Habari
Zitto, Bomani, John Cheyo kuunda Kamati ya Madini
Mwandishi Wetu
Toleo la 003
14 Nov 2007

JAJI mstaafu Mark Bomani na wabunge Zitto Kabwe, John Cheyo, Dk Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige wametangazwa kuwamo katika Kamati mpya ya kupitia sekta ya madini.

Taarifa ya Serikali iliyosambazwa jioni jana tukienda mitamboni iliwataja wanakamati wengine kuwa ni Peter Machunde kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam, David Tarimo wa PriceWater House na Maria Kejo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.

Wengine wanaounda kamati hiyo ni Salome Makange wa Wizara ya Nishati na Madini, Mugisha Kamugisha wa Wizara ya Fedha na Edward Kihundu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadidu za rejea za kamati hiyo ni kupitia mikataba yote ya madini na nyaraka mbalimbali zinazohusiana na migodi nchini.

Kuundwa kwa kamati hiyo kunafuatia kauli ya hivi karibuni ya Rais Jakaya Kikwete kuwa angeunda kamati yenye mchaganyiko wa watu kufanya tathmini ya mikataba na masuala yote yanayohusiana na utajiri mkubwa wa madini.

Kuingizwa kwa Zitto katika kamati hiyo kunatokana na kuwa ndiye aliyeibua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge alipohoji mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, unaomilikiwa na Barrick Gold, hoja iliyomponza hadi kusimamishwa ubunge.

Kwa upande wake, Cheyo ni kiongozi wa UDP, chama ambacho mbali ya kuwa na nguvu kubwa Kanda ya Ziwa, ni chama pekee kilichowahi kuunda tume kuchunguza matukio ya maafa katika mgodi wa Bulyanhulu, tume iliyoongozwa na Steven Mhuli.

Cheyo pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kamati ambayo imekuwa ikifuatilia kwa kina mapato katika sekta ya madini. PAC ikiwa chini ya Hamad Rashid ilichunguza mapato katika mgodi wa almasi wa Williamson Diamond wa Mwadui mkoani Shinyanga na hatimaye kwenda hadi Uingereza, kufuatilia Kampuni ya Tansort inayochambua almasi,hoja ambayo inawaweka katika sahani moja Hamad na Cheyo. Hata hivyo Hamad yuko nje ya nchi kwa matibabu.

Uteuzi huo umeelezwa kuwa ni utekelezaji wa haraka wa ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete, katika hotuba yake nzito aliyoitoa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa CCM, Kizota, Dodoma kiasi cha wiki tatu zilizopita. Katika mkutano huo, Rais Kikwete aliahidi kuunda kamati mpya ya madini ambayo itahusisha makundi yote ya kijamii ili kuifanya iunganishe nguvu na imani kwa jamii kwa maslahi ya Taifa.

Kamati hiyo itatakiwa kushauri marekebisho yanayostahili kufanywa katika mikataba hiyo, ili iweze kuinufaisha zaidi nchi kuliko ilivyo sasa ambapo mikataba mingi inawanufaisha zaidi wawekezaji katika sekta hiyo.

Alisema kamati pia itaangalia na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kisheria katika mikataba ya madini, eneo ambalo limezua mjadala mkubwa kwa wananchi na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Rais Kikwete alisema sekta ya madini nchini inakabiliwa na upungufu katika baadhi ya vipengele vya mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa madini na ana lengo la kuifanyia marekebisho makubwa ili kuwanufaisha Watanzania badala ya hali ilivyo sasa kwa wawekezaji kuwa ndio wanaonufaika zaidi. Sekta ya madini nchini inakuwa kwa kasi na inavutia wawekezaji barani Afrika na ina fursa kubwa ya kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa kwa fedha za kigeni, ingawa hadi sasa mchango wake bado ni mdogo sana ukiwa ni sawa na asilimia 1.9.

Rais alisema katika mikataba ya madini kumekuwapo na kipengele cha kumlinda mwekezaji iwapo anapata hasara kwa mtaji kwa kile alichodai kuwa, iwapo atashindwa kufidia gharama zake za uwekezaji hasara hiyo huhamishiwa mwaka unaofuata.

“Wawekezaji hupewa nafuu ya asilimia 15. Maana ya kipengele hicho ni kuwa, mwekezaji atachelewa kuilipa Serikali kodi ya mapato na inawezekana asilipe kabisa katika uhai wa mgodi wake,” alisema Kikwete.

Alisema kuwa pamoja na nia njema ya kuvutia wawekezaji, sheria hiyo ilijali kumlinda mwekezaji asipate hasara na ikasahau kumlinda Mtanzania anayepata hasara ya dhahabu yake inayochukuliwa kwa ajili ya kufidia hasara anayopata.

Rais alisema kwamba lazima mkataba ulinde pande zote mbili ili zinufaike sawa. Aliongeza kuwa baada ya kuzungumza na baadhi ya makampuni yamekubali kifungu hicho kiondolewe na kubaki na mfumo wa msingi uliopo kwenye sheria.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako