UKITAKA kuukata na kuuangusha mbuyu usianze kufikiria unene wake. Wiki iliyopita, jirani zetu Zambia wamefanya maajabu ya soka. Vijana wa Chipolopolo wametwaa ubingwa wa Afrika kwa kuwafunga Ivory Coast.
Ndio, jirani zetu Zambia wametuhamasisha.
Siri ya ushindi wa Zambia?
Ni Uzambia. Ni utaifa. Ni uzalendo. Tuliwaona vijana wa Chipolopolo wanaojituma uwanjani. Vijana waliokuwa tayari kufia uwanjani, vijana kama akina Kampamba, Mulenga, Sunzu, Nkausu, Chansa na wengineo.
Na katika maisha, ili mwanadamu ufanikiwe unahitaji kuwa na ‘ K’ tatu; Kujitambua, Kujiamini na Kuthubutu.
Vijana wa Chipolopolo wamejitambua. Wameijua historia yao. Wamejua walikotoka. Wamejua, kuwa kuna baba zao, mwaka 1993 walikuwa njiani kwenda Senegal kucheza mechi muhimu kufuzu kutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Dunia. Usafiri ulikuwa mgumu. Walipanda ndege ya jeshi. Ndege ilianguka pwani ya Gabon, wachezaji wote 18 walipoteza maisha. Walikufa kwa ajili ya nchi yao.
Ndio maana kule Gabon , kwa kuitambua historia hiyo. Wazambia wale waliingia uwanjani wakiwa tayari kufia uwanjani kwa ajili ya nchi yao. Tulimwona beki Joseph Mussonda akiumia vibaya. Alijikaza kuendelea. Ikaonekana haiwezekani kabisa. Akatolewa nje. Alitokwa na machozi kwa muda mwingi. Si kwa maumivu ya mguu tu, ni kwa kuona uchungu wa kukosa kuwa uwanjani kuipigania nchi yake. Huo ni moyo mkubwa wa uzalendo. Wazambia wale hawakuwa wakifikiria posho zao, bali taifa lao. Na hakuna ahadi yoyote ya fedha waliyopewa kabla ya mechi hivi karibuni.
Ndio, Wazambia wale walionyesha kujiamini sana. Walicheza mpira wao. Walikuwa focused muda wote. Hawakujali majina makubwa kama ya akina Drogba, Kolo Toure, Yahya Toure, Koite, Gervinjo, Gosso Gosso na mengineyo. Hawakujali kama walicheza na nyota wanaovichezea vilabu vikubwa huko Ulaya.
Chipolopolo walicheza mchezo wao. Mwanzo hadi mwisho. Hata pale Ivory Coast walipokuwa wakijaribu kubadilisha mbinu na hata kubadilisha nafasi za wachezaji uwanjani, bado Zambia waliendelea kucheza mpira wao.
Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa jirani zetu wa Zambia. Na mmoja wa watembeleaji wa mtandao wangu wa http://mjengwablog.com ana haya ya kusema; “Mimi tangu awali niliwapa nafasi kubwa Zambia kushinda mechi ile.
“Nilibishana sana na wanahabari wenzangu tukiwa Dodoma. Wapo waliokubaliana na maelezo yangu, lakini wengine wakawa wabishi kwa sababu ya ubishi tu. Nilisema awali kuwa, Zambia walikuwa wakionekana wako imara na wana dhamira ya kweli. Kuwatoa Ghana lilikuwa somo tosha kwa mtu anayejua mpira kutambua kuwa Wazambia hawakuwa wachovu. Kama ulivyosema, zile K tatu ziliwasaidia sana.
Pili, nilisema Ivory Coast wangefungwa kwa sababu wanacheza Ulaya (mpira wa draft). Wamekutana na Waafrika halisi wanaocheza mpira wenye vionjo na vitu adimu uwanjani. Ulaya mchezaji akiwa na mpira utajua atacheza vipi, kwa Afrika ni tofauti. Waafrika wanacheza mpira wenye ladha.
Tatu, nilisema Ivory Coast wangekuwa na hadhari kubwa ili wasiumie kwa sababu wanachezea timu kubwa zenye kuwalipa mabilioni ya fedha. Kwa Zambia, huo ulikuwa wakati wao wa kuonyesha vipaji vyao ili ikiwezekana watazamwe na ma-scout wa Ulaya kwa ajili ya kucheza huko. Kumbuka kuwa ni mchezaji mmoja tu wa Zambia aliyekuwa akicheza ughaibuni.
Zaidi ya yote, kilichowasaidia Zambia ni nidhamu. Hapa kwetu Tanzania mtu akishapata umaarufu, basi atafuatwa na mashangingi kibao, msimu mmoja anakuwa ameshakwisha kabisa. Tumepata mengi ya kujifunza kwa ndugu zetu Wazambia ambao kimaumbile ni kama sisi. Wanakula ugali wa mahindi kama sisi. Sasa tuamue kufanya kweli.”
Naam, kama Zambia wameweza, kwa nini sisi tushindwe?
Toa maoni yako