WAINGEREZA wana msemo usemao A still tongue makes a wise head. Kwa tafsiri ya moja kwa moja msemo huu una maana kuwa ulimi uliotulia unatengeneza kichwa chenye busara.
Maudhui ya msemo huo yanafanana kwa kiasi kikubwa na yale ya msemo wa Kiswahili: "Heri kujikwaa dole kuliko kujikwaa ulimi". Kwa ujumla misemo hiyo inazungumzia matokeo mabaya yanayoweza kusababishwa na kauli zinazotolewa kuhusu hilo linalozungumzwa.
Tangu litokee sakata la Yanga kuikacha Simba kwenye mashindano ya Kombe la Kagame, mwaka huu, watu ambao wamelizungumza sana suala hilo ni watu wanaoihusu klabu ya Yanga. Wamefanya hivyo katika hatua zote za sakata hilo - lilipotokea, adhabu ilipotolewa, rufani ilipokatwa, uamuzi wa rufani ulipotolewa na Kamati ya Nidhamu ya TFF mpaka ilipotolewa kauli kwamba uamuzi huo wa Kamati ya Rufani utafikishwa tena kwenye Kamati ya Utendaji ya TFF iliyoiadhibu Yanga baada ya kuadhibiwa na CECAFA.
Katika kauli hizo za mashabiki wa Yanga, kuna zenye mantiki; hata kama baadhi zimekosewa au zimekuwa tata, lakini pia kuna kauli za kejeli na za kuchochea uhasama.
Siungi mkono kauli zinazoonyesha kwamba Yanga ni timu tajiri sana kuliko zote kwenye ukanda huu; hivyo isingeweza kususia mechi kwa pesa ndogo.
Cha kusikitisha, kauli kama hiyo pia hutolewa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kubwa ambao ni wasomi. Hutoa kauli zisizolingana na hadhi yao na hadhi ya klabu wanayoiongoza.
Ni wazi kwamba mwenendo huu wa wa viongozi na mashabiki wa Yanga unakera. Siioni kabisa busara ya wao kutamba sana kwamba lazima watashinda kesi hii kwa sababu kama wana uhakika na hilo kutokana na mikakati waliyojiwekea, mambo yao yanapaswa kwenda chini chini tu hadi hapo tutakapotangaziwa matokeo ya mwisho.
Kutamba huku kunawafanya wapinzani wao katika kesi hiyo nao wajiimarishe; kwani watajiona sasa wako vitani kabisa kabisa. Wakijiimarisha, kitakachotamba katika kesi hii ni fitna zaidi kuliko chochote cha maana.
Wanachopaswa kufanya viongozi wa Yanga na watu wengine wanaoitakia mema klabu hiyo ni kuwa watulivu, wanyenyekevu na kuwa na mahusiano ya kirafiki na viongozi wa TFF. Zaidi ya hayo yote, si vibaya wakiomba radhi kwa Rais wa TFF na CECAFA, Leodgar Tenga kwa yote yaliyotokea tangu waache kupeleka timu uwanjani na kauli kali zilizotolewa na watu wanaoihusu klabu hiyo baada ya TFF kutoa adhabu ya pili kwa klabu hiyo.
Waombe hayo yaishe, wacheze mpira. Wakifanya hivyo, viongozi hao wa Yanga hawalazimishwi kututangazia kwamba wamefanya hivyo. Wanaweza kutujulisha, wakipenda.
Tunapaswa tuelezane ukweli kwamba katika sakata hili,Yanga inapaswa kuwa nyenyekevu kwa sababu iko upande wa hatari, upande uliokosea.Haipaswi hata kidogo kuonyesha ina nguvu sana kuwazidi wale ambao hawakukosea kama TFF.
Wao ndiyo walikosea, hivyo wanapaswa kuwa watulivu na kuhakikisha hautokei uchochezi wowote baina yao na TFF. Wawe makini sana na kauli zao zinazoweza kuwapandisha mori wanachama na mashabiki wao, wakiwemo baadhi ya waandishi na wachambuzi wa michezo, ambao wengi hawana muda wa kutafakari mambo wanapoaminishwa klabu yao imeonewa!
