Michezo
Zambia: Wakati wake, maana yake
Ezekiel Kamwaga
Toleo la 226
15 Feb 2012

NYUMA ya mafanikio ya safari ya timu ya taifa ya Brazil kuja kucheza mechi ya kirafiki na timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) mwaka juzi ilikuwa ni kampuni moja iitwayo Kentaro.

Kampuni hii ndiyo kila kitu kwa Brazil. Yenyewe ndiyo inatafuta mechi za kirafiki za kimataifa za taifa hilo na yenyewe ndiyo kwa ujumla huingia dili kuhusu mengi ya mambo yanayohusiana na timu hiyo.

Kwenye mechi ile pekee, Brazil ilitengeneza walau shilingi za kitanzania bilioni mbili. Kimsingi, kwa mujibu wa makubaliano kati ya Kentaro na Chama cha Soka cha Brazil, timu yoyote inayoomba mechi na Brazil ni lazima iweke mezani walau dola za Marekani milioni 1.5.

Huu ndiyo udalali uliopo kwenye soka. Na hii ndiyo dunia ambayo timu ya soka ya taifa ya Zambia (Chipolopolo); mabingwa wapya wa soka wa Afrika, itaingizwa katika siku chache zijazo.

Nafahamu kwamba katika wakati huu ambapo kila mtu anafikiria kuandika makala kuhusu ni kitu gani ambacho Watanzania wamejifunza kutokana na ushindi huo wa Zambia, nimeona ni vema nikaenda katika maeneo ambayo wengi wetu hatuyatazami kwa mapana yake.

Jambo la kwanza ni kwamba siku chache zijazo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), litatoa orodha yake ya timu bora za soka duniani na ninatabiri kuwa kiwango cha Zambia kitapandishwa.

Kwa sasa, Zambia ni ya 16 kwa kiwango barani Afrika (ya kwanza ni Ivory Coast) huku ikishika nafasi ya 71 duniani. Kupandishwa kwa kiwango kwa Zambia kutakuwa na faida kubwa mbili.

Kwanza, sasa akina Kentaro watakuwa na sababu ya kuitafutia Chipolopolo mechi za kirafiki. Nani atakataa kucheza mechi za kirafiki na timu ambayo ndiyo mabingwa wa Afrika?

Kwa hiyo Zambia itapata mechi nyingi za kirafiki kuliko kawaida na zote hizo zitamaanisha kuna fedha zitaingia. Pili, wachezaji wa Zambia sasa watapata bahati ya kupata mechi na timu kubwa za soka duniani (England, Brazil, Hispania, Ujerumani na nyinginezo).

Hili litawatambulisha zaidi kisoka kwa mawakala wa wachezaji. Ndiyo maana nina imani kuwa wachezaji kama Rainford Kalaba, Stopira Sunzu na Emmanuel Mayuka watapata timu nzuri Ulaya kabla mwaka huu haujakwisha.

Kimsingi, wachezaji watafaidika lakini pia nadhani huu ndiyo wakati ambapo mabosi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), watafaidika pia kifedha.

Kwenye mechi yoyote ile ya kimataifa, wanaoingia ‘dili’ ni “wenye mpira” wenyewe kwa maana ya FA. Hawa ndiyo wanaozungumza na Kentaro. Katika majadiliano hayo, kabla mechi haijachezwa, kila mtu anajua atapata ngapi.

Kama kuna mechi imepangwa kufanyika London kati ya Zambia na Argentina, ni lazima akina Kalusha Bwalya watakuwa wanajua nini kitaingia mfukoni mwao kabla hata mechi haijachezwa.

Wachezaji watapata posho yao ya mechi kama kawaida. Na wale ambao hawajawahi kusafisha macho Ulaya, sidhani kama watajali sana. Hata hivyo, kama watacheza vizuri, wanajua kuwa mawakala kama Pini Zahavi na Kia Joorabchan watakuwa uwanjani wakiwatazama.

Ukicheza vizuri tu, bai bai Zambia.

Kitu kingine ambacho kitatokea Zambia ni kuondoka kwa kocha wao, Herve Renard. Wengi wa makocha wa kigeni wanaokuja barani Afrika hufanya hivyo kwa kutafuta kujenga CV zao tu. Wanazitumia nchi za kiafrika kutafuta mikataba ya kufanya kazi Ulaya na Uarabuni.

