipelekwa moja kwa moja kwenye Uwanja wa timu hiyo wa Kaunda na kwa mara nyingine tena kutoa ahadi ya kuufanyia ukarabati mkubwa.

Zaidi ya hilo, Yussuf Manji alinukuliwa akiwataka viongozi wa Yanga kuanza mkakati wa kuhakikisha kuwa Yanga inaifunga Simba katika mchezo wao wa Jumamosi hii.

Wakati akipanga mkakati huo, Yanga ilikuwa inakabiliwa na mchezo mgumu kati yake na JKT Oljoro lakini inaonyesha kuwa mfadhili huyo na uongozi wa Yanga ulikuwa hautilii sana maanani mchezo huo na badala yake nguvu na mikakati yote ilikuwa imeelekezwa kwenye mchezo baina yake na Simba.

Miezi michache kabla ya hapo, Tanzania ilipokea ugeni wa promota mmoja wa mambo ya soka kutoka Afrika Kusini ambaye alikuwa anataka kuandaa mashindano baina ya klabu za soka za Afrika Kusini na zile za Yanga na Simba hapa nchini.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari promota huyo alifafanua vizuri mikakati yake ya kuinua soka ukanda huu kupitia michuano hiyo ambayo hatujasikia tena kinachoendelea. Ilipofika zamu ya kiongozi wa Simba aliishia kusema jinsi michuano hiyo itakavyotoa nafasi kwa timu yake kuifunga tena Yanga!

Hii ni mifano michache tu ya jinsi mchezo baina ya timu hizo mbili kubwa nchini unavyovuta hisia za sio tu wapenzi wa timu hizo bali pia Watanzania wote kwa ujumla.

Kimichezo, timu zote mbili hazitofautiani sana ingawaje Simba inaonekana kuwa juu kuliko Yanga hasa ikichukuliwa kwamba raundi chache tu zilizopita Yanga ilikuwa inanusa nusa kwenye nafasi za chini kabisa za msimamo wa Ligi hiyo huku mwenzake Simba akipepea kwenye nafasi za juu.

Hata hivyo, Yanga inaonekana kuwa imejirekebisha na hivyo kurudi kwenye nafasi iliyozoeleka ya kufukuzana na mtani wake wa jadi kugombea nafasi za juu kwenye Ligi hiyo.

Kubwa zaidi ni kuwa timu hizi mbili zinapokutana, nafasi iliyonayo timu moja kwenye msimamo wa ligi huwa haina mchango mkubwa katika matokeo ya mwisho ya mchezo.

Timu inayofanya vizuri na yenye utulivu klabuni inaweza ikajikuta inachabangwa na timu ambayo inafanya vibaya kwenye msimamo wa Ligi na ambayo ina mgogoro wa viongozi na ushindi wao kuhamishia mgogoro huo kwa wapinzani wao!

Mechi ya Jumamosi inaongezwa msisimko zaidi kutokana na ushindi wa timu hizo kwenye mechi zao za mwisho mwishoni mwa wiki iliyopita kabla ya mpambano wao ambapo Simba iliwashinda JKT Ruvu mabao 2-0 na Yanga kuishinda JKT Oljoro kwa bao 1-0.

Mashabiki wa Simba wanaonekana kujiamini zaidi kutokana na safu yao ya mashambulizi yenye wachezaji, Uhuru Selemani, Emmanuel Okwi wa Uganda, Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu wa Zambia na Ulimboka na Mwakingwe.

Yanga itawategemea zaidi washambuliaji wao wageni kama Hamis Kiiza, Kenneth Asamoah, Haruna Niyonzima watakaoshirikiana na akina Oscar Joshua na Jerry Tegete ambao kasi yao ndogo ya kufunga mabao mwanzoni mwa Ligi kulisabisha Yanga kutocheza mbali na mkia wa Ligi hiyo hadi pale walipozinduka na kuanza kufanya vitu vilivyotegemewa kutoka kwao na kumfanya mwajiri wao kujikita nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi.

Pamoja na majina haya makubwa ya wachezaji hawa, sio lazima sana kwamba mwisho wa siku watazamaji watakaomiminika kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi watashuhudia mchezo wa kusisimua unaostahili kiingilio watakachokuwa wamekamuliwa kwa ajili ya kuuona mchezo huo.

Kutokana na wasiwasi, presha na kukamiana kunakoambatana na mchezo huo, wachezaji hushindwa ama kuogopa hata kuwa ‘watundu’ na wabunifu na kuishia kucheza kioga oga kama maroboti, kila mtu akiogopa kutenda kosa na kusababisha timu yake kufungwa na hivyo kuwa adui nambari moja wa klabu hiyo.

Kutokana na haya, michezo inayozihusu timu kubwa hizi huishia kuwa iliyopooza na isiyokuwa na ustadi ama msisimko wowote unaonendana na sifa na ukubwa wa majina wa timu hizo.

Ni matumaini yetu kwamba kocha aliyerejea Yanga, Kostadin Papic na wa Simba, Moses Basena wa Simba bila kuhofia ajira zao, wataruhusu wachezaji wao kuwa huru kufanya kile wanachoona kuwa ni sawa kiwanjani na pia kuruhusu timu kucheza mchezo wa kushambulia badala ya kujihami, kila mtu kuanzia viongozi, kocha hadi wachezaji akiogopa bakora!

Ni kwa mchezo wa kushambuliana tu ndipo pengine, pengine tunaweza kushuhudia mtu akiraruriwa bao Nane ama Sita kwa moja kama zifanyavyo zile timu tunazoshabikia kwenye ligi yao huko Uingereza!

Tumalizie kwa kuwaomba watanzania watakapoingia kwenye mechi hiyo kila mmoja kuwa walinzi shirikishi kwa kila mmoja kuwa Mlinzi wa mwenziwe ili kuhakikisha kuwa hakuna wahuni wachache wanaofanya uharibifu kwenye Uwanja wetu huo wa Kisasa.

Yote kwa yote, tuzitakie Simba na Yanga mchezo mwema na amani bila baadhi ya wanachama kutaka kuingia msituni pale itakapotokea timu moja kushindiliwa bao 6-1!

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.