Ndiyo maana uongozi wa Yanga ulipokuja na ile kauli ya adhabu mbili kwa kosa moja, waliidaka na kuiimba kwa sauti kubwa Tanzania nzima wakati adhabu ya pili ilipobaki, lakini ikiwa faini ya dola 20,000, uongozi ulipoishangilia, hakuna aliyehoji tena kuendelea kuwepo kwa adhabu hiyo ya pili; bali wote walijiunga kushangilia ushindi!
Nimetoa ushauri huu kwa Yanga baada ya kuona suala hili linarudishwa kwa Kamati ya Utendaji ya TFF ambayo, naamini, inaweza kuamua chochote kwa hasara ya Yanga si kwa kuzingatia kanuni na hali halisi ya mlolongo wa matukio yahusuyo suala hilo bali kwa kuonyeshana ubabe kati yao na "Yanga tajiri"!
Kama Yanga wakifuata ushauri wangu, hata baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF nao wakikomaa, wajumbe wenzao watawaambia "jamani huu sasa si uana michezo, angalia jinsi Yanga walivyokuwa na nidhamu, ona jinsi walivyoomba radhi na kujutia kosa lao. Kwa sababu Kamati ya Nidhamu imeichambua vizuri kesi hiyo, turidhike na maamuzi yake na tuyafanye kupitia kikao hiki kuwa ndiyo maamuzi yetu baada ya kuitafakari kwa kina kesi hii.Sasa tuachane na suala hili, tuangalie masuala mengine ya muhimu ya kuendeleza soka letu".
Vile vile, naomba kuushauri uongozi wa Yanga kuwa makini na baadhi ya magazeti yanayoandika habari za michezo yanayotumia uzito wa habari hii ya sakata lao kufanya biashara kwa kuandika habari potofu kwa lengo la kuuza. Acha waandike siku mbili baada ya Yanga kuadhibiwa kwamba rufani yao (ya Yanga) ilishatua kwenye Mahakama ya Michezo(CAS) wakati mpaka naandika haya uongozi wa Yanga haujatuma rufani hiyo!
Acha waandike kuwa CAF imewapongeza kwa kushinda rufani, kwa sababu habari kama hizo za kuuza magazeti hazina madhara kwa mahusiano ya Yanga na TFF. Lakini msiwaache waandike kauli za kupotosha za viongozi wenu zenye majisifu na kejeli.
Kama kauli hizo zinatolewa kweli na viongozi wenu, basi, viongozi hao waache kuendelea kuzitoa kwa hoja niliyoitoa awali na kama viongozi hao wanalishwa maneno na magazeti hayo, basi, wakanushe kwa nguvu zote habari hizo zinazoimarisha mgogoro baina ya Yanga na TFF.
Nawaomba sana wana Yanga wazingatie niliyowashauri kwa kulimaliza suala hili kirahisi na kirafiki.Si vibaya tukikumbushana kuwa vyombo vya soka vya kimataifa vina mawasiliano ya moja kwa moja na vyombo vya kitaifa kama TFF ya Tanzania na vinaviamini sana vyombo hivyo.
Asiyekubaliana nami katika hilo atazame jinsi suala la Ismail Aden Rage lilivyoshughulikiwa.Katika hili la Yanga, vyombo hivyo vya kimataifa vikielezwa na TFF kuwa Yanga haikupeleka timu uwanjani, taarifa hiyo itakuwa ya kweli kwa aslimia zote tofauti na kesi kama ya Rage ambayo taarifa yake toka TFF inaelezwa kutiwa chumvi kidogo.
Kwa sasa Yanga ijikite zaidi katika maandalizi ya Ligi Kuu ya msimu huu na matarajio yao kwenye ligi hiyo kuliko leo kusema haitakuwa tayari kushiriki mashindano ya ‘njaa njaa’ kama ya Kombe la Kagame na hapo hapo kusema wanakata rufani ili warudishiwe haki yao ya kushiriki mashindano hayo!
Huu si wakati muafaka wa kauli za kejeli kejeli na vijembe.Tukumbushane tena; ulimi uliotulia unatengeneza kichwa chenye busara.
Toa maoni yako