Mara baada ya Chipolopolo kutwaa ubingwa, jina la Renard litakuwa kama keki midomoni mwa watu. Matajiri wa Uarabuni, Asia na Ulaya wataanza kumtolea macho. Kwa fedha ambazo watamwahidi, sidhani kama atabaki tena Zambia.

Milovan Rajevac aliipeleka Ghana mpaka robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka juzi na kisha akaikimbia baada ya kupata ofa Uarabuni. Henry Kasperczak alifanya hivyo kwa Mali kwenye miaka ya 1990.

Baada ya kuifikisha Zambia kwenye Robo Fainali ya kombe hilihili miaka michache iliyopita, Renard huyuhuyu aliiacha Zambia na kwenda zake Angola kufaidi fedha za mafuta.

Kwa bahati mbaya, Angola haikumkubali na ndiyo maana karudi tena Zambia. Huyu hawezi kukataa fedha za waarabu wakimfuata. Ni vema jirani zetu hawa wakaanza mapema mipango ya kutafuta kocha mwingine.

Jana nilikuwa na mazungumzo marefu tu na Felix Sunzu mchezaji mahiri wa Simba ambaye mdogo wake, Stopira, aliifungia Chipolopolo bao la ushindi la penalti lililopeleka kombe Zambia.

Katika mazungumzo yetu, nilimtania kwamba kuanzia sasa jina la Sunzu litakuwa keki Ulaya. Na kwa vile Sunzu hawa wanapishana miaka miwili tu, nadhani siku za Felix Tanzania zinahesabika.

Wazungu wanawasajili Waghana na Wanigeria kwa sababu ya historia ya wachezaji wazuri waliotoka katika mataifa hayo siku za nyuma. Kama Kalaba wa Zambia angekuwa raia wa Ivory Coast, leo hii angekuwa anacheza Ligi Kuu ya Ufaransa au kokote Ulaya zamani sana.

Kwa ushindi huu wa Zambia, mawakala sasa watavamia katika taifa hili masikini. Na kwa vile hawajui mambo mengi kuhusu wachezaji –kwanza wataanza kuangalia majina tu…. Kama unaitwa Sunzu au Kalaba, moja kwa moja utapandishwa ndege kwenda walau Ubelgiji au Uzbekistan.

Kama huwezi kuwapa watu keki, basi wape mkate…. Kama huwezi kuwapa Kalusha Bwalya, kwanini usiwape nani sijui ili mradi uwaambie anatoka Zambia kwa akina Bwalya?

Miaka sita iliyopita, niliwahi kusafiri kwenda ughaibuni Ulaya na kuna jambo sijawahi kulisahau hata leo. Nilikuwa na rafiki yangu raia wa Nigeria na mara baada ya Wazungu kutuona walituuliza sisi ni raia wa wapi na wakati mwenzangu alipowaambia nchi anayotoka, swali lao la kwanza lilikuwa, je unaweza kucheza soka.

Nilipowaambia kuwa mimi ni Mtanzania, walifurahi lakini waliniuliza kama naweza kukimbia kama Juma Ikangaa…. Nikacheka tu.

Natarajia kuwa mapokezi ya Zambia yataongozwa na Rais Michael Sata ‘King Cobra’ mwenyewe. Na kwa vile yeye ni mlokole, ni lazima atatangaza namna alivyouota ushindi huo kabla hata michuano haijaanza.

Mtasikia mengi sana kutoka Zambia. Cha kujifunza? Ya nini. Taifa letu ni la watu wa kujifunza kutoka kwa wengine kila siku. Hata kama ni shule, basi siku moja si tu-graduate basi? Kujifunza tu kila siku?

 

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ezekiel Kamwaga
+255-718814875

Mwandishi ni Msemaji wa Timu ya Soka ya Simba

Maoni ya Wasomaji

hhahahahhahaha hagraduet mtuu hapa si tulisha DISCO

haah..tu graduate halafu ndo tuache kusoma? hapana sisi tutaendelea tu kujifunza kutoka kwa wenzetu tena kinadharia tu hmna ku graduate...tunapenda kujifunza.na ndo maana tunauliza tanzania inajifunza nini? hatusemi tanzani inafundisha nin.nchi yenyewe hii kutwa twadai changa.hii hatari sana.

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.